Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Haki za Binadamu cha (Legal and Human Right Center) Daktari Helen Kijo-Bisimba

Kwa siku kadhaa sasa, gazeti hili limekuwa likichapisha makala kuhusiana na madhila yaliyompata msichana mmoja mkazi wa Dar es Salaam, aliyepelekwa nchini China na mtandao wa watu wanaofanya biashara ya kusafirisha binadamu, lakini akaishia kutumikishwa katika madanguro mbalimbali badala ya kupewa ajira katika hoteli kubwa kama alivyokuwa ameahidiwa. Msichana huyo ambaye hatutamtaja jina kwa sababu za kimaadili sasa amerudi nchini akiwa ameathirika kimwili na kisaikolojia, baada ya kuwatoroka watu waliokuwa wamemrubuni na kumuweka utumwani kwa miezi mitatu hivi.

Msichana huyo ambaye kabla hajapelekwa utumwani nchini China alikuwa na matumaini ya mafanikio katika maisha yake. Hivyo, alipokutana na wanawake hao hapa jijini Dar es Salaam, ambao hakujua walikuwa sehemu ya mtandao wa wafanyabiashara ya kusafirisha binadamu hakuwatilia shaka hata kidogo, kwani aliamini walikuwa na nia ya kumsaidia kutimiza ndoto yake ya kupata ajira nzuri za kimataifa nje ya nchi. Hakuwahi kufikiria kwamba wanawake hao walikuwa wakimpeleka kudhalilishwa utumwani, bali pia kufanya kazi ambazo malipo yake yalikuwa yanakwenda moja kwa moja kutunisha mifuko ya wanawake hao na mawakala wao nchini China.
Ni simulizi zinazotia uchungu mkubwa ambazo zinathibitisha kwamba biashara ya usafirishaji wa binadamu imeshamiri hapa nchini, huku Serikali na vyombo vyake vya ulinzi na usalama vikionekana kutojua ukubwa wa tatizo wala wapi pa kuanzia. Pamoja na maumivu aliyonayo, msichana huyo anasema ameamua kujitokeza na kuzungumzia mkasa huo ili mamlaka husika za hapa nchini na za kimataifa ziingilie kati na kukomesha biashara hiyo ambayo anasema imewakumba wasichana wengi kutoka Tanzania ambao wengi wameshindwa kujikwamua.
Ni simulizi pia zinazoonyesha kwamba mifumo ya kiserikali na kiutawala hapa nchini haifanyi kazi kama ilivyotarajiwa kutokana na kuwapo janga la rushwa na ufisadi miongoni mwa watendaji wengi serikalini na taasisi zake. Tunajiuliza jinsi mitandao ya biashara hiyo inavyoweza kuwaweka watendaji hao mifukoni kiasi cha kutoa viza na pasi za kusafiria kwa vijana ambao hawana uwezo kifedha wala sifa za kupata ajira mahali popote. Inashangaza kuona mitandao hiyo ikifanya biashara hiyo kiulaini pasipo vyombo na mamlaka husika kushtuka.
Makala tulizochapisha kuhusu msichana huyo ndizo zimevishtua vyombo vya dola. Sasa tunaambiwa kwamba Shirika la Polisi la Kimataifa (Interpol), Tawi la Tanzania limemhoji msichana huyo kwa zaidi ya saa 11 likitaka kujua jinsi safari yake hiyo ilivyokuwa na namna wanawake waliowasafirisha kwenda China walivyosuka mipango hiyo. Ofisi hiyo ya Interpol imekiri kumhoji msichana huyo na kusema lengo ni kufahamu kwa undani jinsi Watanzania wanavyotumikishwa katika madanguro hayo, pamoja na kujua jinsi biashara hiyo inavyofanyika kati ya China na Tanzania.
Angalizo letu kwa Serikali ni kwamba iamke na kuchukua hatua, kwani biashara hiyo haiko tu kati ya Tanzania na China, bali kati yake na nchi nyingi za Kiarabu, Ulaya, Asia, Amerika na hata Afrika. Ni biashara kubwa inayoendeshwa na mtandao mpana wa genge la wahalifu wa kimataifa. Msichana huyo sasa anaishi kwa woga baada ya kutishiwa kifo na wanawake waliompeleka China na baadaye kutoroka na kurudi hapa nchini. Tumetiwa moyo na Tamwa pamoja na kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), ambavyo vimeanza kuchukua hatua za kumsaidia.