Unknown Unknown Author
Title: LIPUMBA:RAIS AJAYE AUNGANISHE WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO YA UCHUMI...
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
"Ukweli ni kwamba tumejiparanganisha wenyewe ndani ya UKAWA.Kwa hio watanzania watakuwa na wanaCCM wawili wanaogombea urais wakati ...


“Ukweli ni kwamba  tumejiparaganyisha wenyewe
"Ukweli ni kwamba tumejiparanganisha wenyewe ndani ya UKAWA.Kwa hio watanzania watakuwa na wanaCCM wawili wanaogombea urais wakati Ukawa tulikuwa na wagombea watatu na tulikubaliana Dk Slaa apeperushe bendera"Prof Lipumba
Baada ya miaka 54 ya uhuru wa Tanganyika, Watanzania wengi ni masikini wa kutupwa. Watoto 42 katika kila 100 wamedumaa. Hawana lishe bora na hivyo hawawezi kujenga ipasavyo ubongo wao, kinga ya mwili na maungo yao.
Vijana hawana ajira. Maisha yao ni ya kubangaiza. Hatujaweza kutumia vizuri rasilimali na maliasili ya nchi kujenga uchumi unaoongeza ajira na kuleta neema kwa wananchi wote.
Serikali ina wajibu mkubwa wa kujenga mazingira ya kuleta maendeleo ya uchumi shirikishi yatakayoboresha maisha ya Watanzania wote.
Tumo katika mikikimikiki ya uchaguzi. Vyama vya siasa vimeandaa Ilani ya Uchaguzi. Lengo la ilani za uchaguzi ni kuwavutia wapiga kura. Mara nyingi hazizingatii hali halisi iliyopo na vikwazo vya rasilimali fedha na rasilimali watu vitakavyomkabili kiongozi atakayechaguliwa. Baada ya uchaguzi wa 1995, Rais Mkapa alitamka wazi kuwa Ilani ya Uchaguzi ya CCM haitekelezeki.
Ni muhimu kwa mgombea urais mwenye lengo la kuongoza na kusimamia serikali itakayoleta maendeleo kwa wote, kuelewa hali ya uchumi ilivyo hivi sasa na vikwazo atakavyovikabili katika utekelezaji wa malengo makuu ya Serikali. Kuelewa na kuzingatia majukumu makuu ya kifedha ya Serikali ni jambo la msingi kwa Rais mwenye lengo la kuongeza kasi ya maendeleo ya nchi na wananchi wake.
Majukumu makuu ya kifedha ya Serikali ni pamoja na uchambuzi na utabiri wa maendeleo ya uchumi mpana, kubuni na kutekeleza sera za kodi, ukusanyaji wa kodi na ushuru wa forodha, kuchambua na kuandaa bajeti, menejimenti ya uwekezaji wa umma, kusimamia misaada ya nje na menejimenti ya deni la Taifa.
Mengine ni  kusimamia rasilimali za fedha na madeni ya serikali, kuratibu uhusiano wa kifedha baina ya wizara na idara za Serikali, menejimenti ya fedha na malipo ya Serikali, kuweka vizuri hesabu za Serikali, ununuzi wa umma, mishahara ya wafanyakazi, kuratibu mabenki na asasi nyingine za fedha, kusimamia mashirika ya umma, na kuratibu mabadiliko na marekebisho ya usimamizi wa fedha za umma.
Majukumu haya hivi sasa yanasimamiwa na Wizara ya Fedha na Uchumi, idara na mashirika yanayojitegemea, lakini yanaratibiwa au kusimamiwa na wizara.
Idara hizi ni pamoja na Benki Kuu ya Tanzania, Mamlaka ya Mapato na Mamlaka ya Ununuzi wa Umma. Mipango ya Uchumi inaandaliwa na Tume ya Mipango ambayo pia inasimamia uandaaji wa bajeti ya maendeleo kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha.
Mipango yetu ya maendeleo inaandaliwa kama orodha ya miradi inayotafuta wahisani na wawekezaji wa nje kuigharamia na kuitekeleza. Mipango yetu haizingatii uwezo wa  fedha na rasilimali watu wa kuitekeleza.
Bajeti ya maendeleo na bajeti ya kawaida zinastahili kuchambuliwa kwa pamoja. Utekelezaji wa miradi ya maendeleo una athari kwenye bajeti ya kawaida. Kwa mfano, ujenzi wa shule za sekondari utawekwa kwenye bajeti ya maendeleo.
Ili shule hizo zifundishe wanafunzi inabidi kuandaa walimu wa kutosha. Gharama za vyuo vya kufundisha walimu zimo katika bajeti ya kawaida. Kuongeza ujenzi wa shule katika bajeti ya maendeleo kuambatane na kuongeza bajeti ya kuandaa walimu. Gharama za mishahara  ya walimu na vifaa vya kufundishia vitaongezeka katika miaka ijayo.
