OFISA WA IKULU AHOJIWA KUHUSU SAKATA LA RUGEMALILA...
Mnikulu Shaban Gurumo amekiri mbele ya Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma, kwamba alipokea Sh milioni 80.8 kutoka kwa James Rugemalira na kuzitumia kwa matumizi yake binafsi, ingawa amekanusha kuomba fedha hizo.
Gurumo alitoa utetezi huo Dar es Salaam jana mbele ya baraza baada ya kusomewa mashitaka ya kutumia cheo chake cha uongozi wa umma vibaya na kujipatia fedha hizo, jambo ambalo ni kinyume na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Alikiri kumfahamu Rugemalira, akisema ni rafiki yake kwa zaidi ya miaka 10. Alisema daktari wake, Fred Limbanga ndiye aliyemtambulisha kwa Rugemalira.
“Kama Mnikulu sijawahi kupokea fedha za kiuchumi kwa Rugemalira wala kuwa na mahusiano naye ya kiuchumi, naitambua akaunti ya Mkombozi kuwa ni ya kwangu na niliifungua baada ya James kunishauri,” alisema Gurumo.
Alisema awali hakufahamu nani aliyemwekea kiasi hicho cha fedha kwenye akaunti hadi hapo baadaye alipotambua kuwa ni Rugemalira. Alidai hadi sasa hajafahamu sababu za kupewa kiasi hicho cha fedha na wala hakuhangaika kumuuliza Rugemalira.
Pia, alisisitiza kuwa pamoja na kutofahamu fedha hizo alipewa za matumizi gani, ana uhakika si zawadi kama inavyodaiwa.
“Ila nahisi baada ya kuitwa na Kamati ya Uchunguzi ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kujibu tuhuma zinazonikabili, huenda Rugemalira alinitumia fedha hizo baada ya kusikia kuwa nina mgonjwa anayeumwa saratani ya mfuko wa uzazi,” alisema.
Alisisitiza kuwa hajawahi kuzungumza wala kuomba fedha si kwa barua, simu wala kwa mazungumzo ya ana kwa ana na Rugemalira, ila amekuwa akizitumia kwa shughuli zake binafsi kwa kuwa alizikuta kwenye akaunti yake. “Sijawahi kuomba fedha yoyote kwa Rugemalira wala VIP,” alisema.
Alisema pia hata katika tamko la mali na madeni, aliloliwasilisha Desemba 29, mwaka jana kwa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, akiwa kama kiongozi wa umma, aliziorodhesha fedha hizo kuwa ni mali yake iliyopo katika akaunti yake ya Benki ya Mkombozi alizopewa na Rugemalira.
Alikiri kuwa alikuwa na matatizo ya kuwa na mgonjwa huyo, aliyempeleka India kwa matibabu na hadi sasa ameshatumia dola za Marekani 40,000 ambayo ni sawa na Sh milioni 73.2, hivyo hakuwa na shida yoyote ya fedha. “Mimi nina fedha zaidi ya hizo za Rugemalira ndio maana sikuomba.”
“Nakiri kupokea fedha hizo Sh milioni 80.8, lakini nilishangaa kwa mara ya kwanza niliposikia kwenye redio iliyokuwa ikirusha hewani kipindi cha Bunge, mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu alikuwa akisisitiza nilipewa Sh milioni 800 na kampuni ya VIP Engineering and Marketing Limited, jambo ambalo si la kweli,” alisema.
Aliomba baraza hilo kuwachukulia hatua na kuwachunguza wale wote waliodanganya, wakiwemo wabunge na vyombo vya habari pamoja na mitando ya kijamii, kuhusu kiasi cha fedha alizopatiwa na Rugemalira ili ifahamike kama wamefanya makusudi, wametumika au la.
Awali, akimsomea mashitaka mbele ya baraza hilo, Mwanasheria wa Sekteratieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Hassan Mayunga alidai mlalamikiwa akiwa kiongozi wa umma, aliomba na kupokea Sh milioni 80.8 kutoka kwa kampuni ya VIP kinyume cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Aidha alidai mlalamikiwa huyo, alipokea kiasi hicho cha fedha kinyume cha sheria hiyo, inayokataza kiongozi wa umma kuomba na kupokea fedha kwa maslahi yake binafsi.
Alidai Februari 5, mwaka jana alipokea Sh milioni 80.8 kutoka kwa VIP kupitia akaunti yake namba 00110102645401 iliyopo katika Benki ya Mkombozi tawi la St Joseph jijini Dar es Salaam.
Shahidi upande wa Sekretarieti hiyo, ambaye ni Ofisa Uchunguzi, Bazilio Mwanakatwe, alidai kupitia kamati ya uchunguzi iliyoundwa na sekretarieti hiyo, walibaini Gurumo alikiuka maadili ya viongozi wa umma, kutokana na kupokea kiasi hicho kikubwa cha fedha bila kukitamka kwa viongozi wake ili kipangiwe matumizi.
“Sheria inatamka wazi kuwa kiongozi wa umma haruhusiwi kuomba au kupokea zawadi kubwa kwa maslahi yake isipokuwa zawadi ndogo isiyozidi Sh 50,000 na endapo itazidi atatakiwa kutamka zawadi hiyo na kukabidhi kwa Ofisa Masuhuli wake ili waweze kuipangia namna ya kuitumia zawadi hiyo,” alisema.
Alidai kamati hiyo ilibaini pia uwepo wa mgongano wa malsahi ambapo Gurumo ambaye ni Mnikulu wa Ofisi ya Rais, kwa nafasi aliyonayo anafahamu siri nyingi na kupata fursa nyingi hivyo kitendo cha kupokea fedha kutoka kwa mwekezaji mkubwa ni kujiingiza katika mgongano wa maslahi.
Kwa upande wake, Mwanasheria wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Getrude Cyriacus, alidai Gurumo, baada ya kuingiziwa fedha hizo, hadi sasa ameshatoa na kutumia zaidi ya Sh milioni 77.
Hoja za kila upande kuhusu shauri hilo, zimepangwa kuwasilishwa tena mbele ya baraza hilo, Machi 13, mwaka huu.
Wakati ofisa huyo wa Ikulu akiwa miongoni mwa viongozi wa umma watano waliokwishafikishwa mbele ya baraza kwa madai ya kukiuka maadili, leo Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), Philip Saliboko, pia anapandishwa kizimbani kujibu mashitaka akidaiwa kupatiwa Sh milioni 40.4 kutoka Kampuni ya VIP.
Wakati huo huo, leo baraza hilo linatarajiwa kutoa uamuzi kuhusu pingamizi lililowasilishwa juzi na aliyekuwa Mkurugenzi wa Ushauri wa Kisheria wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Rugonzibwa Mujunangoma aliyetaka shauri linalomkabili la kupokea Sh milioni 423, liahirishwe kusikilizwa kutokana na kesi ya msingi iliyopo Mahakama Kuu.
Post a Comment