ERIC SHIGONGO ATOA UJUMBE MZITO KWA VIJANA WANAO TAMANI MAFANIKIO!
VIJANA NA MAFANIKIO
Nimewahi kuzungumza na vijana wengi, ofisini, nje ya ofisi na hata sehemu nyingine nyingi, kwa kila kijana ninayezungumza naye, ananiambia jambo moja kwamba angependa kufanikiwa, je ni njia gani ambazo ataweza kuzifuata ili afanikiwe, awe na biashara kubwa, aingize kiasi kikubwa cha fedha na kupata mafanikio makubwa.
Najua kwamba mbali na hao niliowahi kuzungumza nao, pia wapo wengine ambao wanatamani sana kufanikiwa. Kufanikiwa hakuji ghafla huku ukiwa umekaa chumbani kwako ukipepewa na feni lako, ili ufanikiwe, yakupasa kujitoa kwa kile unachokifanya.
Kuna vitu ambavyo vinawapoteza sana vijana na mwisho wa siku kuyaona mafanikio yakiwakimbia, vitu hivi ni starehe na uvivu wa kujitolea katika kufanya kazi. Unaweza kumkuta kijana ana kiu hasa ya mafanikio lakini tatizo lake anapenda sana starehe likiwepo na suala la kunywa pombe kupitiliza.
Una kipato kidogo ambacho unaingiza kila siku au kila mwezi, lakini cha ajabu, kipato hichohicho unakigawa katika unywaji wako wa pombe au hata kwenda klabu nyakati za usiku, kisha kesho asubuhi, unaanza kulalamika kwamba kwa nini haupati mafanikio.
Ndugu yangu, kupata mafanikio kunahitaji kujitoa na ndiyo maana wengine wakaanzisha msemo kwa kusema fanya kazi kama mtumwa ili baadae uishi kama mfalme.
Usiangalie cheo chako, sehemu unapoishi au aina ya watu unaoishi nao, unapopata nafasi ya kufanya kazi, ifanye kama mtumwa, jitoe, sulubika, hangaika, acha utoke sana jasho lakini nakuhakikishia mwisho wa siku, utakuwa ndani ya nyumba au ofisi yako ukipulizwa na kiyoyozi.
Hakuna aliyewahi kuwa tajiri kwa kukaa ndani tu, wapo matajiri ambao zamani walikuwa washona viatu, wapo matajiri ambao zamani walikuwa madereva wa daladala na kazi nyingine pia. Lakini kupitia kujitoa kwao, kuona kwamba mishahara wanayoipata haitoweza kuwatoa hapo walipo, wakaanzisha biashara ambazo mpaka leo hii wamekuwa matajiri wakubwa Tanzania au duniani kwa ujumla.
Kijana unayetafuta mafanikio, JITOE, Mungu hataki uwe hapo ulipo, bado una nafasi kubwa ya kuyafikia mafanikio kama wengine, kama wale wameweza, kwa nini wewe ushindwe? Wao wana nini na wewe umekosa nini? UNAWEZA, pambana na ninakuahidi kwamba utafanikiwa na kuwa kama wao, au hata zaidi yao.
E.J SHINGONGO

Post a Comment