Unknown Unknown Author
Title: NEEWZ update:ESCROW MBIVU NA MBICHI JIONI YA LEO!!
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
Kutoka Dodoma: Mwenyekiti wa bunge Mhe.Hassan Zungu,ame ahirisha kikao cha bunge sasa mpaka jioni. Amethibitisha kuwa ripoti ya ESCROW m...

Kutoka Dodoma:
Mwenyekiti wa bunge Mhe.Hassan Zungu,ame ahirisha kikao cha bunge sasa mpaka jioni.

Amethibitisha kuwa ripoti ya ESCROW mpaka sasa imepokelewa bungeni na tayari ni public document.

Amethibitisha kuwa mpaka sasa hakuna barua rasmi ambayo bunge limepokea kama zuio la kutoijadili.


Endelea zaidi....
Kila Mtanzania anangoja kusikia mbivu na
mbichi ndani ya Ripoti ya Escrow kwa mujibu
wa uchunguzi wa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa
Hesabu za Serikali (CAG) pamoja na Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru)
kisha kuwekwa pamoja na Kamati ya Kudumu
ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).
Watanzania wapo njia panda, hawajui mchele ni
upi, chuya zipi. Upo ukweli unaosambazwa
lakini uongo umekuwa mwingi sana. Hao walio
njiapanda ndiyo wenye nchi yao. Wao ndiyo
mabosi wa serikali, mahakama na bunge.
Mihimili yote hiyo lazima ifanye kazi kwa
maslahi ya wananchi. Serikali, bunge au
mahakama, inapofanya kazi kinyume na kile
ambacho wananchi wanataka hiyo ni batili. Leo
Watanzania wanataka Ripoti ya Escrow, ndiyo
maslahi yao yalipo.
Wanataka kujua hali halisi ya rasilimali zao, eti
linaibuliwa Zuio la Mahakama, kwamba bunge
lisisome wala kujadili Escrow.
Chombo gani kisichojua wananchi wanataka
nini kwa sasa? Sasa kwa nini kitende kinyume
na maslahi ya Watanzania? Chenyewe kinatoa
huduma zake kwa muongozo na thamani ipi
ikiwa kinapishana na matakwa na wananchi?
Mahakama kazi yake ni kutafsiri sheria,
kuelekeza na kutoa haki. Haiwezi kutafsiri
sheria bila kutungwa na bunge. Yaani wabunge
wanaochaguliwa na wananchi, hutunga sheria
kwa maslahi ya wapigakura. Kwa mantiki hiyo,
mahakama hutafsiri sheria zilizotungwa na
wawakilishi wa wananchi kwa maslahi ya
wananchi.
Mhimili nambari moja, yaani serikali, kazi yake
ni kusimamia na kutekeleza hizo sheria kama
zilivyotungwa na wawakilishi wa wananchi
(bunge), vilevile kama zilivyotafsiriwa na
mahakama. Mpaka hapo utaona kuwa wananchi
ndiyo mabosi wa mihimili yote.
Ufafanuzi huo, utoshe kuonesha kuwa
mahakama kwa kuzingatia kiu ya wananchi,
vilevile kwa kutii matakwa ya wenye nchi, na
kwa kuepusha hali ya hatari ambayo inaweza
kujitokeza pale wananchi watakapopandwa na
hasira kuona dola inakwenda kinyume nao,
mahakama haina budi kujiweka kando na
kuacha bunge litende kazi yake.
Skendo ya Escrow ni nzito; wahuni wavaa suti
wamekwapua zaidi ya shilingi bilioni 300 za
Watanzania. Wamiliki wa hizo fedha wanataka
kusikia wawakilishi wao (wabunge),
wanachukua hatua gani kuwanyoosha hao wezi
na wasaliti wakubwa wa rasilimali zao.
Mahakama ni ya wanasheria. Basi
niwakumbushe msemo wao kwamba “haki siyo
