Kahama. Mwanafunzi wa
darasa la tatu Shule ya Msingi Majengo, wilayani Kahama, mkoani
Shinyanga amelazwa katika Hospitali ya wilaya baada ya kunusurika kifo
kutokana na jaribio la kuchinjwa na baba yake mzazi.
Tukio hilo limekuja siku 10 baada ya mtu mmoja,
Ustadh Mohamed Kurangwa (36), kumuua mwanafunzi wa Shule ya Msingi
Nzasa, Jamal Salum (12) kisha naye kuuawa, Mbagala, Dar es Salaam.
Kurangwa alimuua Jamal nyumbani kwake Mbagala
Charambe Mianzini kwa kumchinja na kuweka kichwa cha marehemu kwenye
miguu ya mtoto huyo, kisha kuupeleka mwili wake choo cha nyumba
anayoishi muuaji. Muuaji huyo alizoa damu na kuijaza kwenye ndoo kisha
kuiweka pembeni ya nyumba yake kabla ya kuingia chumbani kwake,
kujifungia na kusoma Koran. Katika tukio la Kahama, Mganga Mfawidhi wa
hospitali hiyo, Dk Joseph Fwoma alimtaja mwanafunzi huyo kuwa ni Said
Siraji (13) na alifikishwa hospitalini hapo jana alfajiri baada ya
kuokotwa na wasamaria mwema akivuja damu shingoni.
Dk Fwoma alisema baada ya kufikishwa hospitalini,
madaktari walimfanyia upasuaji na kumshona sehemu ya koromeo aliyokatwa
na hadi jana alasiri hali yakeilikuwa inaendelea vizuri baada ya
kuongezwa damu.
Mama mzazi wa mtoto huyo, Mariamu Idd (35) alisema
mwanaye alichukuliwa na baba yake mzazi, Siraji Salvatory (45) juzi na
kwenda naye nyumbani kwake Mtaa wa Majengo kwa kuwa walitengana siku
nyingi.
Hata hivyo, jana asubuhi alipigiwa simu kuelezwa
taarifa za mtoto wake kunusurika kuchinjwa na baba yake mzazi ambaye
baada ya tukio hilo alijisalimisha polisi anakoshikiliwa hadi sasa.
Idd alisema mzazi huyo mwenziwe alikuwa akimchukua
mara kwa mara na kwenda naye nyumbani kwake Malunga na baadaye
kumrudisha akidai kuchoshwa na huduma za matibabu kutokana na mtoto huyo
kuwa na matatizo ya kiafya mara kwa mara.
Polisi wilayani Kahama wamethibitisha kutokea kwa
tukio hilo na kuongeza kuwa wanafanya uchunguzi na wakati wowote
watamfikisha mahakamani baba mzazi wa mtoto huyo.
SOURCE:MWANANCHI LEO
SOURCE:MWANANCHI LEO
Na Mjumbe Jr
Mbozi
Post a Comment