Unknown Unknown Author
Title: LOWASSA AWATAKA WANANCHI WA KYELA WASIMPE KURA DK MWAKYEMBE...
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
MGOMBEA Urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, amepata mapokezi makubwa jimboni kwa hasimu wake kisiasa, Dk...






MGOMBEA Urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, amepata mapokezi makubwa jimboni kwa hasimu wake kisiasa, Dk. Harrison Mwakyembe.

Wakati akihutuhubia mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Takoshiri jimboni humo jana, Lowassa aliwataka wananchi wa jimboni hilo wamwadhibu Dk. Mwakyembe kwa kumchagua mgombea ubunge wa Chadema anayewakilisha Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Abraham Mwanyamaki.

“Nawashukuru sana kwa mapenzi yenu, naomba mapenzi yenu haya yaonekane katika sanduku la kura kwa huyu mbunge mzuri (Mwanyamaki).

“Nyie mna bahati mbaya ya kuchagua wabunge wa ajabu ajabu, nawaambieni wana Kyela huyu ni mbunge mzuri, mna bahati mbaya ya kuchagua wabunge wenye matatizo. Nawaomba mumpe adhabu tarehe 25, adhabu yake msimpe kura ila mchagueni huyu bwana, (Mwanyamaki),” alisema Lowassa na kushangiliwa.

Dk. Mwakyembe ndiye aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati Teule ya Bunge la tisa lililounda kamati hiyo kuchunguza sakata la Kampuni ya Kufua Umeme ya Richmond iliyosababisha Lowassa kujiuzulu uwaziri mkuu, miaka minane iliyopita.

Awali, kabla Lowassa hajawasili kwenye viwanja hivyo saa 9:50 alasiri, alifanya mikutano ya kampeni katika maeneo ya Tunduma, Ileje, Makete, Tukuyu na Busekero.

Katika mikutano hiyo, mamia ya wapenzi wa Ukawa, walijitokeza kwa wingi kuonyesha ni kwa jinsi gani wanavyomuunga mkono mgombea huyo wa urais.

Katika Jimbo la Kyela, maelfu ya wananchi walikuwa wakizunguka katika viunga vya mji huo wakiimba nyimbo mbalimbali zikiwamo zilizoonyesha kumlaumu Dk. Mwakyembe kutokana na redio yao ya kijamii kufungwa.

Kingunge

Kwa upande wake, mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale Mwiru, alisema ili mtu aweze kushinda urais, lazima abebwe na watu.

“Kwenda Ikulu lazima ubebwe na watu, usipokuwa na watu huwezi kwenda Ikulu kihalali.

“Hata Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema ukikosa haki ndani ya CCM, utaipata nje ya CCM, ndiyo maana Lowassa aliamua kuitafuta haki nje ya CCM.

“Mimi babu yenu wosia wangu ni kwamba, tarehe 25 mkienda kwenye kituo cha kupiga kura, unachukua, unaweka, Lowassa,” alisema Kingunge.

FREEMAN MBOWE

Naye Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alisema uchaguzi wa mwaka huu utahitimisha safari ya kudai haki na kuleta siasa za vyama vingi za ukweli.

“Tunakwenda kupigania utawala mpya na kumrudisha Mungu katika utawala wa nchi yetu.

“Tunajua CCM wanaandaa mbinu mbalimbali za kuiba kura, ndiyo maana wanasema tukapige kura tukalale, CCM wametengeneza kura za bandia na wanatarajia kuziingiza vituoni kwa kutumia waangalizi feki wa kimataifa watakaowapa vitambulisho.

“Pamoja na mbinu hizo, mawakala wetu lazima wawe makini, hawa waangalizi wa kimataifa wanaotarajia kufanya uharamu na kupewa vitambulisho bandia, wasijaribu kubeba kura bandia, zitawatokea puani,” alisema Mbowe.

Asimikwa

Kabla ya Lowassa kuanza kuhutubia, wazee waliotangazwa kuwa ni wawakilishi wa wazee wa Wilaya ya Kyela, walimvika mgolole wa kinyakyusa na kumkabidhi mkuki waliosema unaitwa mbogolo.

Walisema vitu hivyo ni kama ishara ya ushujaa na pia walimpa kitu mfano wa funguo waliosema ni wa kufungulia Ikulu.

About Author

Advertisement

Post a Comment

 
Top