Kitaifa
Waziri wa JK yamkuta
Posted Alhamisi,Januari8 2015 saa 9:36 AM
Kwa ufupi
Walipoulizwa sababu ya kumzomea mbunge huyo, baadhi
wa wananchi walisema hawana imani naye wakidai alichakachua matokeo ya
mwaka 2010.
Dar es Salaam. Wakati utata
ukizidi kujitokeza katika uapishaji wa viongozi wa Serikali za Mitaa
Mkoa wa Dar es Salaam kutokana na waliodaiwa kushinda kuwekwa kando na
kuapishwa walioshindwa, Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk Makongoro
Mahanga jana alikumbana na zomeazomea hadi kulazimika kuondoka kwenye
Ofisi za Manispaa ya Ilala, Arnatouglou ambako shughuli hiyo ilikuwa
ikifanyika.
Dk Mahanga ambaye pia ni Mbunge wa Segerea (CCM),
alizomewa akitakiwa kuondoka katika eneo hilo, akidaiwa kwamba
angebadilisha matokeo na kuwapa ushindi wagombea wa chama chake.
Eneo hilo lilijaa wafuasi wa Chadema, CUF na CCM
huku kila kundi likiwa limesindikiza wenyeviti wake kuapishwa katika
shughuli ambayo ilifanyika kwa awamu tatu kwa kila jimbo; Segerea, Ilala
na Ukonga kupewa saa mbili.
Waziri Mahanga aliwasili wakati wa zamu ya Segerea
saa saba mchana, ndipo kundi la mashabiki wa upinzani lilipoanza
kumzomea na kuimba nyimbo za kumkashifu na kutaka atoke katika ukumbi
ulioandaliwa kwa ajili ya kuwaapisha wenyeviti.
“Escrow... escrow... ondoka, hatukutaki. Hapa
hakieleweki mpaka uondoke, hatutaki uchakachuaji wako...” zilisikika
sauti za watu mbalimbali huku zikiimba nyimbo mbalimbali kumfukuza
mbunge huyo ukumbini.
Baada ya dakika takriban 25 za kelele hizo, waziri
huyo alinyanyuka na kuondoka huku wananchi hao wakimsindikiza kwa
nyimbo hizohizo na polisi wakifanya kazi yao ya kuhakikisha hadhuriki.
Wakati akiondoka, Dk Mahanga alikisogelea kikundi
kimoja kilichokuwa kinahoji alichokuwa amefuata wakati shughuli ya
uapishaji wenyeviti haimhusu na kujibu: “Wenyeviti wangu 59 wa Jimbo la
Segerea wanaapishwa leo. Kwa nini nisihudhurie? Kelele hizi zinaonyesha
jinsi gani ninavyotikisa jiji la Dar es Salaam.”
Baadaye akionekana mwenye kujiamini, mbunge huyo
alikatisha katikati ya kundi la mashabiki waliokuwa wakimzomea na
kuingia katika gari lake na kuondoka.
Kelele ziliendelea hadi gari la kiongozi huyo lilipotoweka kabisa katika viwanja hivyo.
Walipoulizwa sababu ya kumzomea mbunge huyo,
baadhi wa wananchi walisema hawana imani naye wakidai alichakachua
matokeo ya mwaka 2010.
Mmoja wa wananchi hao, Mohamed Said alisema
alipofika katika ofisi za halmashauri, dhana iliyomjia kichwani ni
uchakachuaji. Aliongeza kuwa kuwapo kwa Dk Mahanga kungesababisha vurugu
kubwa bila sababu.
“Mbona katika maeneo mengine wanakoapishwa wenyeviti wabunge wao hawajaenda, yeye amefuata nini?” alihoji.
MWANANCHI
MWANANCHI
Post a Comment