MGOMBEA
ubunge jimbo la Iringa Mjini kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Frederick
Mwakalebela amesema moja ya mambo atakayoyafanya mara tu baada ya kuchaguliwa
kuwa mbunge wa jimbo hilo ni kuhakikisha timu ya Lipuli FC inayoshiriki ligi
daraja la kwanza inapanda daraja.
Akitoa
ahadi hiyo mbele ya maelfu ya wanaCCM na wananchi wa jimbo hilo waliojitokeza
kwenye uzinduzi wa kampeni zake mwishoni mwa wiki iliyopita, Mwakalebela
alisema:
“Najua
watu wa Iringa mna kiu ya kuona Ligi Kuu, niwahakikishieni mwaka huu nitafanya kila
nitakaloweza kuhakikisha Lipuli inapanda daraja.
Mwaka
1999 ikiwa ni sawa na miaka 16 sasa ndio ulikuwa mwaka wa mwisho kwa mkoa wa
Iringa kuwakilishwa na timu hiyo katika Ligi Kuu.
“Tuna
kiu ya miaka 16, tangu Lipuli ishuke daraja jitihada mbalimbali za kuirejesha
katika ligi hiyo zimekuwa hazizai matunda, niwahakikishieni mwaka huu tutafanya
kila tunaloweza kuhakikisha timu hiyo inapanda daraja,” alisema.
Mara
baada ya kushuka daraja mwaka 1999, maendeleo ya Lipuli FC yaliendelea
kuporomoka mwaka hadi mwaka na kujikuta ikishuka hadi daraja la pili mwaka
2012.
Baada
ya kushuka hadi daraja la pili, timu hiyo iliweza kurejea tena hadi ligi daraja
la kwanza baada ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa Jesc Msambatavangu kuinunua
timu ya Polisi Iringa.
Timu
hiyo ya Polisi iliyokuwa ikishiriki daraja la kwanza iliuzwa kwa kada huyo wa
CCM baada ya mwaka 2011 kukumbwa na ukata mkubwa ulioiweka njiapanda ya
kuendelea kushiriki katika mchezo huo ikiwa mikononi mwa jeshi hilo.
Baada
ya kununuliwa mwaka 2012, kada huyo kwa kushirikiana na wadau na viongozi wa
mchezo huo mkoani hapa, waliibadili jina timu hiyo na kuitwa Lipuli FC kwa
lengo la kurejesha hadhi ya timu hiyo.
Jitihada
za timu hiyo kupanda hadi Ligi Kuu baada ya kurudi daraja la kwanza kutokana na
faida hiyo ya kubadili jina, haijazaa matunda hadi sasa.
Post a Comment