Serikali Tanzania imeanza kubomoa nyumba zote zilizojengwa kinyume na sheria katika maeneo ya wazi na maeneo ya hifadhiya barabara.
Shughuli hiyo imeanza siku chache tu baada ya wizara ya ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi nchini Tanzania, kusema nyumba hizo zingebomolewa karibuni.
Utekelezaji huo wa agizo la wizara umeleta simanzi na malalamiko kutoka kwa wengi kwa kupoteza makazi yao na hata ajira zao.
Mwandishi wa BBC Esther Namuhisa anasema majengo mengi yaliyokuwa maeneo ya barabarani yalikuwa yakiendesha biashara mbalimbali.
Ubomoaji huo umekuja wakati ambapo wahusika wa nyumba hizo wanadai kuwa hawakuwa na taarifa yoyote, jambo ambalo limewasababishia kutoweza kuokoa mali zao na wengine kukosa malazi.
Baraka Mkuya ambaye ni mhandisi wa manispaa ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam ndiye anayesimamia ubomoaji huo anakanusha madai hayo.
Amesema watu hao walishafukuzwa katika maeneo hayo katika kipindi cha nyuma lakini inashangaza wamerudi tena, kwani hata alama zilizokuwa zimewekwa wengine walifuta.
Zoezi hili ni endelevu na baada ya Dar es Salaam, mikoa mingine itafuata.
BBC SWAHILI
Post a Comment