Baadhi ya wasomi na wanaharakati wamekemea kauli ya mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli ambaye amekuwa akiwaonya wanaotaka mabadiliko ya haraka nchini akiwakumbusha yaliyojitokeza nchini Libya.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti leo wasomi hao wameiita kauli hiyo ni ya vitisho kwa wananchi, kwa kuwa mabadiliko wanayotaka ni ya kidemokrasia na siyo vita.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Sikika, Irenei Kiria, amesema wananchi wamejiandaa kwa ajili ya kupiga kura na siyo vita kama wachache wanavyofikiri.
“Mabadiliko yanayozungumzwa na wengi ni ya kidemokrasia na siyo vita, hivyo Dk Magufuli hapaswi kutolea mfano wa Libya, tumejiandaa tangu 2010” alisema.
Amesisitiza : “ Ukweli ni kwamba kuna watu wamekuwa wanataja vita hapa nchini tangu mwaka 1995 hao wanatamani kuleta machafuko wamethubutu kufananisha na Rwanda au Burundi, wakati nchi hii ni tofauti kwani CCM imekuwa madarakani kwa 50 na amani ipo,” amesema Kiria.
Mkurugenzi wa Kituo Cha Haki za Binadamu (LHRC), Hellen Kijo-Bisimba amesema wakati wa kampeni si wa kutoa kauli za vitisho bali, wananchi wanachohitaji ni kusikiliza sera za vyama husika ambavyo vitawawezesha kufanya uamuzi wa kuvichagua.
Akiwa mikoa ya Morogoro na Tanga, Dk Magufuli amekuwa akitoa kauli za kuwaonya wanaotaka mabadiliko kuwa wakumbuke yaliyotokea Libya ambapo nchi hiyo imezama kwenye machafuko baada ya kuondolewa aliyekuwa kiongozi wan chi hiyo marehemu Muamar Gadhafi.
Post a Comment