![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEiS9if-nPenmep8WSZopT9jZAUWfOiOpJq82lTtXKbIMzoJrQcD1u-emDJXq_wqJPVudJBi7dPiEceNmy-QIOx87a4DR41awi7YcVp9mlu_yfx09UW4EkG3kz1A294jHv4BXZxDoWMy1Loo/s640/1430501725533.jpeg)
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimepinga serikali kujihusisha na kampeni ya kuwataka wananchi waipigie kura ya ndiyo Katiba inayopendekezwa kwa kutumia rasilimali za Watanzania na kushangazwa na kitendo chake cha kuzuia taasisi za dini zinazotangaza kuipinga.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dk. Hellen Kijo-Bisimba, alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, jijini Dar es Salaam juzi.
“Sote tunakumbuka tamko la Jukwaa la Wakristo Tanzania kuhusu Katiba inayopendekezwa. Jukwaa liliwataka waumini wake wote wajitokeze kwa wingi kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapigakura, waisome na kushiriki kikamilifu vipindi vya elimu juu ya Katiba inayopendekezwa na kisha wajitokeze kwa wingi kupiga kura ya hapana kwa katiba hiyo.
Jambo hili lilipingwa vikali na serikali kwamba tamko la Jukwaa limewawekea mipaka ya kidemokrasia waumini wake,” alisema Dk. Bisimba.
Alisema LHRC imeshangazwa kwamba licha ya serikali kuzuia taasisi za dini kuendelea na msimamo wao, yenyewe imekuwa kinara wa kuvunja sheria kwa kulazimisha Watanzania kupiga kura ya ndiyo kuhusu katiba hiyo.
Dk. Bisimba alisema kitendo cha serikali kuwaelekeza Watanzania kupigia kura ya ndiyo katiba hiyo siyo sahihi kisheria. Alisema hoja hiyo ya LHRC inatokana na ukweli usiopingika kuwa mchakato wa kupata katiba mpya umetawaliwa na ubabe.
“Ukweli ni kwamba Sheria ya Kura ya Maoni imetoa mwanya wa kufanya kampeni ya kura ya ndiyo na hapana ya Katiba inayopendekezwa. Hivyo, kampeni ya ndiyo haiko juu ya hapana, zote zina nafasi sawa na zinatakiwa zijadiliwe kwa usawa mbele ya sheria za nchi na hakuna mwenye haki zaidi au hatimiliki za taifa la Tanzania kuzidi Watanzania wengine,” alisema Dk. Bisimba.
Aliitaka serikali kuacha mara moja kupiga kampeni ya ndiyo kuhusu katiba hiyo, kwani kufanya hivyo ni kuvunja sheria na ni kuwaaminisha Watanzania wafikiri kwamba kufanya kampeni ya kura ya hapana ni kosa.
Alisema kitendo cha serikali kuhama katika nafasi yake ya kusimamia na kujiingiza katika kushabikia upande, ni sawa kabisa na mwamuzi wa mchezo kuwa mwanachama, mshabiki na mchezaji wa mojawapo ya timu zinazocheza, huku yeye akiwa ndiye mwamuzi.
Alitoa mfano kuwa serikali imewaagiza wakuu wa wilaya na mikoa kuwaelekeza wananchi kuipigia kura ya maoni katiba inayopendekezwa wakati muda wa kufanya hivyo bado.
“Kwa lugha nyingine ni sawa na shauri ambalo kuanzia hakimu, mwendesha mashitaka na mshtaki kuwa ni mtu yule yule. Kinachozidi kudhihiri wazi ni kuwa baadhi ya viongozi na wanachama wa CCM na serikali hawataki kabisa Watanzania waufahamu ukweli kuhusu upungufu mkubwa ulioko katika Katiba inayopendekezwa,” alisema Dk. Bisimba.
Alisema wanao ushahidi wa baadhi ya wakuu wa mikoa na wilaya, kama vile Rungwe na Kyela, mkoani Mbeya, ambao waliwakataza wafanyakazi wa LHRC kutoa elimu ya uraia katika wilaya zao kwa hofu kuwa wananchi watang’amua upungufu katika katiba hiyo na kuipigia kura ya hapana.
Hivyo, aliwataka wananchi kufahamu kuwa siyo uhaini kuipigia kura ya hapana katiba hiyo na wala siyo utakatifu kupiga kura ya ndiyo.
“Isipokuwa kila mwananchi yuko huru kushiriki kikamilifu na kuamua kwa hiari yake akiwa na ufahamu sahihi kuhusu jambo analoliamua pasipo kuburuzwa,” alisema Dk. Bisimba.
Alisema suala la matumizi mabaya ya madaraka na kuweka kampeni za upande mmoja katika kaulimbiu za kitaifa, hawawezi kulifumbia macho, likiachwa linaweza kujitokeza tena kwenye sherehe nyingine za kitaifa, litaminya uhuru wa wananchi kupata elimu ya uraia kuhusu maudhui ya hiyo na kushindwa kufanya maamuzi sahihi muda wa kupiga kura ya maoni utakapofika.
NA RICHARD MAKORE
CHANZO: NIPASHE
MJUMBE BLOG
Ni Ukurasa wa Habari,Picha,Matukio,Matangazo.
#KUJERUHI hisia za watu/mtu si Kusudi letu.
MAONI PIGA:0752025002
Post a Comment