Ndugu zangu,
Ama hakika, Watanzania wa Vijijini watamkumbuka Rais Jakaya Kikwete kama ' Rais wa Umeme'.
Jana nilifika kijijini kwetu Nyeregete, Mbarali, Mbeya. Nimewakuta watu wenye furaha hata kabla umeme haujawaka kwenye nyumba zao.
Nguzo za umeme kutoka Rujewa zimeshafika Nyeregete. Wanakijiji wana hamu wanaisubiri kwa hamu kubwa siku ile umeme utakawaka rasmi.
Kwao ina maana kubwa kuliko labda wengine tunavyofikiri. Umeme ni mkombozi wa kiuchumi. Wameshalijua hilo. Umeme utawaongezea maarifa mapya, hata kwa kuangalia televisheni tu.
Kuna mwanakijiji aliyeniambia: " Yaani, mie hata kama kulala na njaa, nitalala na njaa ili nipate fedha za kuingiza umeme! Nimechoka na vibatari na vitochi vya Mchina vye kuharibika mara kwa mara"
Na mwanakijiji mwingine anasema: " Hata kama kulipa laki mbili kuingiza umeme niko tayari!"
Na mwingine ananiambia: " .. Na Jumapili kwenye ibada , na yule ... anatwambia eti umeme wa nini wakati hamna maji ya bomba! Eti, anatwambia sisi hayo wakati yeye kwake ana umeme na huja hapa kanisani kututambia, kuwa mara ameona hiki na mara kile kwenye tv yake nyumbani!"
Na ninanachokiona mimi, na tafadhali usininukuu: Ni kuwa umeme huu wa vijijini utaisaidia CCM kubaki madarakani ifikapo Oktoba mwaka huu, lakini, wasipoweka mambo yao sawa na hususan kwenye usimamizi wa miradi ya maendeleo kwa wananchi, na hata kuwa na watendaji wasio waadilifu na zaidi mafisadi, basi, umeme huu wa vijijini, ndio utakaopelekea kwa kasi ya ajabu, kuiondoa CCM madarakani ifikapo 2020. Maana, umma wa vijijini, kupitia kwenye radio na runinga zao, nao utakuwa umemulikiwa maovu ya CCM kwa mwanga wa ' Umeme Vijijini'.
___________________________________________________________________________________________________________________________________________________________
Credit:Maggid,
Post a Comment