
Mbunge Vicky Kamata akiwa amelazwa Hospitali ya Tabata General, Dar es Salaam jana. Picha na Florence Majani
Ni matukio nadra kutokea katika maisha, lakini haya ndiyo yaliyomkuta Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Vicky Kamata, baada ya kuugua ghafla saa 36 kabla ya harusi yake.
Kuugua kwa bibi harusi huyo mtarajiwa, kumezua gumzo katika Viwanja vya
Bunge mjini Dodoma na maeneo mengine nchini, kutokana na kile
kilichoelezwa kwamba harusi hiyo ilipangwa kuwa ya kifahari ikitarajiwa
kutumia Sh96 milioni.
Kamata ilikuwa afunge ndoa Jana katika Kanisa Katoliki Parokia ya Bikira
Maria Mama wa Mkombozi, Sinza Dar es Salaam na tayari kadi za mialiko
zilishasambazwa kwa watu mbalimbali wakiwamo wabunge.
Habari za kuugua ghafla kwa mbunge huyo ambaye pia ni msanii wa muziki aliyetamba na kibao chake cha ‘Wanawake na Maendeleo’ zilianza kuzagaa kwa kasi juzi jioni nchini.
“Niliugua tumbo ghafla, nilipata
maumivu makali sana nikampigia daktari wangu na nilipomweleza jinsi
ninavyojisikia, aliniambia niende hospitali haraka na kutokana na hali
ilivyo, waliamua nilazwe,” alisema Kamata akiwa kitandani katika hospitali hiyo.
Kamata alifafanua kuwa, pamoja na mambo mengine, hali yake ya ujauzitoimekuwa ikimsumbua na kuchangia yeye kulazwa kwa mara ya pili sasa katika kipindi cha wiki mbili.
Mbunge huyo ambaye alitakiwa kufunga ndoa Jana, alisema kuwa kutokana na
maradhi hayo, haelewi hatima ya ndoa yake, ingawa wanafamilia na
wanakamati wanaendelea na mipango ya harusi kama ilivyopangwa.
“Mama anaenda nyumbani sasa hivi
kuniandalia nguo na kila kitu, lakini sijui itakuwaje kwa sababu daktari
amesema kutokana na hali yangu ilivyo, itakuwa vigumu kuvaa viatu
virefu na kupata usumbufu wote wa purukushani za harusi,” alisema.
Vicky alisema wanakamati wa Dar es Salaam na wale wa Dodoma, wanaendelea
na vikao ingawa, wamechanganyikiwa kutokana na sintofahamu iliyopo,
kama harusi itafanyika au haitafanyika.
Ndugu wa mbunge huyo akiwemo mama yake mzazi Kamata walionekana
hospitalini hapo wakiendelea kumfariji na kujadili kuhusu hatima ya
harusi hiyo, iliyokuwa ikingojewa kwa hamu na wanafamilia wote.
Alisema pamoja na kumpa matibabu, walishauriana kuwa apumzike kwa siku tano ili kuhakikisha kiumbe kilichopo tumboni kipo salama.
“Ilikuwa ni uamuzi mgumu kwa sababu
ni siku yake ya harusi, lakini tunaangalia umuhimu wa kiumbe na kama
ataenda, itabidi asaini ili ijulikane kuwa hatukumkubalia. Kwa kifupi
hayuko fiti kwa shughuli hiyo,”alisema.
Harusi ya Kamata iliandikwa pia na mitandao mbalimbali ya kijamii nchini
na jana redio moja ilitangaza kuugua kwake, ikisema kumetokana na
matatizo ya ujauzito.
Kumekuwa na uvumi unaosambazwa kwa kasi juu ya sababu za kuahirishwa kwa
harusi hiyo, lakini kwa sababu ya maadili ya uandishi hatutaweza
kuziandika katika mtandao huu.
Padri wa Kanisa Katoliki Parokia ya Bikira Maria Mama wa Mkombozi ,
Sinza Dar es Salaam, Cuthbert Maganga alipohojiwa kuhusu taarifa za
kufungwa kwa ndoa hiyo, alikiri kwamba iliandikishwa ili ifungwe
kanisani hapo.
“Ilitarajiwa kufungwa Mei 24 mwaka huu
yaani kesho (Jana), lakini kwa taratibu za kanisa letu ilishindikana kwa
sababu bibi harusi alishindwa kuwasilisha cheti chake cha ubatizo, pia
hakuwa amepata kipaimara, vitu hivyo ni miongoni mwa vitu muhimu
vinavyohitajika ili kukamilisha Sakramenti ya Ndoa,” alisema Padri Maganga.
Juhudi za kumtafuta bwana harusi, Charles Gardner hazikuweza kufanikiwa
baada ya simu yake kuita bila kupokelewa, hata alipotumiwa ujumbe wa
maandishi hakuwa tayari kujibu.
MJUMBE Sr
Post a Comment