UPELELEZI wa kesi ya ugaidi inayomkabili kiongozi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (Jumiki), Shekhe Farid Hadi Ahmed na wenzake bado haujakamilika.
Wakili Mkuu wa Serikali Benard Kongola alidai hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakati kesi hiyo ilipotajwa mbele ya Hakimu Mkazi Janeth Kaluyenda.
Wakili Kongola alidai kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kutajwa, hata hivyo Wakili wa washitakiwa hao Abubakar Salim aliomba Hakimu atoe uamuzi kutokana na maelekezo yaliyotoka Mahakama Kuu.
Alidai baada ya jalada kutoka Mahakama Kuu lilielekeza hoja walizowasilisha zitolewe uamuzi na kama kuna hoja nyingine ziwasilishwe.
Hakimu Kaluyenda alisema jalada hilo limefika kwake kwa mara ya kwanza hivyo aliomba muda akalipitie pamoja na uamuzi wa Mahakama Kuu. Kesi itatajwa tena Januari 22, mwaka huu.
Katika kesi hiyo, washitakiwa wanadaiwa katika tarehe tofauti nchini kati ya Januari, 2013 na Juni, 2014 walipanga njama za kutenda kosa la kuwaingiza watu nchini kwa ajili ya kufanya vitendo vya ugaidi.
Post a Comment