HOTUBA
YA RAIS KIKWETE HAIKUWATENDEA HAKI WATANZANIA, HAIKUITENDEA HAKI TUME
YA MABADILIKO YA KATIBA, HAIKUMTENDEA HAKI JAJI JOSEPH SINDE WARIOBA.
Hakuja kama Rais wa nchi kuhutubia bunge la kihistoria lenye
mchanganyiko wa watanzania wa makundi, mitizamo na itikadi tofauti,
amekuja kama Mwenyekiti wa chama, kuhutubia mkutano mkuu wa CCM,
tumeisikiliza hotuba yake iliyokuwa na lengo la kuwatisha wananchi kuwa serikali tatu zitaleta vita na matatizo makubwa.
Kwa bahati mbaya, katika mchakato huu wa katiba binafsi nilishasema
interest yangu siyo muungano, na mara kadhaa nimesema kwamba hata kama
tukiwa na serikali 10, 3, 2 au 1, sioni kama ina uhusiano wowote na kina
mama wanaolala lundo mahospitalini na wala haina uhusiano na baba yangu
kupata chakula cha usiku au kulala njaa.
Kilichonikitisha sana
ni kumuona mkuu wa nchi akiweka msimamo wa chama chake katika baadhi ya
masuala muhimu na zaidi akitumia muda mwingi kuichambua rasimu na
kuelekeza namna sahihi inavyopaswa kuwa. Kwa mtizamo wangu, Rais
hakupaswa kuichambua rasimu mbele ya wajumbe na kuchukua upande katika
jambo hilo.
Ikiwa Rais ana misimamo yake katika rasimu hii,
anapeleka ujumbe kwa wajumbe wa bunge la katiba kufuata upande wake, na
kwa sababu wengi wa wajumbe si weledi na wachambuzi wazuri wanaweza
kuibeba hotuba yake na kufuata kile walichosema.
Ikumbukwe
kuwa, Rais Kikwete kama mkuu wa nchi ndiye aliyeanzisha mchakato huu na
ameuunga mkono kila ulipokwama. Leo mchakato umefika mahali ambapo
wajumbe wanapaswa kutulia na kuamua bila vishawishi vya wenye mamlaka na
kwa bahati mbaya mwenye mamlaka anakuja na msimamo. Na kisha anawaeleza
wajumbe waamue wakati ameshawapa msimamo.
Kwa mtizamo wangu,
Rais wetu alikuja kufanya kazi kubwa ya kuponda mawazo thabiti ya Jaji
Warioba, Salim Ahmed Salim, Dr. Mvungi(marehemu), Profesa Baregu na
wazalendo wengine wengi sana ambao wanaijua nchi hii vizuri mno lakini
kwa matakwa ya hali tuliyomo walilazimika kuweka pembeni misimamo yao na
kuja na rasimu ya wote. Rais anapoipondaponda rasimu husika ina maana
ya kukanyaga kazi kubwa ya tume na kuyasaga maoni ya wananchi kwa imani
ya chama chake.
Laiti kama Jaji Warioba na wenzie wangelijua
kitakachotokea leo, nina hakika wangekataa kutumika kufanya kazi kubwa
sana ambayo inakuja kutupwa jalalani na aliyewatuma.
Rais
alipaswa kujua kuwa anahutubia taifa ambalo lina mawazo tofauti mno, na
bunge ambalo lina mitizamo tofauti. Kuja na hotuba ambayo ina misimamo
ya chama chake ni kudharau sana kundi kubwa la watanzania wenye misimamo
tofauti, kwa sababu aliahidi kuwa katiba ya sasa inaandikwa na utashi
wa wananchi wenyewe ni vema angeacha kuweka misimamo ili kusaidia
wananchi na hata wajumbe wa bunge la katiba kufikiri kwa uhuru mpana.
Hivi sasa najiuliza maswali yafuatayo; kama Rais, chama chake na
serikali yake wana misimamo thabiti katika baadhi ya masuala, kwa nini
alikubali wananchi watoe mawazo yao? Na kwa nini wananchi wanatoa mawazo
halafu Rais anasema ni wachache? Je alifanya juhudi za kuielekeza tume
iwasiliane na wananchi milioni 20? Je aliipa fedha na uwezo wa kuchukua
maoni ya wananchi milioni 20 ili SAMPLE (sampuli) imridhishe?
