NEC YATOA TAMKO KUHUSU TAREHE ILIYO PANGWA KUPIGIA KURA KATIBA PENDEKEZWA!
Tume ya uchaguzi(NEC) ime sema muda ulio bakia kabla ya tarehe iliyo pangwa ya kuipigia kura ya maoni katiba hautoshi kuandikisha wapiga kura wote.
Imedai hadi sasa ime pokea vifaa 250 kati ya 9000 ilivyo agiza kabla ya mwisho wa mwaka.
PATA HABARI YOTE KWA KINA HAPA CHINI:
By :
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, ametabiri kukwama kwa kura ya maoni kuhusu Katiba pendekezwa, akieleza kuwa maandalizi hafifu ambayo yamefanyika hadi sasa hayaruhusu zoezi hilo kufanyika.
Aidha, amesema iwapo kutatokea ujanja ujanja wowote wa kutaka kukiuka sheria ya kura ya maoni, nchi itaingia kwenye matatizo.
Akizungumza katika mahojiano na NIPASHE jana, Jaji Warioba alisema wiki iliyopita, wajumbe wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, walikutana na majadiliano yao yalijikita kwenye maandalizi ya kura ya maoni kuhusu Katiba pendekezwa.
Alisema sheria namba tatu ya mwaka 2014, ambayo inahusu kura ya maoni inaeleza kuwa jambo la kwanza kufanyika ni uboreshaji wa daftari la wapigakura, ambalo utafuatiwa na elimu kwa umma kwa miezi miwili kisha kampeni kwa mwezi mmoja.
“Tukaona kuna umuhimu wa kufanya maandalizi kwa umakini mkubwa kabisa, tumeichambua sheria hii ya kura ya maoni, tumeona mahitaji ya sheria hii lakini utaratibu wa sheria hauanzi mpaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imeanza aundikishaji wa wapigakura,” alisema.
ELIMU KWA UMMA
Akizungumzia msingi wa elimu kwa umma, Jaji Warioba alisema NEC inapaswa kufanyakazi hiyo kwa kushirikiana na asasi za kiraia kwa kipindi kisichopungua miezi miwili ili kuwaelimisha wananchi nini kilichopo ndani ya Katiba na utaratibu wa kura ya maoni.
“Kwa hiyo tuna miezi mitatu, ratiba iliyowekwa na serikali inasema wanakamilisha kuandikisha Machi kisha kampeni inaanza mara moja. Kipindi cha elimu hakikuwekwa kwenye ratiba. Mimi nafikiri ni vizuri kufuata sheria kwa sababu tukiendesha hii kinyume cha sheria inaweza kuleta matatizo,” alisema.
Jaji Warioba aliongeza kuwa: “Na kama tukifuata sheria inavyosema, ni kwamba NEC ikimaliza kazi Machi; Aprili na Mei itakuwa ni elimu, Juni ni kampeni kwa hiyo kura ya maoni itakuwa ni Julai.”
Hata hivyo, alisema kura hiyo kufanyika Julai ni matatizo kwa sababu ni wakati ambao maandalizi ya uchaguzi mkuu yatakuwa yameanza na itakuwa kipindi vyama vya siasa vinakuwa vinateua wagombea wake.
“Ukafanye yote kwa pamoja inaweza kuleta matatizo lakini muhimu tunalosema tuifuate sheria kuwepo na kipindi cha elimu kwa umma.”
KAMPENI
Alisema sheria hiyo inataka baada ya elimu kwa umma, ziundwe Kamati mbili katika ngazi ya Taifa na ngazi ya jimbo, zitakazoendesha kampeni kwa mwezi mmoja, huku moja ikiunga mkono Katiba pendekezwa na nyingine ikiipinga.
“Kamati ya moja itakuwa inawaambia wananachi wapige kura ya ndiyo na kamati ya pili itakuwa inawaambia waikatae wapige kura ya hapana,” alisema.
