
MAJINA ya baadhi ya watu walionufaika na fedha
Cza akaunti ya Escrow zilizowekwa katika akaunti
ya Benki ya Stanbic jijini Dar es Salaam
yameanza kutajwa, Raia Mwema linafahamu.
Miongoni mwa majina ambayo vyanzo vya gazeti
hili vimethibitisha kwamba yapo ni lile la mke wa
mmoja wa vigogo wa ngazi za juu Ikulu (jina
tunalihifadhi kwa sasa) ambaye anaelezwa
kuchukua kiasi cha dola za Marekani milioni tatu
(Sh. bilioni tano).
“Tayari tunalo jina la mwanamke mmoja ambaye
amefahamika kama mke wa mmoja wa watu
wenye vyeo vikubwa Ikulu. Kwa sababu bado
mapema kukupa jina kamili, vumilia kidogo hadi
kila kitu kitakapokamilika,” kilisema chanzo cha
kuaminika cha gazeti hili kinachoshiriki kwenye
uchunguzi wa suala la namna fedha za akaunti
ya Escrow zilivyolipwa kwa watu.
Raia Mwema linahifadhi jina la mwanamama huyo
pamoja na mumewe kwa sasa kwa vile kuwataja
majina kunaweza kuingilia upelelezi.
Wakati majina ya baadhi ya mawaziri, wanasiasa,
majaji na viongozi wa dini yakionekana kulipwa
fedha za mgao kutoka katika akaunti moja ya
Benki ya Mkombozi, kumekuwa na kitendawili
kuhusu ni akina nani hasa walilipwa fedha
zilizokuwapo katika Benki ya Stanbic.
Wafaidikaji wengine wa akaunti hiyo ambao
gazeti hili limefanikiwa kuwapata kwa sasa ni
mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Rajiv Bharat
Bhesania, anayetajwa kuwa mojawapo wa
wasaidizi muhimu wa mmiliki wa kampuni ya Pan
African Power (PAP), Harbinder Seth Singh.
Katika mojawapo ya miamala katika akaunti ya
Stanbic iliyofunguliwa na PAP ambayo inaonekana
katika ripoti ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za
Serikali (PAC), Bhesania anaonekana kuchukua
kiasi cha dola milioni moja (shilingi bilioni 1.6).
Mtu mwingine ambaye inaonyesha amefaidi fedha
za akaunti ya PAP ni Mwanasheria wa PAP,
Joseph Makandege, ambaye kampuni yake ya
sheria ya Bulwark Associates imeonekana kupata
malipo yakiwamo ya zaidi ya shilingi milioni 500
kwa nyakati tofauti.
Gazeti hili limefanya mawasiliano na mmoja wa
wafanyakazi wa zamani wa IPTL aliyedai kwamba
Rajiv pengine ndiye mtu anayefahamu vizuri zaidi
mienendo na biashara nyingi zaidi za Sethi na
kama Serikali inataka taarifa za mfanyabiashara
huyo mtata; basi inapo pa kuanzia.
Ingawa PAC ilipendekeza Sethi akamatwe na
kuhojiwa kutokana na tuhuma mbalimbali kama
vile utakatishaji wa fedha, kukwepa kulipa kodi na
udanganyifu, Raia Mwema limeambiwa kuwa
mmiliki huyo wa PAP hayupo nchini kwa sasa.
“Kama Serikali inataka kupata chochote kutoka
kwa Sethi inabidi wambane huyuhuyu Rajiv
Bhesania. Yeye ndiye kila kitu kwa Sethi hapa
Tanzania. Hata akitaka mambo yake yanyooke
mahali huwa anamtumia huyu.
“Nafahamu si rahisi kusema kila kitu lakini
nafahamu kwamba kama vyombo vya ulinzi
vitambana kisawasawa, anaweza kutoa siri zote
za Sethi na hatimaye Watanzania wakapata
wanachokitaka,” alisema mfanyakazi huyo wa
IPTL.
Malipo hayo yote yalifanyika katika kupitia katika
akaunti namba 912 0000 12 52 94 ambayo
ilifunguliwa tarehe 28 Novemba mwaka 2013 na
kufungwa tarehe 14 Septemba 2014.
Ni katika benki hii ndiko ambako muamala wenye
thamani ya shilingi bilioni 73.5 ulifanyika siku ya
Januari 23 mwaka huu; muamala ambao sasa
ndio unachunguzwa na vyombo vya ulinzi.
Ni katika siku hii ambapo ripoti za Ofisi ya
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
(CAG) pamoja na ile ya Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (Takukuru), zilieleza
kwamba kuna watu waliondoka katika ofisi za
benki hiyo wakiwa na magunia yaliyojaa fedha.
“Kwa mujibu wa Takukuru baadhi ya watu
walienda kugawana fedha kwenye Benki tajwa
(Stanbic) wakiwa na mifuko ya rambo, sandarusi,
maboksi, magunia na lumbesa,” ilisema sehemu
ya ripoti iliyowasilishwa bungeni na PAC.
Muamala huo unachunguzwa vikali na Takukuru
pamoja na ule wa Februari, 2014 katika Benki ya
Mkombozi jijini Dar es Salaam ambapo kiasi cha
shilingi bilioni 3.3 zinadaiwa pia kuchukuliwa kwa
siku moja.
Habari za mke wa mmoja wa maofisa wa ngazi
za juu wa Ikulu kuhusishwa na uchotaji wa fedha
za Escrow inakuja katika kipindi ambacho
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, akidai
bungeni kwamba ofisi hiyo ya juu nchini ina
mkono katika utolewaji wa fedha hizo kutoka
Benki Kuu ya Tanzania.
Wakati akizungumza bungeni, Mbowe ambaye pia
ni Mbunge wa Jimbo la Hai na Kiongozi wa
Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni, alimtaja
Prosper Mbena ambaye ni Katibu wa Ofisi ya Rais
(Ikulu), kuwa ndiye aliyeandika barua ya kuruhusu
fedha zilizokuwa zimehifadhiwa zitolewe katika
akaunti hiyo.
Habari hizi za Stanbic kuhusishwa na fedha za
Escrow zimesababisha benki hiyo kumpa
uhamisho aliyekuwa Meneja wake, Paul Omara,
ambaye sasa anadaiwa kurejeshwa nchini
Uganda.
Omara anaelezwa kuitumikia benki hiyo kwa
muda wa miaka zaidi ya 11 na Raia Mwema
limeelezwa kwamba ofisa huyo tayari amehojiwa
na Takukuru kuhusu suala hilo kabla hajaondoka.
Mmoja wa maofisa wa Takukuru aliyezungumza
na gazeti hili kwa masharti ya kutotajwa jina kwa
maelezo kwamba uchunguzi unaendelea, alisema
wamepata ushirikiano mzuri kutoka Stanbic na
kuna uwezekano kwamba “ watu watakula
Krismasi wakati tayari Takukuru ikiwa imemaliza
kazi”.
Suala la fedha za Escrow lililiteka Taifa wiki
iliyopita na sasa wananchi wanasubiri kwa hamu
hatua itakayochukuliwa na serikali kuhusu vigogo
wanaotajwa kusaidia kutokea kwa kashfa hii.
Chanzo:Raia mwema
Post a Comment
Click to see the code!
To insert emoticon you must added at least one space before the code.