Mwenyekiti Mwenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Dk Emmanuel Makaidi.
Mwili wa Mwenyekiti Mwenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Dk Emmanuel Makaidi unatarajiwa kuletwa Dar es Salaam kwa ajili ya mazishi yanayotarajiwa kufanyika Oktoba 20, mwaka huu.
Dk Makaidi ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Chama cha NLD na mgombea ubunge wa Jimbo la Masasi mkoani Mtwara, alifariki dunia juzi katika Hospitali ya Nyangao mkoani Lindi baada ya kupata shinikizo la damu.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu jana, msemaji wa familia hiyo, Oscar Makaidi ambaye pia ni mtoto wa Makaidi alisema wameamua mwili huo uzikwe Dar es Salaam baada ya kujadiliana.
“Kuna sababu nyingi zilizosababisha tufikie uamuzi huo, ikiwamo kwamba baba mwenyewe enzi za uhai wake alituagiza kuwa akifa tumzike alipozikwa mkewe wa kwanza,” alisema.
Oscar alisema pia mama mzazi wa Dk Makaidi alizikwa Dar es Salaam, suala ambalo litawafanya watoto na wajukuu wanapozuru makaburi wafanye hivyo kwa pamoja.
Alisema kutokana nafasi ya kisiasa aliyokuwa nayo baba yake, wameamua azikwe Dar es Salaam ili kutoa nafasi watu wengi washiriki kwenye maziko hayo tofauti na iwapo watamzika kwao Masasi.
“Jumanne tunatarajia ndiyo tutaupumzisha mwili wake. Tumesogeza siku kutokana na maombi ya viongozi wa kitaifa wa Ukawa ambao walituomba ili wapate nafasi ya kushiriki. Tunashukuru kwa ushirikiano wa wananchi wa huku, akiwamo mbunge wa Masasi anayemaliza muda wake, Mariam Kasembe,” alisema msemaji huyo.
Post a Comment