WANAFUNZI wawili wa darasa la pili katika Shule ya Msingi Goba, Dar es Salaam, wamefariki dunia wakati wakiogelea.
Wanafunzi hao wametajwa kuwa ni Frank Charles (11) na Videson Peter (11), wote wakazi wa Goba.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura, alisema
kuwa tukio hilo lilitokea juzi, saa 5 asubuhi wakati wanafunzi hao
walipokuwa wakiogelea katika dimbwi la maji ya mvua.
Alisema wanafunzi hao ghafla walizama na kunywa maji mengi na kufariki dunia papo hapo.
Kwa mujibu wa Kamanda Wambura, maiti zote ziliopolewa na wananchi wa
eneo hilo na miili yao imehifadhiwa Hospitali ya Mwananyamala.
Wakati huohuo, Askari wa JWTZ kikosi cha Navy Kigamboni, Emmanuel
Kamugisha anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka kati ya 20 na 25,
amefariki dunia baada ya kugongwa na gari.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Englibert Kiondo, alisema ajali
hiyo ilitokea juzi, saa 7 mchana eneo la Mgulani, huko barabara ya
Kilwa na kuhusisha gari T 141 CVJ Dong Fen iliyokuwa ikiendeshwa na
Athumani Kibuda (48), mkazi wa Morogoro.
Alisema dereva huyo aliyekuwa akitokea Mivinjeni kuelekea Keko,
wakati akizunguka mzunguko wa Mgulani, aligongana na pikipiki T 428
CKU aina ya Fekon ikiendeshwa na askari wa JWTZ MT Florian Kamugisha
ambaye alikuwa amembeba abiria Emmanuel, wote ni askari JWTZ Navy
Kigamboni.
Alisema katika ajali hiyo, Florian alipata majeraha sehemu mbalimbali
mwilini na amelazwa hospitali ya Lugalo. Maiti imehifadhiwa hospitalini
hapo, na dereva wa gari hilo anashikiliwa na polisi.
MJUMBE sr
Post a Comment