moja wa watuhumiwa wa kashfa ya uchotaji
fedha katika akaunti ya Tegeta Escrow ambao
ni watumishi waandamizi wa umma, Theofillo
Bwakea akiwa chini ya ulinzi wa Polisi
akipanda ngazi kuingia katika Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam
walipofikishwa kusomewa mashtaka yao jana.
(Picha na Fadhili Akida).
WATUMISHI wawili waandamizi wa Serikali
wamepandishwa kizimbani katika Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam
wakikabiliwa na mashitaka ya kupokea zaidi
ya Sh milioni 485 ambazo ni sehemu ya fedha
zilizokuwa kwenye akaunti ya Tegeta Escrow.
Washitakiwa hao ni Mkurugenzi wa Masuala
ya Kisheria wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, Rugonzibwa
Mujunangoma na Mhandisi Mkuu wa Wakala
wa Nishati Vijijini (REA), Theophil Bwakea.
Washitakiwa hao walifikishwa mahakamani
hapo jana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana
na Rushwa (Takukuru) na kusomewa
mashitaka mbele ya mahakimu wawili
tofauti.
Awali, Bwakea alifikishwa mbele ya Hakimu
Mkazi, Frank Moshi akidaiwa kupokea
rushwa ya Sh milioni 161,700,000 kutoka kwa
mmiliki wa kampuni ya kufua umeme ya VIP
Engineering and Marketing ambaye pia
alikuwa Mkurugenzi wa kampuni ya IPTL,
James Rugemalira.
Wakili kutoka Takukuru, Leonard Swai alidai,
Februari 12, 2014 katika jengo la Benki ya
Mkombozi Ilala, alijipatia fedha hizo kupitia
akaunti namba 00410102643901 akiwa kama
mjumbe aliyeandaa sera kuruhusu sekta
binafsi kuzalisha na kuliuzia umeme Shirika
la Umeme (Tanesco).
Mujunangoma alifikishwa mbele ya Hakimu
Mkazi Emilius Mchauru na kusomewa
mashitaka ya kupokea Sh milioni 323,400,000
baada ya kushughulikia masuala ya kampuni
ya IPTL kama mfilisi jambo ambalo
linahusiana na kazi yake.
Wakili Swai alidai Februari 5, 2014 katika
jengo la Benki ya Mkombozi alipokea rushwa
ya fedha hizo kupitia akaunti namba
00120102602001 kutoka kwa Rugemalira.
Inadaiwa fedha hizo ni sehemu ya zilizokuwa
kwenye akaunti ya Tegeta Escrow.
Washitakiwa walikana mashitaka na upande
wa Jamhuri ulidai upelelezi wa kesi hizo
umekamilika na kuomba terehe nyingine kwa
ajili ya washitakiwa kusomewa maelezo ya
awali.
Washitakiwa wote wameachiwa kwa dhamana
baada ya kutimiza masharti yaliyotolewa,
ambapo Bwakea alitakiwa kuwa na
wadhamini wawili wanaofanya kazi serikalini
waliotoa Sh milioni 25 kila mmoja. Aidha,
Mahakama imeamuru fedha zilizo katika
akaunti ya Bwakea zisitumike hadi kesi hiyo
itakapokwisha.
Mujunangoma aliwasilisha hati ya mali
isiyohamishika yenye thamani ya nusu ya
fedha anazodaiwa kupokea, alikuwa na
wadhamini wawili watumishi wa umma
waliosaini hati ya Sh milioni 10 kila mmoja,
aidha upande wa Jamhuri umetakiwa
kuwasilisha ombi la kuzuia matumizi ya
akaunti yenye fedha anazodaiwa kupokea.
Kesi zitatajwa Januari 29 mwaka huu kwa
ajili ya kuwasomea washitakiwa maelezo ya
awali. Mujunangoma atafika mahakamani
kesho kwa ajili ya kuwasilisha tathmini ya
hati alizotoa mahakamani kama dhamana
pamoja na baadhi ya nyaraka za wadhamini
wake.
WanaCCM kikaangoni Katika hatua nyingine,
sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow
limechukua sura mpya ndani ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM), baada ya Kamati Kuu ya
chama hicho kuagiza hatua za kimaadili
zichukuliwe dhidi ya wote waliohusika na
ukiukwaji wa maadili katika sakata hilo.
Wanaobanwa zaidi ni wale ambao ni sehemu
ya vikao vya maamuzi katika chama hicho
tawala. Hayo yalisemwa jana na Katibu wa
Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape
Nnauye alipozungumza na waandishi wa
habari mjini humo kuzungumzia
yaliyojadiliwa katika kikao cha Kamati Kuu ya
CCM kilichokutana juzi.
Alisema Kikao cha Kamati Ndogo ya Maadili
kitafanyika Januari 19, kwa ajili ya utekelezaji
wa agizo hilo.
Aliongeza kuwa, CCM imesikitishwa sana na
sakata hilo linalohusishwa na uchotaji fedha
zaidi ya Sh milioni 306 katika akaunti ya
Tegeta Escrow katika Benki Kuu ya Tanzania
(BoT) iliyofunguliwa baada ya kuibuka kwa
mgogoro wa kibiashara baina ya kampuni ya
kufua umeme ya IPTL na Shirika la Umeme
Nchini (TANESCO).
“Baada ya kulijadili kwa muda mrefu na kwa
kina Kamati Kuu imeamua pamoja na yale
ambayo yameshatekelezwa na serikali, Kamati
Kuu imeitaka serikali na vyombo
vinavyohusika kuendelea kutekeleza
maazimio ya bunge juu ya swala hilo.
“Aidha, Kamati Kuu imewataka wote
wanaopewa dhamana wajenge utamaduni wa
kuwajibika kwa dhamana zao, na
wasipowajibika waliowapa dhamana
wachukue hatua za kuwawajibisha. “Na Tatu,
Kamati Kuu imeiagiza Kamati Ndogo ya
Maadili kuchukua hatua za kimaadili kwa
wale wote waliohusika na ukiukwaji wa
maadili kwenye sakata la Escrow na wako
kwenye vikao vya maamuzi vya Chama.”
Sakata la Escrow, baada ya kuibua mjadala
mzito bungeni, wabunge walitoka na
maazimio kadhaa yaliyowasilishwa kwa Rais
Jakaya Kikwete, ikiwa ni pamoja na kutaka
kuwajibishwa kwa wahusika wa sakata hilo,
wakiwemo mawaziri na watendaji wengine
serikalini.
Tayari Rais Kikwete ameshachukua hatua
kadhaa, ikiwa ni pamoja na kutengua uteuzi
wa aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna
Tibaijuka.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Eliakim
Maswi amesimamishwa kwa muda
usiojulikana ili kupisha uchunguzi wakati Jaji
Frederick Werema amejiuzulu wadhifa wake
wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, akisemaa
anawajibika, ingawa amekuwa akisisitiza
haoni kama alifanya kosa lolote katika
kushauri juu ya suala la akaunti ya
Escrow.
Shukrani:HABARI LEO
posted from Bloggeroid
Post a Comment