KAMANDA WA POLISI MKOA WA TEMEKE ANDREW SATTA.
MKUU wa Kitengo cha Kuzuia na Kupambana na Ujambazi Mkoa wa Morogoro, Elibariki Pallangyo (53), amepigwa risasi na kufa papo hapo nyumbani kwake eneo la Yombo jiji Dar es Salaam.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Andrew Satta alisema kuwa usiku wa kuamkia jana majira ya saa tisa usiku, kundi la watu zaidi ya kumi lilivamia nyumbani kwa Pallagyo eneo la Yombo kwa kuruka ukuta, kisha kuvunja mlango na kuingia ndani walikopora fedha na simu za mabinti wanne waliokuwa ndani kabla ya kufanya mauaji.
“Hili tukio ni la kusikitisha kwani watu hawa wanaonesha walikuwa na lengo la kumuua tu na si kupora mali, kwani wamechukua fedha Sh 130,000 pamoja na simu za mkononi 4 ambazo walikuwa nazo hawa wasichana waliowakuta sebuleni,” alisema Satta.
Alisema baada ya watu hao kupora simu na fedha kutoka kwa mabinti, waliekea kwenye chumba cha Pallangyo, wakampiga risasi moja kifuani na kumuua.
Wauaji hao walitokomea kusikojulikana huku wakisahau kifaa kinachotumika katika milipuko. Mwili wa marehemu umehifadhiwa Hospitali ya Temeke na utapelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kwa uchunguzi kabla ya maziko
Post a Comment