Wakati
Serikali ikibanwa na wabunge kwa kushindwa kutekeleza Bajeti ya mwaka
2013/14 kutokana na kutegemea fedha za wahisani, Kamati ya Bunge ya
Uchumi, Viwanda na Biashara imesema deni la taifa limeongezeka kwa Sh8.2
trilioni kwa kipindi cha miezi saba tu.
Ilisema jana
kuwa hadi Juni, mwaka jana deni hilo lilikuwa Sh21.2 trilioni lakini
hadi Januari mwaka huu, deni hilo lilipaa hadi Sh29.4 trilioni na fedha
hizo zimekopwa kwa ajili ya kuendeshea warsha, semina, safari, mafunzo
na matengenezo ya magari.
Akiwasilisha
taarifa ya kambi ya Upinzani, Waziri Kivuli wa Fedha, James Mbatia
alisema ukiligawanya deni hilo kwa idadi ya Watanzania milioni 45, kila
mwananchi atakuwa anadaiwa Sh600,000.
Kati ya Sh5.8trilioni za bajeti ya Wizara ya Fedha mwaka 2014/15, Sh4.3trilioni zimetengwa kwa ajili ya kulipa Deni la Taifa
Akiwasilisha
taarifa ya Kamati, Mwenyekiti wake, Luhaga Mpina alisema
Sh24.18trilioni ni deni la Serikali, Sh3.75trilioni ni deni la sekta
binafsi na Sh1.15trilioni ni deni la Benki Kuu Tanzania (BoT).
“Ongezeko
hili la deni haliendi sambamba na kasi ya utekelezaji wa miradi ya
maendeleo na ujenzi wa miundombinu ya uchumi. Hali hii inajenga hofu
kuwa huenda deni hili limekuwa ni uchochoro wa ubadhilifu wa fedha za
umma,” alisema Mpina.
Alisema
licha ya Serikali mara kadhaa kueleza kuwa deni hilo ni himilivu, kuna
viashiria vinavyoonyesha kuelemewa kwa taifa na mzigo mkubwa wa madeni.
“Mfano ni
mapato ya ndani yamezidiwa na matumizi ya kawaida hivyo kuifanya
Serikali kukopa hata kwa ajili ya warsha, semina, safari, mafunzo na
matengenezo ya magari,” alisema Mpina.
“Deni la
Taifa sasa limefikia asilimia 47 ya Pato la Taifa na kwa kipimo cha bei
ya sasa deni la taifa limefikia asilimia 24, huku deni la nje pekee
likiwa ni asilimia 19” alisema Mpina na kuongeza:
“Licha ya
Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) kuahidi kwa muda mrefu
kufanya ukaguzi maalumu wa deni la taifa, hadi sasa taarifa yake
haijawasilishwa. Ni lini taarifa hiyo itawasilishwa bungeni ili
kuwawezesha wananchi kufahamu undani wa jambo hili?” alihoji.
Kamati hiyo
pia iliilipua Serikali kwa kuuza mashine za elekroniki (EFD), kati ya
Sh600,000 hadi 700,000 kwa maelezo kuwa kiwango hicho ni kikubwa kwa
mzunguko wa biashara ya mtaji wa Sh14 milioni kwa sababu mtaji wake
hauzidi Sh5milioni.
Mpina
alisema mashine hizo zinatakiwa kugawiwa bure kwa wafanyabiashara wenye
kipato chini ya Sh40milioni na kufafanua kuwa chombo hicho chenye
taarifa muhimu za mapato ya Serikali hakitakiwi kuuzwa na kufanyiwa
matengenezo na mtu binafsi.
Mpina
alibainisha kuwa utafiti uliofanywa na Mtandao wa Kimataifa wa Global
Financial Integrity (GFI), umebaini kuwa Tanzania inapoteza Sh3trilioni
kila mwaka kutokana na mzunguko wa fedha haramu.
“Kamati
inataka taarifa ya mabilioni ya fedha zilizofichwa katika Benki za
Uswisi iwasilishwe mapema kabla Bunge halijaisha ili kuwawezesha wabunge
na wananchi kujua ukweli wa jambo hili,” alisema.
Chanzo: Mwananchi.
Post a Comment