Kila mwaka Wizara ya Fedha hupaswa kuandaa mpango wa matumizi ya fedha za umma wa miaka mitatu unaojumlisha matumizi yote ya kawaida na ya maendeleo (Medium Term Expenditure Framework). Mpaka hivi sasa mipango hii haiandaliwi kwa umakini unaohitajika. Mpango huu hauna uhusiano wa karibu na mpango wa miaka mitano.
Matatizo ya bajeti yetu
Hivi sasa mfumo wetu wa bajeti una matatizo makubwa. Matatizo hayo ni pamoja na ukosefu wa nidhamu na uwazi katika masuala ya bajeti. Bajeti inayopitishwa na Bunge haifanani na bajeti inayotekelezwa na Serikali. Makadirio ya mapato ni makubwa kuliko mapato halisi. Misamaha holela ya kodi inapunguza mapato ya serikali. Bajeti yetu ni tegemezi.
 Matumizi ya kawaida ni makubwa kuliko mapato ya Serikali. Mapato ya ndani hayachangii miradi ya maendeleo ambayo inategemea misaada na mikopo ya nje na mikopo ya ndani.
Deni la taifa linaongezeka kwa kasi ya juu baada ya kusamehewa madeni mwaka 2000 na 2006. Rushwa na matumizi mabaya ya fedha za umma yanaainishwa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), lakini hakuna hatua zinazochukuliwa dhidi ya wahusika.
Ili mpango wa maendeleo uwe na maana na tija, ni muhimu bajeti ijikite katika kutekeleza mpango wa maendeleo. Mpango wa maendeleo uwe unatekelezeka na usiwe wa kusadikika.
Ili kuratibu utekelezaji wa mipango ya maendeleo na sera za uchumi ni muhimu kuchambua na kuandaa kwa pamoja bajeti ya maendeleo na bajeti ya kawaida na kuwa na bajeti inayotekeleza mpango wa uchumi.
Umuhimu wa wizara moja
 Hivyo basi, ni vyema kuziweka shughuli za kuandaa mipango ya Serikali na bajeti katika wizara moja. Masuala ya ushirikiano wa maendeleo na nchi za nje na hasa masuala ya usimamizi wa misaada ya kiuchumi yawe chini ya wizara hii badala ya wizara ya mambo ya nchi za nje. Lengo kuu la wizara hii litakuwa kuratibu na kutekeleza sera na mipango ya Serikali ya kukuza uchumi na kutokomeza umasikini.
Malengo ya wizara ni pamoja na kuhakikisha kuna utengamavu katika uchumi mpana (macroeconomic stability), mfumuko wa bei wa chini wa  asilimia tano, nakisi ndogo ya bajeti na deni la Taifa la wastani, lisizidi asilimia 60 ya pato la Taifa.
Majukumu mengine ni kuandaa mipango ya maendeleo na mipango wa uwekezaji wa serikali inayotekelezeka. Pia kukusanya mapato ya ndani na ya nje na kuyatumia vizuri katika kutekeleza sera na mipango ya maendeleo.
Baadhi ya wachambuzi hasa wa mrengo wa kushoto hujenga hoja kuwa kuweka masuala ya mipango na fedha katika wizara moja kunadhoofisha uandaaji wa mipango na dira ya maendeleo ya muda mrefu.
Bado wana kumbukumbu ya enzi za Tume ya Mipango katika nchi za Kisoshalisti. Inadaiwa kuwa majukumu ya kila siku ya bajeti ya Wizara ya Fedha yatasababisha mambo ya mipango kutopewa kipaumbele. Hoja hii ni ya msingi. Hata hivyo chimbuko lake ni bajeti ya nchi kutosimamia utekelezaji wa mpango wa maendeleo.
Tume ya Mipango inaweza kuandaa mipango mizuri lakini kama haitekelezwi au haitekelezeki ni upotezaji wa muda na rasilimali. Jambo la msingi ni kubadilisha mtazamo wa Wizara ya fedha na Bajeti. Serikali iwe na nidhamu katika shuguli zake na bajeti iwe ndiyo nyezo muhimu ya kutekeleza mipango ya Serikali.
Botswana na Mauritius  ni nchi za Afrika zinaongoza kwa kufanikiwa kusimamia uchumi wake vizuri kwa muda mrefu, zina wizara moja ya fedha na mipango ya uchumi.
 Nchi haiwezi kukuza uchumi na kuongeza ajira zinazolipa vizuri bila kuwa na serikali yenye mfumo imara wa menejimenti ya fedha za umma. Rais ajaye atafakari kuwa na wizara ya fedha na mipango ya uchumi yenye uwezo wa kuandaa bajeti itakayotekeleza mpango wa maendeleo wa Serikali.
CHANZO:MWANANCHI

About Author

Advertisement

Post a Comment

 
Top