tu itendeke, bali ionekane ikitendeka.” Kwa
kuheshimu huo msemo wao, niwaambie kuwa
wananchi wa Tanzania hawataona haki
inatendeka kama Ripoti ya Escrow haitasomwa
na kujadiliwa bungeni.
JE, MAHAKAMA INATAKA KUVUNJA KATIBA
YA NCHI ?
Hakuna chombo wala mtu yeyote
anayeruhusiwa kuvunja Katiba. Sheria au
uamuzi wowote unaokwenda kinyume na Katiba
ni batili. Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977
ambayo bado ipo hai, Ibara ya 100 katika
vifungu vyake viwili vinavyoelezea Madaraka na
Haki za Bunge, vinazuia mahakama kuingilia
bunge.
Inatamka;
(1) Kutakuwa na uhuru wa mawazo, majadiliano
na utaratibu katika bunge na uhuru huo
hautavunjwa wala kuhojiwa na chombo
chochote katika Jamhuri ya Muungano, au
katika mahakama au mahali pengine nje ya
bunge. (hapa Katiba imeifunga mahakama dhidi
ya uhuru wa bunge)
(2) Bila kuathiri Katiba au masharti ya sheria
nyingine yoyote inayohusika. Mbunge yeyote
hatashtakiwa au kufunguliwa shauri la madai
mahakamani kutokana na jambo lolote
alilolisema au kulifanya ndani ya bunge au
aliloleta bungeni kwa njia ya maombi, muswada,
hoja au vinginevyo.
Vifungu hivyo viwili vipo pia kwenye Sheria
namba 15, ibara ya 14, iliyotungwa mwaka
1984, kuhusu Uhuru wa Majadiliano na Uratibu
wa Shughuli bungeni.
Bunge pia linabebwa na Katiba katika Ibara ya
101, inasema: “Bunge laweza kutunga sheria
kwa ajili ya kuweka masharti ya kuwezesha
mahakama na sheria kuhifadhi na kutilia nguvu
uhuru wa mawazo, majadiliano na utaratibu wa
shughuli katika bunge ambao kwa mujibu wa
Ibara ya 100 umedhaminiwa na katiba.”
Mpaka hapo ni wazi Katiba inaigaragaza
mahakama. Amri ya Zuio la Mahakama (Court
Injunction Order), haina ubavu mbele ya bunge.
Hao majaji ambao wamekaa kikao na
watuhumiwa wa Escrow na kuamua kuwabeba
kwa mtindo wa Amri ya Zuio, wamefeli kikatiba.
Sheria ya Kinga, Madaraka na Haki za Bunge,
kwa ufasaha kabisa, inapigilia msumari kuwa
mahakama haitaingilia bunge. Kwa maana hiyo,
Amri ya Zuio kwa bunge ni kuendelea kushusha
hadhi chombo hicho.
NINI UHURU WA MAHAKAMA? NINI UHURU
WA BUNGE ?
Bunge haliruhusiwi kuingilia uhuru wa
mahakama. Kadhalika mahakama inakatazwa
kuingilia uhuru wa majadiliano na uendeshwaji
wa shughuli ndani ya bunge. Kila mhimili
umekatazwa, sasa nani anastahili nini?
Kwa kifupi ni kwamba bunge halitathubutu
kujadili kesi iliyopo mahakamani, kwa msingi
kwamba shauri lilifunguliwa mahakamani kabla
ya kufika bungeni. Katika mazingira hayo,
ikitokea bunge limejadili kesi hiyo, litakuwa
limeingilia uhuru wa mahakama.
Kama shauri limeanzia bungeni kabla ya kufika
mahakamani, mahakama haitakuwa na budi
kuacha mchakato wa kibunge kuendelea, huku
yenyewe ikijikita kwenye utekelezaji wa kutafsiri
sheria katika kesi husika pasipo kutekwa na
uelekeo au uamuzi wa bunge.
Sakata la Escrow lilianzia bungeni, Kamati ya
PAC ikaandaa hadidu za rejea na kumkabidhi
