Lindi. Baadhi ya wanaume mkoani hapa
wanadaiwa kuwanyanyapaa wake zao kwa
kuwapa talaka pindi wanapogundulika wana
na maambukizi ya virusi Ukimwi.
Wataalamu wa afya kutoka Zahanati ya
Mitwero walisema hayo jana walipokutana na
timu ya Shirika la Elizabeth Glaser Pediatric
Aids Foundation (EGPAF).
Muuguzi Grace John na Mganga Mfawidhi wa
zahanati hiyo, Ally Daudi walisema baadhi ya
wanaume hukataa kupima afya zao pale
wanapoombwa na wake zao ili waweze
kufahamu kama wapo salama au la.
Dk Daudi alisema kutokana na hali hiyo
wanawake huchukua uamuzi wa kupima VVU
na kama wakigundulika wameathirika,
hunyamaza kwa kuhofia kupewa taraka.
“Hivi ninapozungumza na ninyi leo hii kuna
mama mmoja alimweleza mumewe wakapime
ili kutambua afya zao, mume alimkatalia,
lakini mwanamke huyu alipokuja na
kubainika ana VVU, tulimuanzishia dawa.
“Lakini akasema atalazimika kuzificha chini
ya ndoo ya maji ili asiachwe na mumewe,”
alisema Dk Daudi.
Muuguzi John alisema alishawahi
kusuluhisha ugomvi wa wanandoa wawili,
waliofika kupima afya zao na mwanamke
aliyegundulika kuwa na VVU huku
mwanamume akiwa hana.
“Baada ya wanandoa hao kufika hapa kupima
afya zao, mwanamke alikutwa na
maambukizi, lakini mwanamume
hakuwanavyo, kulitokea vuta nikuvute,
mwanamume alikwenda dukani kununua
karatasi na peni kutaka kumwandikia mkewe
talaka mbele yangu,” alisema.
Alisema kutokana na jitihada za kusuluhisha
ugomvi huo, wanandoa hao walifanikiwa
kupatana na kuweza kurejea nyumbani kwao.
LIKE page yetu MJUMBE BLOG facebook au Tutembelee Mtandaoni andika MJUMBE BLOG kisha ingiq hapo upate picha,Matangazo,Taarifa muhimu,Habari mpya kila mara.
Post a Comment