![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEjFiFSbKW5PqcGJ2VbnMkzlB9kamPMWp8o8YKVgSv5dhXKIaZw1NjVBdYF3sELlIuM9dL41kKHCVvsCLHWhl3Zq1gshNDjjAbQ7OjVYjawaWRr_b1KssAFxQPXKFCuYjou7iV9DoC3hncYS/s640/1430595418762.jpeg)
RAIS Jakaya Kikwete ameahidi kuongeza mishahara ya wafanyakazi kuanzia Julai mwaka huu, ili walau kima cha chini kikaribie Sh 315,000 ambazo Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta) limekuwa likiipigia kelele kwa muda mrefu.
Kikwete alisema hayo alipokuwa akihutubia wananchi waliohudhuria sherehe za Siku ya Wafanyakazi Duniani, zilizofanyika kitaifa kwenye viwanja vya CCM Kirumba jijini Mwanza jana.
Rais Kikwete alisema, “Ongezeko lililoko ni dogo sana lakini si haba. Na mwaka huu tutaongeza mshahara kufikia Sh 315,000 kima cha chini na kama hakitafikia, tutaangalia mahesabu yetu kwa nini, angalau ikaribie hiyo”.
Rais Kikwete alisema serikali imechukua hatua za makusudi za kuongeza mshahara kila mwaka tangu alipoingia madarakani mwaka 2005 ambapo kima cha chini alikuta Sh 65,000 na amekipandisha na sasa kimefika Sh 265,000 ambayo ni zaidi ya mara nne.
Kuhusu kauli iliyotolewa na vyama vya upinzani vinavyounda Ukawa kuwa serikali imepanga kusogeza uchaguzi mkuu usifanyike Oktoba mwaka huu ili kumuongezea muda Rais Kikwete aendelee kutawala, amejibu na kusema hana mpango huo.
“Nimesikia wazee (viongozi wa Ukawa) wanasema serikali haina mpango wa kufanya uchaguzi. Urais wangu hauna mpango wa kufanya hivyo. Aibu! Sijui maneno haya wameyatoa wapi...” alisema.
Kwa upande mwingine alisema serikali imeendelea kupunguza kiwango cha kodi wanayotozwa wafanyakazi (PAYE) mwaka hadi mwaka. Alikuta asilimia 18.5 na kimeshuka katika utawala wake na kufikia asilimia 12.
“Na mwaka huu tutapunguza sijui tutafikia asilimia 9 kama mnavyotaka ila tutakapofikia si pabaya,” alisema Kikwete bila kutaja kiwango cha asilimia kitakachopunguzwa.
Akizungumzia mshahara katika sekta binafsi, alisema kima cha chini hupangwa na bodi za mishahara za kisekta na kwamba majadiliano yalikuwepo ambayo yalipandishwa kutoka Sh 48,000 hadi Sh 700,000 kulingana na sekta.
Aidha alikitaka Chama cha Waajiri (ATE) kuliweka kwenye ajenda suala la waajiri wanaolipa chini ya kiwango watakapokwenda kukutana naye.
Alisema katika kipindi cha uongozi wake aliahidi ajira milioni moja lakini hadi anaondoka madarakani zaidi ya ajira milioni 2.6 zinapatikana kutoka serikalini pamoja na sekta binafsi.
Kikwete alionya baadhi ya waajiri ambao hawalipi viwango vilivyokubaliwa vya mishahara, kwa kusema hilo sio jambo la kiungwana na linahuzunisha. “Waajiri hufikia makubaliano ya bodi za kisekta katika ulipaji wa mshahara.
Tusikubali watu hawa waendelee kuhujumu haki za wafanyakazi. “Naomba mamlaka husika tusikubali watu hawa wakaendelea kudhulumu haki za wafanyakazi,” alisema Rais Kikwete.
Pia alisema wanajishughulisha kwa kadiri ya uwezo wao kutafuta matatizo yanayowakabili wafanyakazi, yale ambayo hayakupatiwa ufumbuzi si kwa sababu ya udogo wa dhamira bali ugumu wa tatizo lenyewe.
“Ambayo sijasema leo naendelea na nitaendelea kuyashughulikia mpaka nitakapokabidhi kwa huyo atakayekuja. Tutaendelea na Wizara ya Kazi na Ajira na ofisi ya takwimu kukuza ajira Tanzania,” alisema.
Alisisitiza kuwa rais ajaye atamkabidhi orodha ya yale mambo ambayo ni kiporo na anayojua mwenyewe na atatoa ushirikiano kwa rais ajaye.
Katika sherehe hizo Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta), Nicholus Mgaya alitaja madai waliyoyatoa kwa rais, kuwa makato ya kodi ni makubwa.
