
SHERIA YA ‘MAKOSA YA MTANDAO’
CYBER LAW
1. Kifungu 7 (2b): Mpokeaji wa ujumbe (receiver) anaweza kushtakiwa kwa kosa la kupokea ujumbe ambao sheria imeufanya kuwa wa jinai. (Mfano: Mtu akikuforwadia ujumbe, ukiupokea na wewe umefanya kosa la jinai).
2. Kifungu 21(1): Mtumia mtandao wa Intaneti yeyote hayuko salama kwani mtoa huduma wake analazimika kutoa habari zake kwa serikali pale zitakapohitajika (kwa lazima).
3. Kifungu 8: Itakuwa ni kosa la jinai kama mtu ataweka wazi nyaraka za siri za serikali hata kama ni nyaraka ya kusaidia nchi kwa ujumla (Mfano: Matumizi mabaya ya mali ya umma)
4. Kifungu 14: Picha yoyote yenye mwelekeo unaoweza kuonekana kama ‘mchafu kingono’ inaweza kupelekea mtu kufungwa hadi miaka 10 au kulipa milioni 30; Sasa kama mtu kaweka picha yake Instagram ambayo sio ya ponografia lakini ‘ikatafsiriwa’ hivyo. Sheria haijatafsiri ponografia!
5. Kifungu 23: Je, ulijua kuwa ‘kusababisha maudhi ya hisia’ kwa mtu mwingine ni unyanyasaji na unaweza kufungwa kifungo kisichopungua mwaka mmoja?
6. Rejea adhabu ya ibara mbalimbali: Sheria hii kila kosa linaweza fanya mtu afungwe kifungo hadi cha maisha na kulipa pesa hadi zisizohesabika kwani hakijawekwa kikomo cha juu cha adhabu bali kikomo cha chini tu kwa kiingereza “not less than”
7. Sheria haijaeleza vizuri suala la kutumia jina lisilo lako kwenye mtandao na hivyo mtu anaweza kushitakiwa kama kuna mtu mwingine mwenye jina kama hilo katika maisha halisi.
8. Serikali kupitia waziri husika ndio ina mamlaka ya kusema jambo lililowekwa kwenye mtandao ni la kweli, uongo au la kupotosha. Kumbuka hata ESCROW, EPA walisema ni uwongo; ni wangapi katika mtandao wangeshtakiwa kiuonevu kwa hili?
9. Kifungu 22: Ukiweka ujumbe katika mtandao na ukaufuta au kuuboresha, kama ukishtakiwa kwa kuweka ujumbe huo unaweza kuhukumiwa pia kwa adhabu ya kuuboresha au kuufuta. Ni mara ngapi unafuta status zako za WhatsApp? Unaweza shtakiwa kwa kuchelewesha ushahidi kisa tu ulifuta na hamna mtu anayeweza kujua ulifuta kwa kusudi au la.
10. Mkuu wa kituo cha Polisi chochote kile nchini anaweza kuagiza wewe umpatie simu/laptop yako au taarifa zako zote (kwenye email, chats n.k) au hata vifaa vyako au ofisi yako kwa ajili ya upelelezi bila oda ya Mahakama.
11. Kifungu 31 (3a): “As soon as practicable” the law states.
Askari Polisi wakichukua vitu vyako wanaweza kukupatia listi ya vitu walivyovipokea muda watakaoona kwao inawezekana kufanya hivyo. Jiulize, inaweza chukua muda gani?
12. Kifungu 31-35 & 39-45: Kama wewe ni Blogger au Mtoa Huduma ya mtandao, pale unapobaini kosa ukalitoa na uko katika mikakati ya kuitaarifu mamlaka husika (Kama sheria inavyosema) askari naye anaweza kwa wakati huohuo akaja kukagua na kuchukua vitu vya kazi zako (kama sheria inavyosema), hivyo sheria inakinzana yenyewe kwa yenyewe. Blogger yuko sawa kisheria na askari yuko sawa kisheria.
WAPE TAHADHARI WATUMIAJI WA MTANDAO WENGINE PIA.
