Dodoma. Uongozi wa Bunge Maalum umetuhumiwa kuwanyima wajumbe randama ya 2 ya Rasimu ya Katiba kwa makusudi, huku ukifahamu fika kuwa nyaraka hizo ni muhimu kwani zinachambua kwa kina masuala yanayoonekana kulikwaza Bunge hilo.
Akizungumza na Mwananchi mjini hapa leo, Mjumbe wa Bunge hilo anayewakilisha Vyama vya Wafanyakazi, Ezekiah Oluoch, amesema kuwa wao walipewa randama yenye muhtasari tu wa mapendekezo yaliyowakilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, ambayo haijitoshelezi.
“Kuna randama nyingine namba mbili, ambayo Mh. [Joseph] Warioba alituambia ametoa nakala 200.[Hii] ndiyo ina uchambuzi wa kina na majibu kwa maswali yote yanayotusumbua ndani ya Bunge hili,” alisema Oluoch.
Mjumbe huyo amesisitiza kuwa kama wasipopewa nyaraka hizo, anaamini kuwa masuala mbalimbali yanayolitatiza Bunge hilo, kama yale ya idadi ya serikali katika Muungano, yataendelea kuwagawa zaidi wajumbe.
Pamoja na hilo suala la randama, baadhi ya wajumbe pia wamelalamikia vigezo vilivyotumika kufanya uteuzi wa wajumbe 5 wataoingia katika Kamati ya Uongozi ya Bunge hilo Maalum, wakidai kuwa umelenga kukinufaisha chama tawala cha CCM.
Hali hiyo ilipelekea Mwenyekiti wa CUF, Ibrahim Lipumba, akatae uteuzi wake kwenye kamati hiyo ya Uongozi, akisema hayuko tayari "kutumiwa kama chambo," cha kuonyesha kuwa kamati "ina mwenyekiti mkubwa wa chama kikubwa cha upinzani."
Chanzo:Mwananchi
Mjumbe Jr
Post a Comment