Mgaya alisema mwaka jana PAYE ilipungua hadi kufikia asilimia 12, lakini mategemeo yao ifikie asilimia 9 mwaka huu. Mgaya aliwataka wafanyakazi kutumia kura yao ipasavyo katika uchaguzi mkuu kwa kuchagua viongozi wanaojali tabaka la wafanyakazi.
Na jijini Dar es Salaam,
Wafanyakazi wamelitaka Bunge kutopokea na kujadili bajeti za taasisi za umma, ikiwemo wizara mbalimbali zilizopelekwa bungeni bila kuzingatia sheria inayotaka kuwashirikisha wafanyakazi kupitisha bajeti za taasisi zao.
Sheria hiyo ya ajira na uhusiano kazini namba sita ya mwaka 2004 inataka kuwashirikisha wafanyakazi kupitisha bajeti zao kwa kutumia mabaraza ya wafanyakazi.
Wafanyakazi hao walisema hayo pamoja na kudai kima cha chini cha mshahara kuwa Sh 720,000 badala ya Sh 100,000 au 250,000 kilichopo sasa katika hotuba yao iliyosomwa na Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Migodi, Nishati, Ujenzi na Kazi Nyingine (Tamico) kanda ya Dar es Salaam na Pwani, Charles Mgashi.
Hotuba hiyo ilitolewa katika maadhimisho ya siku ya wafanyakazi iliyoadhimishwa kimkoa katika Uwanja wa Uhuru, huku mgeni rasmi akiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki.
Akizungumza katika hafla hiyo na kujibu baadhi ya maombi hayo, Sadiki alikiri kuwa ni ukweli usiopingika mshahara hautoshi na sehemu nyingine za kazi mazingira ni magumu lakini pamoja na changamoto, wafanyakazi wamekuwa wakifanya kazi kwa tija na ubunifu.
Na huko Zanzibar,
Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi (SMZ), Dk Ali Mohamed Shein amewataka wanasiasa kuacha kuwadanganya vijana kwamba wana uwezo wa kuwapatia ajira na kusisitiza dunia yote sasa inakabiliwa na tatizo hilo ambalo linatokana na kuyumba kwa uchumi.
Akizungumza katika kilele cha sherehe za siku ya wafanyakazi duniani zilizofanyika kisiwani Pemba katika uwanja wa Makonyo, alisema nchi maarufu zenye uchumi mkubwa duniani zimeyumba na kukabiliwa na tatizo la ajira ikiwemo za Ulaya na kutolea mfano Denmark.
“Nawaomba wanasiasa muache tabia ya kuwadanganya vijana kwamba mna uwezo mkubwa wa kuwapatia ajira vijana si kweli...si Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wala Serikali ya Muungano ajira ni tatizo kubwa,” alisema.
Alisema Serikali ya Mapinduzi ya awamu ya saba tangu ilipoingia madarakani imefanya kazi kubwa ya kuzalisha ajira kupitia taasisi zake pamoja na sekta binafsi ambazo zimepewa nafasi kubwa ya kufanya kazi nchini.
Kwa mfano alisema katika mwaka 2010 jumla ya ajira za vijana 25,019 zimepatikana katika taasisi mbalimbali Unguja na Pemba, huku katika sekta binafsi ajira zilizopatikana ni 4,850.
Aidha alisema kima cha chini cha mshahara kiliongezeka kutoka Sh 100,000 katika mwaka 2011 na kufikia Sh 125,000 pamoja na posho kwa wafanyakazi wake huku kiwango hicho kikipanda na kufikia Sh 150,000 sawa na asilimia 20.
Aidha katika hotuba yake alisema Serikali haitovumilia kikundi cha wanasiasa kuanzisha vurugu kwa kisingizio cha kutekeleza demokrasia na kuongeza kwamba uchaguzi unasimamiwa na taasisi zilizopewa jukumu hilo kwa mujibu wa katiba na sheria.
“Nataka niwahakikishie wafanyakazi na wananchi kwa ujumla kwamba Serikali zote mbili, mimi na Rais Jakaya Kikwete tutasimamia amani na utulivu kuelekea uchaguzi mkuu kwa lengo la kuona wananchi wanaishi katika mazingira ya utulivu,” alisema.
Imeandikwa na Grace Chilongola, Mwanza, Khatib Suleiman, Zanzibar na Theopista Nsanzugwanko
MJUMBE BLOG
Ni Ukurasa wa Habari,Picha,Matukio,Matangazo.
#KUJERUHI hisia za watu/mtu si Kusudi letu.
MAONI PIGA:0752025002
Post a Comment