| Profesa Mwesiga Baregu |
Kamishna wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Profesa Mwesiga Baregu ,
amesema Rais Jakaya Kikwete, alitakiwa kuieleza tume kasoro alizoziona
kwenye rasimu badala ya kutumia bunge la katiba kuikosoa.
Aidha, alishangazwa na hatua ya Rais ya kujibu maoni yaliyotolewa
kwenye rasimu ya katiba badala ya kutoa hotuba ya kuzindua bunge hilo.
Alisema huenda Rais alijisahau na kujifanya sehemu ya bunge na kwamba
maelezo aliyokuwa akiyatoa alitakiwa kuieleza tume hapo awali na sio
kutumia bunge kuishutumu.
“Rais amejishauri au ameshauriwa vibaya, alienda kulifungua bunge lakini kilichofanyika amelifunga,” alisema.
Alionya kuwa kama alitegemea angepanda mbegu ya maelewano na kuleta muafaka ndani ya bunge ametoa msimamo wake na chama chake.
Aliendelea kusema;“tulitegemea awaunganishe Watanzania badala yake
ametoa hotuba ya kuwatenganisha, hii itafanya wajumbe kila mtu awe na
msimamo wake. ”
Profesa Baregu alionya kuwa endapo katiba itakayotokana na matakwa ya Watanzania haitapatikana nchi inakaribisha migogoro.
Kuhusu serikali tatu, alimkariri Rais aliyewahi kusema hilo ni suala
linalozungumzika na kwamba hakuna kilicho tofauti na msimamo huo.
“Haya hata tume tuliyafikiria ndiyo maana tulipeleka mapendekezo,
lakini tamko la Rais ni matamko ya kichochezi na vitisho, je endapo
bunge likipitisha serikali tatu itakuwaje?” alihoji.
Mjumbe huyo wa tume ya mabadiliko ya katiba ambayo kisheria imemaliza
muda wake juzi baada ya uzinduzi wa bunge maalumu, alisema endapo
mchakato huo ukiharibika au kushindikana, nchi inaweza kuingia katika
mgogoro kwenye uchaguzi mkuu kama ilivyotokea Kenya.
“Rais ndiye mwenye dhamana ya kujenga maelewano anatakiwa kuwawezesha
Watanzania kupata katiba bora, vinginevyo tutangaze tunataka katiba ya
maoni ya Rais na chama chake?,” aliuliza.
Akichambua hotuba hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na
Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Hellen Kijo- Bisimba, alisema maelezo ya
Rais yamedhihirisha kuwa anaogopa muundo wa serikali tatu, ndiyo
sababu ya kutumia muda mwingi kuchambua suala hilo.
Mchungaji William Mwamalanga wa Kanisa la Kiinjili la Kipentekoste,
akizungumzia hotuba hiyo, alisema amejaa woga kuwa wapo watu wanaotaka
kuuvunja muungano.
“Kusema kama kuna watu wanataka kuuvunja wauvunje lakini si wakati
akiwapo ni woga na Rais amesahau kuwa yeye ni sehemu ya Watanzania au
atuambie atakwenda kuishi wapi?”
Alisema kama mkuu wa nchi anapaswa kuhakikisha hilo halitokei na si kuonyesha hofu.
Pia alisema hotuba yake imefuta kazi iliyofanywa na Tume na kuongeza rasimu nyingine jambo ambalo siyo msimamo wa Watanzania.
Pia alisema hotuba yake imefuta kazi iliyofanywa na Tume na kuongeza rasimu nyingine jambo ambalo siyo msimamo wa Watanzania.
“Mkuu wa nchi anapotoa au kueleza jambo huwa ni mwisho maana yake
aliyoyaongea yanatakiwa kuzingatiwa, ndiyo maana nasema amefuta rasimu
ya Tume, kama aliona kuna sababu ya kuwa na serikali mbili hapakuwa na
sababu ya kuwa na bunge hili,” alisema.
Aliwaomba viongozi wakuu kuondoa misimamo yao kwenye suala hilo nyeti na kuwaacha wajumbe wafanyekazi yao.
Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson
Bana, alisema maoni ya Rais Kikwete yasichukuliwe kwa hasira kwani
alikuwa akitoa maoni yake kama wananchi wengine walivyofanya.
Dk. Bana alisema maoni hayo yalitakiwa kutolewa kwenye tume, hivyo
maoni hayo yasichukuliwe kama ni muongozo wa upatikanaji wa katiba mpya
kwani kinachotakiwa ni hoja kujibiwa. Alisema endapo maoni hayo
yakitumika kama muongozo wa upatikanaji wa katiba mpya huenda bunge hilo
likatibuka jambo ambalo hawalitarajii.
Mhadhiri mwingine wa UDSM, Dk. Bashiru Ally, alisema bunge tayari
limeshapewa vitendea kazi hivyo ni wajibu wao kuyafanyia kazi. Alisema
Rais Kikwete ametoa hutuba nzuri na kwamba aliyokuwa akiyazungumza ni
yale ambayo yalikuwa kwenye tume, kazi ipo kwa wajumbe kuyafanyia kazi.
Kutoka Dodoma, mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter
Msigwa, ambaye ni mjumbe wa bunge hilo, alisema kinachofanyika bungeni
ni kuandika katiba ya mawazo, matakwa na msimamo wa CCM.
Akichambua hotuba hiyo alisema wajumbe watakuwa hawatungi katiba bali kuandika mawazo ya chama tawala.
Mbunge wa Viti Maalum (CUF) Mkiwa Kimwaga alisema Rais amekwenda
kuzindua kama Mwenyekiti wa CCM na si kama kiongozi wa kitaifa hivyo
hakufanikiwa kuwaunganisha wajumbe na Watanzania.
Aliikosoa hotuba hiyo kuwa ina vitisho akitaja mfano wa jeshi
kupindua nchi na kuonya kuwa hata kama bunge hilo litaendelea wajumbe
hawatatoa maoni kwa huru.
Imeandaliwa na Romana Mallya, Beatrice Shayo Dar, Emmanuel Lengwa na Jacqueline Massano, Dodoma
Imeandaliwa na Romana Mallya, Beatrice Shayo Dar, Emmanuel Lengwa na Jacqueline Massano, Dodoma
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
MJUMBE Sr
Post a Comment