Afisa Madini Mkazi, Mkoa wa Kilimanjaro, Fatuma Kyando akielezea sheria na kanuni za uchimbaji wa madini nchini katika mafunzo yaliyoshirikisha wachimbaji wa madini Mirerani kuanzia tarehe 25 hadi 26 Julai, 2015. Lengo la mafunzo hayo lilikuwa ni kuwapa uelewa juu ya huduma za leseni kwa njia ya mtandao.
……………………………………………………………………
Na Greyson Mwase;Arusha.
Imeelezwa kuwa ili kuondokana na migongano kwenye usimamizi wa sekta ya madini Kanda ya Kaskazini, Wizara ya Nishati na Madini imeandaa mafunzo kuhusu sekta ya madini yatakayoshirikisha viongozi mbalimbali katika mikoa ya Manyara, Arusha na Kilimanjaro yanayotarajiwa kufanyika Agosti 12, mwaka huu.
Akizungumza katika mahojiano maalum jijini Arusha jana, Afisa Madini Mkazi, Mkoa wa Kilimanjaro, Fatuma Kyando alisema kuwa mafunzo hayo yatashirikisha wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri, maafisa tawala wa wilaya, watendaji na wenyeviti wa vijiji na kata na wawakilishi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
Alieleza kuwa katika usimamizi wa sekta ya madini katika kanda hiyo, kumekuwepo na mgongano wa mamlaka ambapo kila upande umekuwa ukiona una nguvu kuliko mwingine kwenye utoaji na usimamizi wa leseni za madini.
Alisema ni vyema kila mamlaka ikafahamu majukumu na mipaka yake katika usimamizi wa shughuli za madini ili kuzuia migogoro inayoweza kujitokeza.
Alisisitiza kuwa kati ya mambo watakayojifunza ni pamoja na sheria na kanuni za madini, utunzaji wa mazingira katika shughuli za madini na fursa za madini yaliyopo.
Akielezea changamoto nyingine katika usimamizi wa shughuli za utafutaji na uchimbaji wa madini katika kanda hiyo, Kyando alisema kumekuwepo na migongano kwenye tozo la kodi kwenye mapato yatokanayo na madini.
Alisema mapato wanayokusanya wamekuwa wakiwasilisha serikali huu ambapo fedha hizo hurudishwa tena kwenye halmashauri kwa ajili ya kuimarisha huduma za jamii lakini bado watu wamekuwa wakihoji kwanini fedha hizo zisilipwe moja kwa moja tu kwenye halmashauri na kutumika kwa maendeleo moja kwa moja.
Aliongeza kuwa hali hii inatokana na wananchi na viongozi kutokuwa na uelewa wa sheria na kanuni za madini na ndio maana ofisi yake imeandaa mafunzo hayo.
Alisema kuwa mafunzo hayo yatawawezesha mamlaka zote kuwa na lugha moja na kufanya kazi kwa pamoja na kuzuia migogoro inayoweza kujitokeza.
Post a Comment