Na kama Rais anadharau sampuli iliyotoa mawazo juu ya muundo wa muungano
kuwa ni ndogo mno kuwakilisha mawazo ya taifa, iweje aunge mkono
mapendekezo mengine ya Rasimu ambayo pia yametolewa na wananchi
wachache? Kwa mfano(siyo ripoti ya tume); kwa nini wananchi 17,000
wapendekeze masuala ya uwepo wa tume huru ya uchaguzi na jambo hilo liwe
jema kwa Rais lakini 17,000 haohao wakipendekeza serikali tatu iwe
sampuli ndogo kwa Rais(ni mfano si takwimu sahihi).
Kwa hiyo
baada ya Warioba na wenzie kutumia zaidi ya miezi 20 wakitoka jasho,
alikuwa anasubiri kuwakomesha leo? Lol, niseme nini zaidi?
Rais
ameeleza juhudi kubwa ambazo zimeshafanyika kuondoa kero zote za
muungano. Jaji Warioba alieleza juzi, hata akaunti ya pamoja ya muungano
imeshindikana kuanzishwa baada ya miongo kadhaa, mapendekezo ya tume ya
jaji nyalali, tume ya jaji Kisanga, tume ya Amina na wenzie
hayajatekelezwa hadi leo, Rais anawezaje kutulete "pipi ya kijiti"
kutuaminisha kuwa serikali mbili ndio muundo unaofaa? Hivi wale wataalam
na wazee walioishi na Mwalimu Nyerere kama kina mzee Butiku na wenzie
walikuwa wendawazimu kutoa napendekezo ya serikali tatu.
Rais
ameponda dhana ya kuweka masharti ya utekelezaji wa masuala ya kilimo,
rasilimali na mengineyo. Anasema haya hayapaswi kuwa katika katiba. Jaji
Warioba alieleza namna alivyokutana na wakulima wanaokufa masikini,
wakimueleza kuwa wanalima pamba kwa gharama ya shilingi 800 kwa kilo
moja halafu wakija kuuza wanapewa shilingi 600 pungufu ya shilingi 200
kwa gharama walizotumia kulima.
Warioba alieleza kuwa wakulima
wanateseka na lazima katiba mama ielekeze majukumu ya serikali
kuwahudumia wakulima, wafugaji, wafanyakazi n.k. Rais Kikwete anapuuza
maoni haya ya wakulima, anataka yaondolewe katika katiba ili chama chake
kipate fursa ya kuwatungia sheria au sera nje ya katiba ili kuilinda
serikali. Kuna dhambi gani masuala ya wakulima, wafanyakazi, wavuvi n.k.
yakiingizwa katika katiba?
Tanzania inatajwa kuwa na asilimia
80 ya wananchi wanaoendesha maisha kwa kutegemea kilimo. Kwa nini Rais
anakuja na wito wa kutotaja mahitaji muhimu ya afya, wakulima,
wafanyakazi n.k. katika katiba? Ni nini anachoogopa? Huu ni ujanja, huku
ni kukwepa uwajibikaji wa serikali kwa wananchi, Rais anataka katiba ya
kuongelea mfumo wa kugawana madaraka tu na vyeo(Msemo wa Kingunge).
Nihitimishe kwa kusema, bado taifa letu lina safari ndefu mno. Pole
Jaji Warioba, Pole Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Poleni Watanzania.
Tusikate tamaa, mapambano yanaendelea.
Mungu Ibariki Tanzania.
J. Mtatiro,
Mjumbe - Bunge Maalum la Katiba,
Dodoma.
Home
»
»Unlabelled
» JULIUS S MTATIRO:HOTUBA YA RAIS KIKWETE HAIKUWATENDEA HAKI WA TANZANIA! ....AMEKUJA KAMA MWENYEKITI WA CHAMA!
About Author
The part time Blogger love to blog on various categories like Web Development, SEO Guide, Tips and Tricks, Android Stuff, etc including Linux Hacking Tricks and tips. A Blogger Template Designer; designed many popular themes.
Advertisement
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post a Comment