Kamanda wa mkoa wa kipolisi wa Tarime na Rorya, Lazaro Mambosasa
Tarime. Mfuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kadogo John Msabi, mkazi wa kijiji cha Remage, kata ya Nyagicheri, wilayani Tarime mkoani Mara ameuawa kwa kuchomwa kisu tumboni na mtu anayedaiwa kuwa ni ndugu yake wa damu baada ya kutofautiana kisiasa.
Taarifa kutoka kijijini hapo ambazo zimethibitishwa na Kamanda wa mkoa wa kipolisi wa Tarime na Rorya, Lazaro Mambosasa zinaeleza kuwa ndugu huyo ambaye ni mfuasi wa Chama cha Mapinduzi alichukua uamuzi wa kumuua Msabi (35) usiku wa kuamkia leo baada kutofautiana katika masuala ya kisiasa waliyokuwa wakibishania.
Taarifa za kipolisi mkoani humo zinazema, baba wa ndugu hao amesema hajui aliyehusika na mauaji hayo, hatua inayochukuliwa kuwa anajaribu kumlinda mwanaye anayetuhumiwa kwa mauaji hayo asichukuliwe hatua za kisheria.
Kwa mujibu wa Kamanda Mambosasa, polisi wameanza uchunguzi wa tukio hilo na kwamba taarifa zaidi zitatolewa baadaye leo.
Uchaguzi wa rais, wabunge na madiwani umefanyika jana nchini kote ambapo hali ya amani na utulivu imeripotiwa kutawala, isipokuwa dosari chache zilizojitokeza katika baadhi ya maeneo.
CHANZO:MWANANCHI
Post a Comment