Dodoma. Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), kimemuomba Rais Jakaya Kikwete, kuingilia kati na kukemea
vitendo vya kuingiliwa kwa uhuru wa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba
katika kufanya uamuzi.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Mkurugenzi wa
Mawasiliano na Mahusiano wa Chadema, John Mnyika, kufuatia hatua ya
Bunge hilo kuwa njia panda katika kuamua ama kutumia kura za wazi au za
siri katika kupitisha katiba.
Kauli hiyo ya Chadema inatokana na Kamati ya Kuandaa Kanuni za Uendeshaji wa Bunge hilo kushindwa kuafikiana.
Wajumbe wa CCM wanashikilia msimamo wa kura za wazi na wale wa makundi na vyama vya upinzani wakitaka kura ya siri.
Wajumbe hao wa makundi wanasema hayo ni matakwa muhimu ya kidemokrasia na kwamba yatawapa wajumbe uhuru wa kufanya uamuzi.
Akizungumza na gazeti hili mjini Dodoma jana,
Mnyika alisema kwa hatua ambayo suala hilo limefikia, ni vizuri Rais
Kikwete akaingilia kati na kuvitaka vyama vya siasa, makundi na taasisi
kuheshimu Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
“Tunatoa mwito kwa Rais Kikwete atumie hotuba yake
ya mwisho wa mwezi Februari, ambayo bado hajaitoa, kusisitiza vyama,
makundi na taasisi kuheshimu sheria hiyo kwa kutoingilia uhuru wa
wajumbe katika kufanya uamuzi,”alisema Mnyika.
Mnyika alisema ni muhimu Rais akafanya hivyo kwa
kuwa uteuzi wake wa wajumbe 201 uliacha shaka kwamba walioteuliwa ni
viongozi na makada wengi wa CCM ili kuongeza idadi ya wajumbe wanaoweza
kuingilia uhuru wao.
Mnyika pia amemsihi Rais Kikwete kutoa kauli juu
ya waraka wa CCM ili wajumbe wa CCM wafanye uamuzi uhuru wa kuzikubali
kura za siri.
Mnyika alisema endapo Rais hatachukua hatua hiyo sasa, Bunge Maalum la Katiba halitaweza kumaliza kazi zake ndani ya siku 70.
Alisema badala yake linaweza kumaliza kazi yake ndani ya siku 90 ikiwa njama za kuchelewesha hazitadhibitiwa.
Chanzo;Mwananchi leo
Chanzo;Mwananchi leo
Na Mjumbe Jr
Mbozi
Post a Comment