MAONI BINAFSI YA MWANAHABARI NA MTUMIAJI WA MITANDAO:
#Mimi Mwanakijiji
Hatutaitii Sheria Yao ya Mitandao Jinsi Ilivyo Sasa
Na. M. M. Mwanakijiji
Kwa mara nyingine tena watawala wetu walioshindwa wamekuja na ubunifu wao wa hali ya juu wa kuwalazimisha Watanzania waseme ukweli wakati wote. Baadhi ya watu - na wanasiasa na vyombo vya habari - wameonekana kushtushwa sana na ujio wa ile inayoitwa 'Sheria ya Usalama kwenye Mitandao" au jina jingine tamutamu. Watu wameshtushwa kwa sababu wanaona kama inawalenga wao na kutishia watu kupeana habari. Wameshtushwa kwa sababu kwa muda mrefu walikuwa wanaamini - sijui kwanini - kuwa utawala huu unajali saaaana (kwa sauti ya Baba Mshami kwa wanaomkumbuka) uhuru wa maoni na habari.
Kwa baadhi yetu hakuna lolote lililoko kwenye Sheria yao hiyo ambalo ni la kushtua wala la kushangaza. Kubwa ambalo limetushangaza ni kwa nini wamechelewa kuileta. Baadhi yetu tulitaraia kuwa sheria kama hiyo ingekuja mapema zaidi baada ya Uchaguzi Mkuu hasa kwa vile madhara makubwa ya utawala wao yalitokea kwenye uchaguzi ule hasa pale ambapo baadhi yetu kwa kutumia mitandao tuliweza kupata na kutoa habari za uchaguzi ambazo vinginevyo zisingeweza kupatikana. JInsi marehemu Regia alivyobanwa kule Morogoro na jinsi gani Masha alivyojaribu kulazimisha matokeo yaende kinyume Mwanza Mjini ingekuwepo Sheria hii wakati ule wengi wangefungwa!
Tulijua kwa usahihi kabisa kuwa Sheria kama hii ingekuja na ingekuja baada ya kufunga mtambo wao wa mawasiliano ambao unaweza kukata mawasiliano ya mitandao yote - na hili nalitarajia usiku wa uchaguzi hasa kama mambo yataenda kombo kwa watawala. Mtambo huu kwa amri ya mtu mmoja tu unaweza kufanya mawasialiano yasipatikane kwenye mitandao (denial of service kind of an action) huku watu wakiweza kutembelea mitandao michache tu isipokuwa ile ya "kijamii". Kufungwa kwa mtambo huu wa kisasa ulikuwa ni utangulizi wa sheria na tayari umejaribiwa na vyanzo vinadokeza uko tayari kutumika kwa hilo - japo kwa sasa matumizi yake yanaonekana ni ya kawaida.
Kwa hiyo hatukushtuka na wala hatujashtuka kupitishwa kwa sheria hii. Kinachoshangaza baadhi yetu ni jinsi gani Watanzania na hasa wanaharakati wanaonekana kushtuka sasa; wadau wa mitandao nao wanashtuka sasa wakati tulionya hili miaka karibu minne iliyopita! WAnashtushwa na nini hasa? kwamba "ah hawa jamaa wanaweza kutufunga?" au "aah hawa jamaa wanataka kutunyima habari?" Mlitaka wafanye nini? Mlitaka kweli kabisa waende kwenye Uchaguzi Mkuu na uhuru uliokuwepo kabla ya uchaguzi wa 2010? Ili kiwe nini kwao?
Kinachoniudhi mimi na kinachofanya niwakebehi watawala hawa walioshindwa ni kuwa ati wanazungumza kana kwamba wanajali sana taarifa za ukweli! Watu ambao dini yao imekuwa ni uongo leo wanataka kutoa sadaka kwenye madhabahu ya ukweli? Yaani wale wale ambao kila siku hutulisha maneno yaliyojaa ulaghai leo wamekaa kwenye viti vya enzi kuwa mahakimu wa wasema uongo? Na wanasimama na macho meupe wala hawapepesi kope wakituhubiria kuwa wanataka tunaotumia mitandao tuwe wa kweli wakati wote, popote, vyovyote, kwa yeyote na lolote? Na wanasema hivyo ati kwa sababu wanawalinda Watanzania na habari za uongo, uchochezi, ulaghai au upotoshaji? Seriously! Hawa hawa?
