
Bunge limehitimisha mjadala wa
Kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow kwa
kupitisha maazimio manane, likiwamo la
kuwawajibisha Waziri wa Nishati na Madini,
Profesa Sospeter Muhongo na Waziri wa
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
Profesa Anna Tibaijuka.
Wengine waliowajibishwa pamoja na
mawaziri hao ni Mwanasheria Mkuu wa
Serikali, Frederick Werema, na wajumbe wa
Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Umeme
Nchini (Tanesco) na kuwavua nyazifa zao
wenyeviti watatu wa kamati za kudumu za
Bunge.
Wenyeviti waliovuliwa nyadhifa zao ni
Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini,
Victor Mwambalaswa, Kamati ya Katiba,
Sheria na Utawala, William Ngeleja na Kamati
ya Bajeti, Andrew Chenge. Viongozi hao
wamevuliwa nyadhifa zao chini ya azimio la
Bunge namba mbili.
Maazimio hayo mapya manane yalisomwa
bungeni jana jioni na Mwenyekiti wa Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali
(PAC), Zitto Kabwe.
Akizungumza bungeni Zitto alisema, mabilioni
ya fedha yaliyotolewa kwenye Akaunti ya
Tegeta Escrow yametumika kuwapa kile
kinachoonekana kuwa ni rushwa.
Zitto alisema baadhi ya watu waliochukua
fedha hizo ni viongozi wa umma na maofisa
wa Serikali kama mawaziri, majaji, wabunge,
wenyeviti wa kamati za Bunge, wakuu wa
taasisi za umma, viongozi wa dini, mawakili
wa kujitegemea na watu binafsi.
“Vitendo vilivyofanywa na watu hawa
vinaashiria uzembe na makosa mbalimbali ya
jinai kama vile wizi, ubadhilifu kutakatisha
fedha haramu, matumizi mabaya ya
madaraka, rushwa na kupokea mali ya wizi,”
alisema.
Alitaja azimio la kwanza la Bunge ni kulitaka
Jeshi la Polisi na vyombo vingine husika vya
ulinzi na usalama vichukue hatua stahiki kwa
mujibu wa sheria za nchi yetu.
Zitto alisema watu wote waliotajwa na taarifa
maalumu ya kamati kuhusika na vitendo
vyote vya kijinai kuhusiana na miamala ya
Akaunti ya Escrow na watu wengine
watakaogundulika kufuatia uchunguzi
mbalimbali unaoendelea kuhusika katika
vitendo hivyo vya jinai, watachukuliwa hatua
stahiki kwa mujibu wa sheria.
Azimio la tatu ni kuzitaka Kamati husika za
kudumu za Bunge zichukue hatua za haraka
na kwa vyovyote vile kabla ya mkutano wa 18
wa Bunge kuwavua nyazifa zao za wenyeviti
wa kamati husika za Bunge. Zitto alitaja
azimio la nne ni la kumuomba Rais auende
Tume ya kijaji kuchunguza tuhuma za utovu
wa maadili dhidi ya Jaji Aloysius Mujulizi na
Jaji Profesa Eudes Ruhangisa wa Mahakama
Kuu ya Tanzania.
Alisema utaratibu wa kushughulikia nidhamu
za majaji kwa mujibu wa Katiba unamtaka
Rais kuunda Tume ya Uchunguzi ya Kijaji,
kuchunguza tuhuma za utovu wa maadili
dhidi ya majaji.
Pia azimio la tano ni mamlaka husika za
kifedha na za kiuchunguzi kuitaja Benki ya
Stanbic na benki nyingine yoyote
itakayogundulika kufuatia uchunguzi wa
mamlaka za kiuchunguzi, kujihusisha na
utakatishaji wa fedha zilizotolewa katika
Akaunti ya Escrow, kuwa taasisi zenye shaka
ya utakatishaji wa fedha haramu.
Rejea:Mwananchi.
LIKE ukurasa wetu MJUMBE BLOG facebook kwa Matukio na Habari za Mara kwa mara.
©Mjumbe Blog Volunteers
Post a Comment