Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Magufuli, ametangaza kufuta sherehe za Uhuru wa nchi hiyo za mwaka huu zinazofanyika disemba tisa badala yake ameagiza siku hiyo itumike kufanya usafi kwa kila mwananchi.
Rais Magufuli alisema ni aibu kwa taifa kuadhimisha miaka 54 ya uhuru mwaka huu huku taifa likikabiliwa na ugonjwa wa kipindupindu ambao kwa kiasi kikubwa unasababishwa na uchafu, na ameagiza watendaji wote wa halmashauri na manispaa nchini kuhakikisha wanatayarisha vifaa vya kufanyia usafi ili kila mwananchi aweze kushiriki.
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam alisema fedha ambazo zingetumika kwenye maadhimsho ya sherehe za Uhuru mwaka huu zitaelekezwa kwenye maeneo ambayo rais ataona yanahitaji kupatiwa mahitaji sana.
Kuhusiana na safari za nje kwa watumishi wa umma, Balozi Sefue pia amesema rais amegiza kufanyika tathmni ya kina kwa kila anayeomba kusafiri nje ya nchi kabla hajafikiria kuomba kibali kwa katibu mkuu kiongozi.
Tangu kuingia madarakani katika awamu ya tano ya uongozi wake Rais Magufuli ametangaza kukata baadhi ya mambo ikiwemo kuzuia safari za nje zisizo za lazima pamoja hafla au tafrija mbalimbali alizosema zinapoteza fedha nyingi za walipa kodi ambazo zingetumika kutatua kero mbalimbali za wananchi
Wakati huo huo Balozi Ombeni Sefue amewataka watumishi wote wa Umma nchini kuanza kuvaa Beji au vitambulisho maalum vyenye majina yao mahala pa kazi ili kutoa fursa kwa wananchi kujua anahudumiwa na nani
Chanzo:VOA
Post a Comment