Nianze na kisa hiki cha ndege aina ya kong’ota ambaye sifa yake kuu ni kuwa na mdomo wenye ncha kali unaomuwezesha kuchimba na kuutoboa mti wowote ule anaotaka afanye makazi au shughuli yake yoyote ile.
Sifa hiyo ilimtamanisha sana ndege mwingine aitwaye mbayuwayu aliyeamua siku moja kumuuliza mwenzake imekuwaje akawa na sifa hizo nzuri.
Mbayuwayu akamuomba kong’ota amsaidie kuwa na mdomo mrefu, mgumu utakaomuwezesha kutoboa miti. Akakubali kumsaidia mwenzake akaliweka jiwe chini ya ardhi huku akielekeza kinachotakiwa kufanywa. Akamueleza mbayuwayu aruke juu sana na arudi ardhini kwa kasi na kulidonoa jiwe kwa mdomo kwa nguvu na akifanya hivyo mdomo wake utakuwa mgumu hivyo utaweza kutoboa miti.
Kwa kuwa mbayuwayu alidhamiria kupata mdomo mgumu alifanya hivyo, lakini alipokuwa akilikaribia jiwe lile wazo lilikamjia kichwani mwake kuwa ‘akili za kuambiwa changanya na zako’.
Kama angefuata maelekezo ya kong’ota angekufa. Ndege huyo aliamua kuchanganya akili za kuambiwa na zake kisha akafanya uamuzi wenye masilahi kwake na kwa jamii inayomzunguka.
Kutokana na kuibuka kwa watu hawa wanaoutaka urais. Sasa Watanzania wanatakiwa kuiga ya Mbayuwayu, yaani kuchanganya akili zao na zile za kuambiwa zinazotoka vinywani mwa hao ‘wanaolilia kwenda Ikulu’. Siyo siri tena. Kila anayejisikia hivi sasa anatangaza nia yake ya kuutaka urais mwaka 2015.
Uamuzi wa watu hawa wanaoutaka urais umeibua mijadala kila kona na kusababisha wasomi, viongozi wa dini na wananchi wa kawaida nao kuingia katika mkumbo wa kueleza juu ya sifa za kiongozi na nani anayestahili.
Baadhi wanaamini kuwa uongozi ni karama au kipaji anachozaliwa nacho mtu, wengine wanaamini mtu anaweza kufundishwa kuwa kiongozi. Kwa upande mwingine wapo wanaoamini kwamba mtu akiwa na sifa za kuzaliwa na akapewa mafunzo ya uongozi, huyo ndiye kiongozi anayefaa.
Hata hivyo, wote hawa hukubaliana na jambo moja kwamba siyo kila mtu hata aliyekuwa na sifa anaweza kuwa kiongozi.
Kwangu kiongozi ni mtu mwenye uzalendo, msomi wa uhakika na siyo bora msomi, mwelewa wa mambo, mchapakazi, mwenye maono na awe mfano bora kwa anaowaongoza na asiyetanguliza masilahi yake binafsi.
Kwa bahati mbaya Taifa letu limejaliwa kuwa na watu wa aina hii wengi, lakini wengi wao hawapo katika tasnia ya siasa, hawaipendi na hawataki hata kuisikia na kama wapo basi hawautaki urais hata kidogo, achilia mbali uongozi wa kawaida.
Dunia imewahi kuwapata watu wa aina hii na mfano mzuri ni aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini, Nelson Mandela ambaye licha ya kufungwa miaka 27 hakukata tamaa ya kuikomboa nchi yake.
MWANANCHI LEO
Post a Comment