Kama kweli 'wameokoka' na sasa wamekuwa waumini wa ukweli basi mimi nina mapendekezo machache; mapendekezo ambayo wakiyafanyia kazi basi watanishawishi kweli wanataka Watanzania wawe wa kweli. Kwanza kabisa; waanze kwenye Bunge lao wenyewe! WEnzetu wanalindwa na "kinga ya Bunge" kiasi kwamba uongo, uchochezi na ulaghai wao unalindwa! Ni mara ngapi tumesikia wakisema uongo, kejeli, matusi na hata lugha "chafu" kwenye Bunge lao na adhabu pekee wanayopeana ni "Naomba mwongozo afute kauli yake". Kama wao wanauwezo wa kufuta kauli zao za kejeli, uongo, upotoshaji, matusi n.k bila kutishiwa faini au vifungo iweje wapitishe kali kuwabana raia? Kama kweli wanaona mambo hayo hayafai wabadilishe kanuni zao kwanza na adhabu iwe kama wanazozipendekeza kwa wananchi!
Endapo Mbunge au WAziri atatoa kauli ambayo itathibitika kuwa ni ya uongo, kejeli, matusi, uchochezi n.k - na mwamusi awe chombo nje ya Bunge - basi mbunge au waziri huyo atapigwa faini kama wanazopendekeza kwa wananchi na kwa vile wao ndio watunga sheria basi vifungo vyao vitakuwa mara mbili ya vile wanavyowatakia kina wenzangu na miye! Iweje raia apigwe faini milioni tatu kwa uongo au kifungo cha miaka miwili halafu mbunge au waziri aombe radhi halafu aendelee kuzikunja na kukalia ofisi ya walipa kodi?
Kama kweli wamekuwa waumini wa ukweli; endapo yeyote kati yao atatoa taarifa kwenye mtandao (TV na Radio zinaunganishwa siyo haya ya kijamii tu) basi mtu huyo (waziri au mbunge) atapoteza nafasi yake ya Ubunge!!! Kama mnataka kuwafunga watu na kuwaondoa kwenye jamii kwanini nyinyi mkisema uongo muendelee kubaki? Na kwa sababu hiyo wao wenyewe ni lazima wawe mfano wa watu wanaosema ukweli kwenye mambo yote na wasije kutoa takwimu na majibu ya kubabaisha.
Vinginevyo, vinginevyo sheria yao hiyo haramu naamini haipaswi kutiiwa na watu wenye dhamira safi na mimi naamini ni mmoja wao. Nitaitii pale tu dhamira yangu itaniruhusu lakini si katika ujumla wake.
La mwisho ni kuwa watawala wetu wakumbuke kuwa Katiba yetu ilivyo sasa haina haki ya "Maoni sahihi" au "habari sahihi". Haki haipo duniani. Tulipotishiwa nao mwaka 2008 nilienda kwenye BBC wakati ndugu zetu kina Max wameshikiliwa na Polisi; niliuambia ulimwengu kitu ambacho bado ni kweli hata leo; haki ya maoni ni haki ya msingi. Lakini haki hii haihusishi maoni mazuri na yanayopendeza; hata maoni ya kijinga yanalindwa! Hata maoni ya kichaa yanalindwa!
Tanzania itakuwa ni nchi ya ajabu sana kulazimisha wananchi wanapowasiliana wakati wote na wao kwa wao kuanzia sasa lazima watoe maoni na taarifa zilizo sahihi! Huu ni uwendewazimu wa watawala na ni dalili ya watawala ambao muda wao wa kutawala unaelekea kwenye "the end" na sasa wanatafuta sababu ya kuuendeleza. Ni dalili za watu ambao wamelewa na ukwaju wa madaraka.
Anzeni kwanza kujifunga kamba wenyewe shingoni ndio tutaamini kuwa kweli mnaupenda ukweli kivile. Vinginevyo, mmetupa sababu ya ziada ya kuharakisha kuukomesha utawala wetu ili tuzitupilie mbali sheria zenu mbovu mlizowabebesha Watanzania miaka sasa. Sheria ambazo zimekuwa kama nira na kongwa juu yao; huku wenyewe hamko tayari kubeba hata moja. Kama kweli hiyo sheria yenu ni nzuri saaaaaana ( kwa sauti ya baba Mshami tena) ongezeni kipengele kinachojumuisha pia mijadala yenu na michango yenu Bungeni. Mkifanya hivyo hata sisi wengine tutatii.
Nje ya hapo tunatangaza -kutoitii sheria hiyo yaani civil disobedience- kwani tunaamini ni kandamizi na inayotishia haki za msingi za kiraia.
MMM
Mbiu Ya Uchaguzi
MJUMBE BLOG
Pata picha,Matukio,Taarifa,Matangazo,Habari mpya kila mara ndani na nje ya Tanzania.
No comments:
Post a Comment