TANZANIA YAPATA MEDALI YA DHAHABU YA KWANZA! MJUE ALIYE IPA HESHIMA HIYO NCHI YETU HAPA!
Dar es Salaam.
Mwanariadha wa Tanzania, Sabas Daniel ameibuka kinara kwenye fainali ya kurusha mkuki na kutwaa medali ya dhahabu kwenye mashindano ya Shule za Sekondari za Jumuiya ya Afrika Mashariki (Feasssa).
Daniel amekuwa Mtanzania wa kwanza kutwaa medali ya dhahabu kwenye mashindano hayo yanayoendelea kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, akiwa amerusha umbali wa mita 55:56.
“Nimefarijika kushinda medali hii, nashukuru kocha wangu na uongozi wa shule kwa maandalizi waliyonipa,” alisema
Daniel mwanafunzi wa Lord Barden Powel. Ocaya Samuel wa Uganda alikamata nafasi ya pili baada ya kurusha umbali wa mita 55:33 na James Malul wa Sudan Kusini alikamata nafasi ya tatu akirusha mita 54:24.
Kwenye mbio za mita 200 na 100, mwanaridha Jane Maiga alitwaa medali za fedha akikimbia kwa sekunde 12:06 kwenye mita 100 na sekunde 25:05 kwenye mita 200.
Nafasi ya kwanza kwenye mbio za mita 100 ilichukuliwa na Jesca Ilau wa Uganda aliyekimbi kwa sekunde 12:02 na Casty Kendi wa Kenya alikamata nafasi ya pili akikimbia kwa sekinde 12:05.
Kwenye fainali ya mita 200, Maximila Imali wa Kenya aliibuka kinara akikimbia kwa sekunde 23:07 na Agness Apio wa Uganda aliyekimbia kwa sekunde 25:03 akikamata nafasi ya pili.
Kwenye mpira wa kikapu, Lord Barden Powel imetinga nusu fainali itakayochezwa leo baada ya jana kuigalagaza F S K ya Kenya kwa pointi 66-48 kwenye mchezo wa robo fainali uwanjani hapo.
Lord Barden Powel iliyokuwa ikiongozwa na Sihaba Said na Enock Maengela ilimaliza kota zote nne kwa matokeo ya pointi 26-14, 14-5, 11-15 na 15-14.
Kwenye netiboli, timu za Tanzania za Kizuka na Jitegemee zilipoteza mechi zake za jana za kuhitimisha hatua ya makundi ambapo kizuka ilifungwa magoli 67-14 na St Mery’s Kitende ya Uganda na jitegemee kufungwa na Kibuli ya Uganda magoli 49-16.
Kwa matokeo hayo, Uganda imeingiza timu zote kucheza nusu fainali itakayochezwa leo uwanjani hapo, ambazo ni London College na St Juliana kwenye Kundi A na St Mery’s Kitende na Kibuli kwenye Kundi B.
Chanzo: Mwananchi
Post a Comment