
Aliyekuwa
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba
amewashauri viongozi wazee na waliokaa madarakani muda mrefu kuacha
kung'ang'ania madaraka.
Amesema
kuwa ni vyema kwa viongozi hao kung'atuka ili kutoa nafasi kwa vijana
wenye nguvu na akili kulitumikia taifa katika uongozi.
Warioba
aliyasema hayo juzi jijini Dar es Salaam katika mahojiano maalumu na
gazeti hili, pamoja na mambo mengine alizungumzia uongozi wa nchi hii.
"Mwalimu
Julius Nyerere aling'atuka akiwa na nguvu zake kabisa. Kiasili
kung'atuka ni dhana ya kuwapisha vijana kuwa mbele katika kutekeleza
majukumu na ninyi wazee siyo kuondoka, bali kuendelea kuwapa ushauri na
mwongozo,"alisema Jaji Warioba.
Alieleza
kuwa kung'atuka kunamfanya aliyechukua hatua hiyo kuishi maisha ya raha
yenye furaha na amani jambo ambalo yeye sasa analifurahia.
Aliongeza:
"Haiwezekani mzee ukakaa kundi moja na kijana wako aliyetahiriwa juzi,
kwani kwa kawaida, kijana akitahiriwa hupandishwa daraja na kukaa kundi
la wakubwa, hapo wewe baba yake hata kama una miaka 40, unahamishwa na
kuingia kundi la wazee."
Alifafanua
kuwa hata katika uongozi ni muhimu kung'atuka na kuwapisha vijana ili
waweze kutumia akili na nguvu zao kuendeleza taifa huku wakipata
maelekezo na mwongozo kutoka kwa wazee.
"Maisha
yangu sasa baada ya kuacha uongozi ni ya furaha na amani bila woga
kuliko wakati wowote, tofauti na nilipokuwa bado kiongozi katika
Serikali," alisema.
"Ukiwa
kiongozi unaweza kuishi kwa hofu na shaka huku ukituhumiwa," alibainisha
Jaji Warioba aliyewahi kuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais
mwaka 1985 - 1990.
Kauli ya
Warioba imekuja huku kukiwa na kundi kubwa la viongozi wenye umri mkubwa
katika nafasi mbalimbali madarakani muda mrefu, huku wakiendelea
kutamani nafasi za juu zaidi. Miongoni mwa viongozi hao, wapo wanaotajwa
kuunda makundi ya kusaka urais wa Tanzania katika uchaguzi mkuu ujao
mwaka 2015.
Hii siyo mara ya kwanza viongozi wenye umri mkubwa kutakiwa kung'atuka madarakani.
Januari
14, 2010, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, aliwashauri wazee watumie busara
kupima uamuzi wa kugombea tena nafasi za ubunge kwenye uchaguzi mkuu.
Pinda alitoa rai hiyo alipokuwa akijibu maswali ya wahariri katika
mkutano alioitisha kujibu maswali yao jijini Dar es Salaam.Alibainisha
kuwa kwa sasa Tanzania haina tena uhaba wa vijana wasomi na wataalamu wa
kuitumikia nchi yao katika nafasi mbalimbali.
"Nafikiri
Mkoa wa Rukwa umeonyesha mfano. Mzindakaya na Kimiti wametangaza
kung'atuka, nafikiri wazee wengine wafuate busara hiyo," alisema Pinda.
Dk Chrisant Mzindakaya alikuwa Mbunge wa Kwela na mwenzake, Paul Kimiti alikuwa Mbunge wa Sumbawanga Mjini.
Alisema
kuwa rai ya kutaka wazee kung'atuka madarakani ina mambo mawili, ikiwamo
kupumzika kwa watu waliokaa madarakani kwa muda mrefu na kwa watu walio
na umri mkubwa.
Warioba
alisema mtazamo wake ni vyema kuwa na ukomo wa mtu kuwa mbunge, ambapo
alipendekeza vipindi vitatu vya miaka mitano mitano yaani miaka 15.
CHANZO MWANANCHI
CHANZO MWANANCHI
MJUMBE Sr
Post a Comment