CAG achunguze. Upande wa pili, Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda naye aliiagiza Takukuru.
Maagizo yote yalitoka katika mfumo wa bunge.
Kwa hiyo, mahakama haina ubavu wa kuzuia
bunge lisiendelee na kazi yake.
Kwa nini bunge na kinga? Tafsiri ni kuwa
wabunge wapo kwa ajili ya wananchi, kwa hiyo
lazima walindwe wanapokuwa wanafanya kazi
yao ya uwakilishi wa wananchi katika kutunga
sheria na kuisimamia serikali.
Mwaka 1883, Bunge la Canada liliambiwa na
kuitikia kwa pamoja kuwa “Kinga za bunge ni
kinga za wananchi na haki za bunge ni haki za
wananchi.” Kwa maana hiyo, mahakama ikizuia
Escrow isijadiliwe bungeni, itakuwa kwa pamoja
imevunja kinga na haki za wananchi.
Mwandishi Erskine May, katika kitabu chake
‘Treaties on the Law, Privileges, Proceedings
and Usage of Parliament’ ameandika: “Haki za
bunge ni haki zote za kipekee za bunge na za
kila mbunge binafsi kwa jumla, ambazo bila
kuwepo kwake, bunge na wabunge hawawezi
kutekeleza majukumu yao ipasavyo.”
Suala la kuwashughulikia wezi wa Escrow ni
moja ya majukumu ya wabunge. Sasa kwa
tafsiri ya Erskine, hapo kinga ya bunge na
wabunge itakuwa wapi ikiwa watakubali zuio la
mahakama kujadili ripoti hiyo. Labda isemwe
leo kuwa bunge halina kinga na Katiba ya nchi
iwe imevunjwa.
SPIKA AKIKUBALI ESCROW ISIJADILIWE
TATIZO NI YEYE
Spika wa Bunge ni mtu mkubwa sana katika
nchi. Ukiondoa Rais na Makamu wa Rais,
Katiba inamtambulisha kama yeye ndiye bosi
namba tatu, halafu wa nne nne ni Jaji Mkuu.
Mama Anne Makinda ni mkuu wa nchi baada ya
Rais na Makamu wa Rais. Katiba inasema
hivyo.
Kwa kutambua nafasi yake kwamba yeye ni
mkubwa kuliko Jaji Mkuu (kikatiba), vilevile
mhimili anaouongoza ni namba mbili baada ya
serikali, mahakama ni wa tatu. Hana sababu
yoyote ya kuburuzwa au kuyumbushwa
ukizingatia anazo kinga zote.
Uamuzi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es
Salaam kusitisha Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kujadili Ripoti ya CAG
kwa hati ya dharura, eti mpaka hoja ya msingi
ipatiwe ufumbuzi ni mtego hatari kwa wananchi
dhidi ya bunge, mahakama na serikali yao.
Kwa nini walalamikaji waende kufungua kesi
baada ya kubaini ‘uharamia’ wao
umegundulika? Walikuwa wapi wakati PAC
inamuagiza CAG kwenda kufanya ukaguzi?
Baada ya kuona upepo wa kaskazi na kusi
umekuwa kimbunga ndiyo wakimbilie
mahakamani?
Hoja yao kwa nini CAG alifanya ukaguzi wakati
mahakama ilishatoa hukumu? Hoja dhaifu sana,
yaani walitegemea fedha zote zaidi ya shilingi
bilioni 300 zibebwe na ukaguzi usifanyike.
Hapohapo ipo hoja kuwa mahakama haijawahi
kutamka popote kuwa IPTL ilishinda kesi.
Spika wa Bunge anaweza kuamua mambo
mawili, ama kukubali kudharauliwa kwa kuwa
mtiifu wa mahakama (kinyume na Katiba ya
nchi) halafu baadaye abebe msalaba wa
dhambi za wezi sambamba na kuonja
machungu ya hasira za wananchi, au asimamie
heshima na thamani yake kwa kuendelea na
Ripoti ya Escrow ili ajiandike historia
iliyotukuka, kasha vizazi vijavyo vimkumbuke.
