Ndugu zangu,
Yumkini Idd Amin alitia shaka uwezo wetu wa kulipiza kisasi. Watanzania ni wakali sana wanapochokozwa. Februari 27, 1978, siku kama ya leo, baada ya kupokea amri ya kusonga mbele kutoka kwa Amiri Jeshi Mkuu, Julius Nyerere, Vijana wetu Wapiganaji, asubuhi kama ya leo walikuwa wameukamata mlima Gayaza na jioni yake Mji wa Mbarara ulitekwa. Anaandika Yoweri Museveni ( Sowing The Mustard , Seed, pg 99)
NA Maggid Mjengwa
William Kaijage Maggid
Vita ilianza rasmi tarehe 30-Oct-1978 na iliisha rasmi tarehe 11-Apr-1979 (miezi mi-5, wiki 1 na siku 5). Tarehe iliyotajwa nina wasiwasi kama kulikuwa na vita.
Endelea kusoma Maelezo Zaidi:
Inaelekea waTanzania wengi wamesahau historia kati ya Libya na Tanzania. Marehemu Gaddafi alikuwa rafiki yake mpenzi nduli mshenzi Dikteta Idi Amin Dada wa Uganda! Gaddafi alitaka Amin amwoe binti yake! Gaddafi alituma wanajeshi kutoka Libya kuwasaidia Uganda katika vita vya Kagera mwaka 1978-79. Sisi wazee tunaukumbuka huo vita na miezi kumi na nane (miaka 18) ya shida iliyofuata! Maoni chini yameandikwa na mwanachama la kundi - Wanabidii
Wanabidii!
Binafsi nachukia sana kuandika bila ya ushahidi! Na zaidi sipendi kuandika "propaganda" na taarifa za uzushi; isipokuwa napenda kuandika taarifa zilizotafitiwa kwa kuandikwa na mtafiti mwenyewe (na au mwandishi aliyeandika matokeo ya utafiti au kufanya upembuzi wa utafiti husika). Takriban wiki moja sasa (tangu Alkhamis ya tarehe 20 Oktoba, 2011) uwanja wa "Wanabidii" na majukwaa mengine ya kijamii yamekuwa yakijadili "Kuuawa kwa Kanali Muammar Gaddafi" kulikofanywa na wale wanaoitwa waasi (wa NTC) wakisaidiwa na NATO wakiongozwa na Uingereza, Marekani, Ufaranza na washirika pamoja na Waarabu (Saudia na Qatar). Gaddafi ameuawa; kwa jinsi gani, kila mmoja amesoma, ameona (kwenye picha za mnato) na au kwenye picha za video!
Ninachotaka kuandika na pengine kuanzisha "mjadala" wa kiakili ni juu ya "GADDAFI KUMSAIDIA IDI AMIN DADA KWENYE VITA VYA KAGERA [UGANDA DHIDI YA TANZANIA MWAKA 1978 HADI 1979]". Napenda niweke wazi kwamba, "historia haisomwi ili kufufa 'chuki' bali husomwa kujua yaliyopita, kuyasanifu yaliyopo na kupanga mipango kwa yajayo!". Hivi ndivyo tunavyosoma historia iwe yenye kuhuzunisha au kufurahisha! Tanzania ilipigana vita na Uganda, vita iliyoitwa VITA YA KAGERA (japokuwa ilipiganwa hata ndani ya Uganda na Idi Amini Dada kufurushwa na kuikimbia Ugnda!).
Kwa ujumla, tangu pale kifo cha Muammar Gaddafi kilipotangazwa kwa mara ya kwanza na kituo cha runinga cha Al-Jazeera na kukaririwa na vituo vingine na mashirika ya habari ya kimataifa kama BBC, CNN, Reuters, Xinhua, AFP, AP na IRNA (Press Tv) kumekuwa na mchanganyiko wa "mawazo" kwa wananchi wa Tanzania juu ya "hali" ya Gaddafi kisiasa katika mtazamo wa kifalsafa...hususan wengi wa wachangiaji kwenye mijadala hiyo wanamuona Muammar Gaddafi kama "shujaa" na "mwanamapinduzi" na "kiongozi mtukuka" na "aliyejitolea kuunganisha Afrika" na hata wengine kufikia kiasi cha kuonyesha kwamba hajawahi kutokea kama Muammar Gaddafi na hata kumpa "daraja" ya kuwa "Baba wa Afrika" na mshumaa uliyozimika! Hata hivyo wengi wamesahau kamba ni Muammar Gaddafi ndiye aliyemsaidia Idi Amin Dada kwenye Vita vya Kagera! Naomba sasa tuangalie nini alifanya Gaddafi wakati wa vita vile.
