Bibi
mmoja raia wa Nigeria, Olabisi Ibidun Cole (65) amevunja rekodi ya umri
wa watu wanaokamatwa wakiwa na dawa za kulevya katika Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).
Cole
alikamatwa Jumatatu akiwa amemeza kete 82 aina ya heroini zilizokuwa
zimefungwa kwenye karatasi zinazofanana na ganda la sigara, ambazo si
rahisi kuonekana katika mitambo.
Habari
zilizopatikana na kuthibitishwa na Mkuu wa Kitengo cha Kupambana na Dawa
za Kulevya, Alfred Nzowa zimesema pamoja na mbinu zake na kujiamini,
mwanamke huyo alikamatwa kutokana na ushirikiano wa vitengo mbalimbali
vya uwanja wa ndege.
Kamanda
wa Polisi wa Uwanja wa Ndege, Hamisi Selemani alisema mwanamke huyo
alikamatwa Mei 19, mwaka huu saa tisa alasiri akijiandaa kwenda Paris,
Ufaransa kwa ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia.
Selemani
alisema raia huyo aliwasili nchini Mei 15, mwaka huu na alikaa muda wote
bila ya kuwa na shughuli yoyote, jambo ambalo lilitiliwa shaka na
kumkamata.
"Huyu
mwanamke achana naye, akisimama mbele yako huwezi ukaamini kwa jinsi
anavyojiamini. Alikuwa na mbinu mpya ya kufunga hizo kete. Kila moja
ilifungwa kwa karatasi inayofanana na ganda la sigara," alisema
Selemani.
Alisema mwanamke huyo alitumia mbinu hiyo ili asigundulike wakati akikaguliwa kwa mitambo maalumu inayogundua dawa za kulevya.
Taarifa
zaidi zinasema kuwa kutokana na mbinu yake ya ufungaji wa kete, mwanamke
huyo alikuwa tayari amevuka hatua ya kwanza ya ukaguzi.
Nzowa alisema baada ya kumhoji, mtuhumiwa huyo alidai kuwa aliingia nchini kwa ajili ya kutafuta soko la kuuza vipodozi na nguo.
"Wakati
tukiendelea kumhoji, Kikosi Kazi cha Kuthibiti Dawa za Kulevya kilibaini
na kugundua kuwa alikuwa amemeza dawa za kulevya.
"Huyu ni
mzee, lakini tumeshangaa kuona bado ana nguvu za kutosha na tulishangaa
baada ya kutoa kete 20 kwa mara moja katika awamu ya kwanza, jambo hili
si rahisi kutokana na umri wake," alisema Nzowa.
Mtuhumiwa huyo aliyekuwa na hati ya kusafiria ya Nigeria, anaendelea kuhojiwa na upelelezi ukikamilika atafikishwa mahakamani.
Chanzo:Mjengwa blog
Post a Comment