Kwa kifupi ni kwamba kama Ripoti ya Escrow
haitajadiliwa bungeni, maana yake Makinda
atakuwa hajiamini na haelewi nguvu ya mhimili
anaouongoza. Zaidi ya hapo atakuwa amevunja
Katiba ya Nchi. Upande wa pili, itaonekana kuna
madudu anaficha na zuio la mahakama ni
mbeleko tu.
Majaji watatu waliotoa Amri ya Zuio kwa bunge
leo, wamekiuka Sheria namba 15, Ibara ya 14,
ya mwaka 1984 inayohusu Uhuru wa
Majadiliano na Uratibu wa Shughuli ndani ya
bunge. Wamekosa heshima kwa Sheria ya
Kinga, Madaraka na Haki za Bunge, vilevile
wamevunja Katiba Ibara ya 100.
Makinda pia kwa kukubali kusitisha mjadala wa
Escrow, atakuwa ameshindwa hata kutumia
fursa ambayo amepewa na Katiba katika Ibara
ya 101, kwamba bunge linaweza kutunga sheria
ya kujilinda, kujihifadhi dhidi ya mahakama.
Sheria hiyo inatungwa chini ya dhamana ya
Ibara ya 100.
AMRI YA ZUIO ILIGONGA MWAMBA KWA
DAVIDO;
Oktoba 18, mwaka huu, mwanamuziki kutoka
Nigeria, David Adedeji Adeleke ‘Davido’ alipanda
jukwaani, akatumbuiza na kuondoka kurudi
nchini kwao bila kupata usumbufu wowote.
Davido alipanda jukwaa la Fiesta wakati
kulikuwa na Amri ya Zuio kutoka Mahakama ya
Kisutu, ikiikataza Kampuni ya Prime Time
Promotion kumtumia Davido kwenye shoo ya
Fiesta kutokana na mgogoro wa kimkataba
baina yake na Kampuni ya Times Promotions
and Entertainment, vilevile alinyimwa kibali na
Baraza la Sanaa la Taifa (Basata).
Hata hivyo, Davido alipanda jukwaani na
hakuna uamuzi wowote wa dharura ambao
ulichukuliwa kutoa fundisho kwa wakaidi wa
Amri ya Zuio. Ile adhabu ya kudharau
mahakama (Contempt) haikufanya kitu.
Ni aibu kubwa kwa taifa letu ambalo
linaongozwa na misingi ya sheria na dola. Ni
nchi isiyokuwa na dola peke yake ndiyo
alichokifanya Davido hapa nchini kinaweza
kutokea na kuvumiliwa kana kwamba
hakikutokea kitu. Mahakama haikuona aibu hii!
Kama kwa Davido ilitokea hivyo, nitashangaa
sana kama bunge litanywea na kuamua
kusitisha hoja nzito yenye maslahi mapana kwa
taifa. Bunge linaweza kuendelea na kazi yake.
Halafu wahusika waendelee kutapatapa
mahakamani. Swali; kama kweli ni watu wazuri
na walitenda kilicho halali na haki, wasiwasi wa
kukimbilia mahakamani wa nini wakati Ripoti ya
Escrow haijasomwa?
Jibu ni kwamba wanajua walichokifanya na
wanaelewa kilichomo ndani ya Ripoti ya Escrow
na wanatambua nini ambacho kinaenda
kusomwa na Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe,
kwa maana hiyo ni waelewa wa kile
kinachokaribia kuwapata. Ripoti isomwe, hata
wakizuia itavuja na wananchi watachukua
uamuzi. Tuache kulinda ufisadi kwa amani yetu
na maendeleo ya uchumi wetu.
Mungu ibariki Tanzania.
Mungu waongoze wabunge wetu kusimama
kidete Ripoti ya Escrow isomwe.
Credit:Jf

LIKE page yetu MJUMBE BLOG facebook au Tutembelee Mtandaoni Kwa Kuandika MJUMBE BLOG kisha ingia hapo Upate picha,matangazo,Taarifa Mpya,Habari muhimu kila mara.



©Mjumbe Blog Volunteers

About Author

Advertisement

Post a Comment

 
Top