Vita vinahitaji rasilimali watu (askari na wataalamu wa kijeshi), fedha za kuendeshea vita na zana (za kivita na za mawasiliano ya kivita). Kwa mujibu wa taarifa rasmi na zinazothibitishwa na taarifa rasmi za kihistoria Muammar Gadafi alimpa Idi Amin Dada usaidizi ufuatao:
1. WANAJESHI (WAPIGANAJI) 3,000 (Elfu tatu kutoka Libya na nchi zilizokuwa na mahusiano na Libya ambazo Gaddafi likuwa anazisaida na zenye uzowefu wa mazingira ya vita [military knowhow and skills on interlocustrine terrain]);
2. ZANA KAMA VIFARU AINA YA T-54, T-55, BTR, APCs, BM-21, Katyusha MRLs;
3. MIZINGA; na
4. NDEGE ZA KIJESHI AINA YA MiG-21s na Tu-22 Bomber.
Wanajeshi wa Libya waliyotumwa Uganda walikuwa katika makundi yafuatayo: ASKARI WA KAWAIDA; WANAMGAMBO; NA ASKARI WA VITA VYA MSITUNI (WENYE UZOWEFU WA VITA VYA KIENYEKI KUTOKA JANGWA LA SAHARA [MAARUFU KAMA WATUAREG KUTOKA TCHAD, NIGER, ALJERIA NA DARFUR]). Hata hivyo, shukrani za pekee kwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (TPDF) waliyefanyakazi ya ziada ya kujitoa mhanga kupigana "kiume" na hatimaye kuyashinda majeshi ya Idi Amin Dada akisaidiwa na Muammar Gaddafi. Hata ilipofika mwezi wa Aprili, 1979 na Idi Amin Dada alipopoteza udhibiti wa nchi ya Uganda aliamua "kuikimbia" Uganda na kituo chake cha kwanza kilikuwa Libya (kwa Muamar Gaddafi) na alipewa "hifadhi" ya muda na baadaye kwenda "uhamishoni" nchini Saudi Arabia (alikoishi hadi kufa kwake akiwa Jeddah).
Kwa wasomaji na "wanabidii" na wengine wanaomtazama Muammar Gaddafi kwa kusahau "aliyoyafanya" dhidi ya kumsaidia Idi Amin Dada kuendesha vita na Tanzania nadhani wana wajibu wa kujiuliza masuala haya (hii ni pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo inawajibu wa kusema ukweli):
1. Wamesahau "hadithi" hii ya Vita vya Kagera? Au, vita hivi vilikuwa "propaganda" ya kisiasa?
2. Gaddafi alidhamiria nini kumsaidia Idi Amin Dada aliyeapa kuisambaratisha nchi (Tanzania) na kwa kuanzia aliteka Kagera na kuifanya sehemu ya Uganda?
3. Kama Idi Amin Dada wa Uganda alitangazwa "dikteta", "bundi", "joka", "fisi mla watu", na masimulizi mengine ya kutisha (hata ya kula nyama za watu); mtu aliyekuwa akimsaidia mtu wa aina hiyo (kama Gaddafi) anaitwaje?
4. Je, historia ya Vita vya Kagera iliandikwa kwa wino "gani" hadi leo imesahaulika?
5. Au, wote wanaodhani kwamba Muammar Gaddafi ni "shujaa" wa Afrika wamezaliwa miaka ya 1980? Na kwa jinsi hiyo hawajui kilichotokea kati ya miaka ya 1978 na 1979?
Mwisho, siandiki haya katika kuwakumbusha "majonzi" wananchi wa Kagera waliyeuawa kikatili na Idi Amin Dada; siwakumbushi machungu ya kutiwa vilema vya maisha; siwakumbushi madhila ya "kubakwa" wanawake kulikofanywa na askari wa Idi Amin Dada; na wala siwakumbushi jinsi mali zao (mashamba na nyumba) zilizvyoharibiwa na "ushenzi" wa Idi Amin Dada! Nataka niwakumbushe kwamba, "hatuwezi kurudisha nyuma historia; lakini ni wajibu kuisoma ili vizazi vijavyo vipate kumbukizi yenye kujenga mujtamaa wao." Gaddafi alikuwa "rafiki" na wakati huohuo alikuwa "adui" kwa vile alikuwa na "sura mbili ndani ya moja".
Na kwa serikali (iliyoonekana kumuunga mkono); hii ni dhana (binafsi) inawezekana Muammar Gaddafi alilipa sehemu ya "maumivu" ya vita alivyomsaidia rafiki yake mpenzi Idi Amin Dada...kama ndivyo, basi ni vema watuambie! Hatuwezi kusomeshwa historia ya "uongo" juu ya Muammar Gaddafi kumbe "mtu" huyu (yaani Gaddafi) alikuwa "mtu mwema" na kiongozi "mzuri" kuliko hata Mzee Mandela na Mwalimu Nyerere...naomba tuwe "wakweli" na kwa kusisitiza: UKWELI UTATUWEKA HURU; KAMA GADDAFI ALIKUWA RAFIKI WA AFRIKA KWA NINI ALIMSAIDIA IDI AMIN DADA KUTUPIGA? TAFAKARI SEMA UKWELI JAPOKUWA UKWELI WENYEWE NI DHIDI YA NAFSI YAKO!
Bakari M Mohamed, BBA[PLM], CPSP[T], MSc (PSCM)
MJUMBE BLOG Tunashukuru kwa kutupa fursa ya kukuhudumia mtandaoni;karibu tena.
Post a Comment