Kwa namna moja ama nyingine, hatua hiyo ya UN
imeonekana katika macho ya wengi duniani kama inalenga kuishawishi dunia
kupambana na vitendo vya ujangili katika sehemu mbalimbali duniani,
hasa Tanzania na nchi nyingine kadhaa ambazo zimeshindwa kabisa
kudhibiti vitendo vya ujangili na kusababisha mauaji makubwa ya
wanyamapori ambao wako hatarini kutoweka, wakiwamo tembo na faru.
Ni jambo la kusikitisha kuona kwamba jina la
Tanzania kwa muda mrefu sasa limetawala vichwa vya habari katika vyombo
vingi vya habari duniani kutokana na Serikali kushindwa kukomesha
vitendo vya ujangili dhidi ya wanyamapori hao walio katika hatari ya
kutoweka, ingawa imekiri wazi kwamba inayajua vizuri majangili hayo.
Siyo siri tena kwamba linapozungumziwa tatizo la
ujangili, dunia inajielekeza moja kwa moja kwa Tanzania kama marejeo.
Kama tulivyoeleza hivi karibuni katika safu hii, Tanzania inaonekana
mbele ya jumuiya ya kimataifa kama taifa ambalo halitambui kwamba
kushamiri kwa vitendo vya kuangamiza wanyamapori kutalifanya kuwa
maskini milele.
Pamoja na kushutumiwa na kusutwa kila kona ya
dunia kutokana na kutopambana na ujangili unaosababisha mauaji ya tembo
11,000 kila mwaka, Serikali bado imeshikwa na kigugumizi kutekeleza
ahadi yake ya kuteketeza tani zipatazo 90 za shehena ya meno ya tembo
yaliyohifadhiwa katika maghala yake baada ya kuzikamata kutoka kwa
wahalifu sehemu tofauti. Badala yake imekuwa ikifanya juhudi kwa muda
mrefu ikitaka ipewe kibali cha kuuza shehena hiyo, lakini juhudi hizo
zimegonga mwamba.
Pengine ni vyema tukakumbuka kwamba hadi miaka ya
hivi karibuni, Serikali imekuwa na mkakati wa kuzishawishi nchi
zilizosaini Mkataba wa Kimataifa Dhidi ya Biashara ya Wanyamapori na
Mimea Iliyo Katika Hatari ya Kuangamia (CITES), ili iuze shehena hiyo
katika soko la kimataifa. Pamoja na msimamo wake kwamba fedha hizo
zingesaidia katika vita yake dhidi ya ujangili, nchi hizo ikiwamo Kenya
zilipinga vikali ombi hilo.
Hali ya nchi kushutumiwa na kuaibishwa kimataifa
ilijitokeza pia jijini London wakati wa kongamano lililoitishwa na
Serikali ya Uingereza kujadili mbinu za kulinda wanyamapori dhidi ya
ujangili. Kongamano hilo lilihudhuriwa na wajumbe kutoka nchi 46,
wakiwamo marais wanne kutoka Afrika na wakuu wa mashirika 11 ya
kimataifa. Tanzania ndiyo iliyoonekana kuwa katikati ya masikitiko na
shauku za wajumbe wa kongamano hilo kutokana na ukubwa wa tatizo la
ujangili hapa nchini.
Ni wakati wa kongamano hilo, ndipo ujumbe wa
Tanzania ulioongozwa na Rais Jakaya Kikwete ulipotangaza kwamba umefuta
mpango wake wa kuuza shehena ya meno ya tembo, pengine ikiwa ni hatua ya
kuonyesha kwamba Tanzania sasa inayo dhamira ya kupambana na ujangili
na biashara ya meno ya tembo.
Muda mrefu umepita sasa tangu ahadi ya kuteketeza
shehena ya meno ya tembo ilipotolewa. Sisi tunauliza: Kama kweli
Serikali imedhamiria kupambana na ujangili na kuionyesha dunia kuwa ina
dhamira ya kweli, ni sababu zipi zinazokwamisha utekelezaji wa ahadi
hiyo?
Na Mjumbe Jr
Mbozi
Post a Comment