ABIRIA 48 WA PRECISION AIR WANUSURIKA BAADA YA NDEGE YAO KUPATA HITILAFU IKIWA ANGANI!
Ndege ya Shirika la PrecisionAir iliyokuwa imeruka kwa safari zake kutoka Mwanza kwenda Nairobi nchini Kenya kupitia Kilimanjaro jana, imelazimika kutua kwa dharura baada ya kupata hitilafu ikiwa angani.
Taarifa zilizopatikana kutoka kwa baadhi ya abiria waliokuwamo ndani ya ndege hiyo namba 5H-PWC ATR 72, zilieleza kuwa tayari walikuwa wameruka lakini baada ya muda mfupi waliambiwa hawawezi kuendelea na safari kutokana na ndege kupata hitilafu.
Baada ya kuruka, ndege ilitaka kukunja magurudumu kwa ndani ikashindikana hali iliyomlazimisha rubani kuzunguka eneo la uwanja huo, huku akijaribu kuyarudisha bila mafanikio na kuamua kutua kwa dharura.
Alisema abiria 48 waliokuwa kwenye ndege hiyo hadi jana saa 12:00 jioni walikuwa wanasubiri nyingine ili kuendelea na safari.
Akizungumza kwa simu Meneja wa Uwanja wa Ndege wa Mwanza, Ester Madale alisema hitilafu hiyo ilikuwa ya kawaida hivyo haikuwa na madhara.
Madale alisema iliruka saa 7:54 mchana kwenda Kilimanjaro, lakini baada ya kuruka magurudumu yalishindwa kujikunja kurudi ndani hivyo rubani alijaribu kuyarudisha ikashindikana, hivyo akalazimika kutua kwa dharura.
“Hitilafu hiyo ni ya kawaida, wahandisi wetu waliangalia hitilafu hiyo na saa 9:15 alasiri walifanya majaribio kuirusha na imetua, hivyo siyo tatizo kubwa la kawaida,” alisema Madale.
Matukio ya karibuni
Desemba 13, mwaka jana ndege ya PrecisionAir aina ya ATR 42-600 ilipasuka magurudumu manne ya nyuma wakati ikitua uwanja wa KIA, miongoni mwa abiria waliokuwa ni Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa.
Julai 24, 2012 ndege ya shirika la PrecisionAir magurudumu yalipasuka wakati ikitua Uwanja wa Ndege mkoani Kigoma.
Credit:Mwanahabari Huru
Post a Comment