KIMENUKA! Beautiful Onyinye, Wema Isaac Sepetu na Mkurugenzi wa
Kampuni ya Five Effects, William Mtitu wamekwinda ‘live’ ndani ya gari,
Risasi Jumamosi lina kisanga kamili.
UWANJA WA VITA
Taarifa za uhakika zilieleza kuwa, tukio hilo lilijiri juzikati
maeneo la Bunju, Dar nyumbani kwa mke wa aliyekuwa mwigizaji na prodyuza
wa Bongo Movies, Adam Phillip Kuambiana wakati ndugu, mastaa na jamaa
walipokuwa wameweka matanga ya msiba.
Kwa mujibu wa chanzo makini kilichoomba kustiriwa gazetini, kisa cha
yote kilidaiwa kuwa ni Mwenyekiti wa Bongo Movie Unity, Steven Mengere
‘Steve Nyerere’ kueneza sumu kwa mastaa kuwa wawachunie Mtitu na
mwigizaji Jacob Steven ‘JB’ ambao alitofautiana nao msibani hapo.
TUJIUNGE NA CHANZO
“Steve alipishana kauli na JB, Mtitu akaingilia, sasa Steve akamwaga
‘sumu’ kwa wasanii wengine ambao ghafla walianza kuwachunia JB na Mtitu
msibani hapo,” kilisema chanzo.
MTITI WAIBUKA
Chanzo hicho kilizidi kudai kuwa, Mtitu, baada ya kuchuniwa huko na
wasanii wengine, kuna wakati alikuwa kwenye gari na kutaka kupishana na
gari la mwigizaji Aunt Ezekiel ambalo ndani yake alikuwemo Wema, mtiti
ukaibuka.
“Aunt alishusha kioo na kumuuliza Mtitu umemfanya nini Steve? Wakati
Mtitu akitaka kumjibu juu ya kile kilichotokea, dada mkubwa au mama la
mama (Wema) akaununua ugomvi usiomhusu,” kilitiririka chanzo.
KIHEREHERE CHA WEMA CHAANZISHA MTITI
Chanzo hicho bila kupepesa macho, kiliweka bayana kuwa, Wema alindandia kauli ya Aunt na kumwambia Mtitu ni mtu asiyempenda.
“Wema alisema katika watu ambao hawapendi duniani, Mtitu ndiyo namba
moja ndipo hapo uvumilivu ulipomshinda Mtitu na kushuka kwenda kumvaa
Wema.
“Alipofika aliingiza mkono kupitia upenyo mdogo ulioachwa katika
dirisha, akafungua loki ya mlango na kumkalia Wema mapajani huku
akimkwida shingoni.
“Wema naye akajibu mapigo kwa kumkwida Mtitu huku akiporomosha maneno
machafu (hayaandikiki gazetini) ndipo Mtitu alipoonesha uanaume na
kumpa maneno ya kuashiria atampa kipondo ambacho hajawahi kukiona
maishani mwake,” kilisema chanzo.
AUNT AOKOA JAHAZI
Ilidaiwa kuwa, baada ya Wema kutaitiwa vilivyo na Mtitu, Aunt ilibidi
aingilie kati na kumuomba Mtitu amsamehe bure na amuondoe shetani eneo
hilo.
“Aunt alimuomba sana Mtitu kuwa amuachie Wema kwa kumsihi kuwa yeye
wanaheshimiana sana, Mtitu akamuachia na kushuka ndani ya gari huku
akimtahadharisha Wema kuwa asije akarudia kuingia kwenye kumi na nane
zake,” kilizidi kumwaga data chanzo.
WAO WANASEMAJE?
Baada ya kujiridhisha na chanzo hicho, wanahabari wetu walianza
kuwasaka wahusika ambapo wa kwanza alikuwa ni Wema ambaye simu yake
iliita bila kupokelewa (anaweza kututafuta akiisoma habari hii).
Baada ya Wema kutopokea, mapaparazi wetu walimgeukia Mtitu ambaye
alijibu kwa kifupi kisha akakata simu na alipopigiwa tena, hakupokea:
“Mimi sipendi mambo ya kijinga, mtu hawezi kuingilia visivyomhusu nikamuangalia tu.”
Jitihada za kumpata Aunt ziligonga mwamba baada ya simu yake ya kiganjani kuita bila kupokelewa.
@Sr

Post a Comment