Barcelona, Hispania. Nahodha wa klabu ya Barcelona, Carles Puyol amesema atavunja mkataba wake wa kuendelea kuitumikia klabu hiyo mwishoni mwa msimu huu.
Puyol (35) raia wa Hispania ana mkataba na klabu
ya Barcelona mpaka 2016, lakini amekubaliana na uongozi wa klabu hiyo
kuvunja mkataba huo mwishoni mwa msimu huu.
Tangu aanze kuichezea Barcelona mwaka 1999 katika
Ligi Kuu ya Hispania ‘La Liga’ na mashindano mengine. Puyol ameichezea
klabu hiyo katika mechi 593.
Akiwa na klabu ya Barcelona, Puyol ametwaa mataji
sita ya La Liga, mataji matatu ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na makombe
mawili ya ligi ya Hispania. Pia Puyol ameisaidia Barcelona kutwaa
ubingwa wa Uefa Super Cup mara mbili na Super cup ya Hispania mara sita.
Vilevile Puyol ameisaidia timu ya taifa ya
Hispania kutwaa ubingwa wa Ulaya mwaka 2008 na ubingwa wa dunia 2010
katika fainali zilizofanyika nchini Afrika Kusini.
Hata hivyo, baada ya fainali hizo za dunia Puyol
alianza kukumbwa na majeraha ya goti yaliyosababisha ashindwe kuwapo
katika kikosi cha Hispania kilichoshiriki katika mashindano ya Ulaya
2012.
“Baada ya kufanyiwa operesheni ya goti mara mbili
nimekuwa napata wakati mgumu kurudi katika kiwango ninachokihitaji ili
niweze kuichezea Barcelona. Kwa hiyo ndiyo maana nimeamua mwishoni mwa
msimu huu nitaondoka Barcelona,” alisema Puyol.
Alisema,”Imebakia takriban miezi mitatu kabla ya
ligi kumalizika msimu huu kwa hiyo nataka kwa muda huo niendelee kuwa
kwenye klabu ya Barcelona.”
Puyol, ambaye alicheza mechi ya 100 akiwa na timu
ya taifa ya Hispania Februari 2013 dhidi ya Uruguay, alisema amepanga
kupumzika kucheza soka atakapoondoka Barcelona.
“Lakini ukweli sijui nini nitakachofanya baada ya
Juni 30 wakati nitakapoondoka Barcelona, ila nina uhakika nitapumzika,”
alisema Puyol.
Alisema: “Natarajia nitafanya mkutano na waandishi
wa habari mwishoni mwa msimu huu baada ya kuitumikia klabu ya Barcelona
kwa miaka 19.”
Hivi sasa klabu ya Barcelona inashika nafasi ya
pili katika msimamo wa La Liga ikiwa nyuma kwa pointi moja kwa vinara wa
ligi hiyo, Real Madrid.
Source:Mwananchi
Source:Mwananchi
Na Mjumbe Jr
Mbeya
Post a Comment