Alisema kamati zote hizo zitatakiwa kuwa na viongozi wanajulikana na ijulikane mapato ya kampeni yatatoka wapi na wananchi wajue kampeni zitakavyoendeshwa.
“Hizi kamati hazijaundwa na ni lazima ziundwe na ziandikishwe kwenye tume ya uchaguzi,” alisema.
Jaji Warioba alisema maandalizi hayo hayajafanyika na haijulikani itafanyika lini na kwa namna gani.
UBORESHAJI WA DAFTARI
Alisema NEC inatumia utaratibu wa kuandikisha wapigakura kwa njia ya kielektroniki (BVR), ambao alisema ni mzuri na unaoweza kuzuia udanganyifu.
Alisema utaratibu wa BVR unafuta wapigakura wadanganyifu ambao wamekuwa wakijiandikisha zaidi ya mara moja, lakini NEC italazimika kufanya uhakiki baada ya kumaliza kuandikisha wapigakura.
Alisema uandikishaji huo ulitumika Malawi mwaka 2004, lakini uliibua malalamiko kwa kuwa wakati wa uandikishaji serikali ya nchi hiyo haikupata muda wa kuhakiki taarifa za wapigakura.
Alisema mfumo wa BVR unafuta majina ya wapigakura watakaojiandikisha zaidi ya mara moja na kubakisha jina kwenye kituo atakachokuwa amejiandikisha mara ya kwanza, hivyo ili kuepuka malalamiko hayo hata hapa nchini ni vyema uhakiki ukafanyika.
“Ukitumia utaratibu huu, ukimaliza unatakiwa uhakiki, bandika vituoni kila mtu aone. Ambaye hataona jina lake mfumo huo utamwonyesha jina lake lilipo,” alisema.
Alisema zoezi la uandikishaji unaofanywa sasa na NEC linawahusisha pia vijana watakaoshiriki uchaguzi mkuu ambao ifikapo Oktoba watakuwa wametimiza miaka 18.
“Ukiwaandikisha sasa hivi, wakijakupiga kura ya maoni watakuwa hawajafikisha miaka 18, usipowaandikisha sasa hivi, ikifika Oktoba hawatakuwa na haki ya kupigakura, tukaona hilo tatizo kwa hiyo tunaona maandalizi yafanywe,” alisema.
Alisema bila kufanya maandalizi, kunaweza kuwa na wapigakura wasio na sifa au wanaweza wakakwama kushiriki uchaguzi mkuu.
Serikali imepanga kura ya maoni kufanyika Aprili mwaka huu, ingawa makundi mbalimbali ya jamii yanaeleza wasiwasi kwamba kutokana na maandalizi hafifu, uwezekano wa kufanyika kwa kura hiyo ni mdogo.
Baadhi ya mambo yanayohojiwa ni kutosambazwa kwa nakala za Katiba inayopendekezwa kwenda kwa wananchi ili waisome na kuielewa Katiba inayopendekezwa kabla ya kuipigia kura kuikubali au kuikataa.
WANANCHI VUNJO
Alisema kuhusu wananchi wa Vunjo, mkoani Kilimanjaro ambao wamemchangia ili akawape elimu ya Katiba, alisema wajumbe wa iliyokuwa tume yake wataendelea kutoa elimu kwa kutumia rasilimali na uwezo usio na mashaka na usioegemea upande wowote.
“Sisi tunafanya, lakini moja ambalo tuko makini kabisa hatutaki kuonekana tunaungana na kundi lolote. Tunasema tukiwa na uwezo tutaendelea kutoa elimu lakini uwezo ule ni uwezo ambao hauna mashaka, hatutaki kuonekana tunajiunga na kundi lolote,” alisema.
Chanzo: Nipashe
MJUMBE BLOG
Tuna kushukuru kwa kukubali tukuhudumie.
Karibu tena.
MJUMBE BLOG
Tuna kushukuru kwa kuamua kutumia huduma zetu.
Karibu tena.
Post a Comment