Siku moja baada ya kufuta sherehe za Uhuru, zinazoadhimishwa Desemba 9 ya kila mwaka, jana Rais John Magufuli amefuta maadhimisho ya Siku ya Ukimwi na kuagiza badala yake, fedha ambazo zingetumika zinunulie dawa za kufubaza makali ya Ukimwi (ARV).
Jana, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alisema: “Rais ameagiza hivyo leo na taarifa imeshasambazwa kwa wahusika, natumaini wameanza kulifanyia kazi agizo hilo,” alisema.
Kaimu Mkurugenzi wa Mwitikio wa Taifa wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids), Dk Morris Lekule alisema wamepokea agizo hilo na kwamba kilichofutwa ni sherehe zinazojumuisha kuwaalika viongozi wa kitaifa, vikundi vya ngoma, kusoma hotuba au risala na maadhimisho hayo kufanyika kila mkoa.
Dk Lekule alisema badala yake, kitakachofanyika siku hiyo ni elimu ya kawaida kuhusu Ukimwi, takwimu na hali halisi ya kitaifa ya ugonjwa huo.
“Elimu hiyo ni sehemu ya kazi, kwa hiyo tutaendelea na elimu ya kawaida kwa wananchi kuhusu ukubwa wa tatizo na namna ya kuendelea na vita hiyo,” alisema.
Alisema tayari Tacaids imeshatoa taarifa ya kusitisha shughuli zote za maadhimisho hayo mikoani ikiwamo maandamano, maonyesho na shughuli nyingine zinazohusiana na sherehe hizo.
Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi duniani yalianza kufanyika Desemba Mosi, 1981 baada ya virusi vya Ukimwi kutambuliwa rasmi na wanasayansi.
Chanzo:Mwananchi
Post a Comment