Diwani wa Kata ya Mabawa katika Halmashauri ya Jiji la Tanga, Muzzamillu Shamdoe amewataka wajasiriamali wanawake kulitumia soko la pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kutangaza bidhaa zao.
Akizungumza baada ya kufungua Kituo cha ushonaji nguo cha Raha Gani kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu jana, Shemdoe alisema wajasiriamali hawalitumii soko hilo ndiyo maana kazi zao hazijulikani.
Alisema wajasiriamli kutoka nchi wanachama wamekuwa wakilitumia kikamilifu soko hilo na bidhaa zao kutangazika.
Shamdoe aliwakumbusha wajasiriamali nchini, kulifikia soko hilo ili kufikia malengo waliyojiwekea.
“Wajasiriamali wa hapa kwetu hawana uelewa wa soko la pamoja, angalia wenzetu bidhaa zao zilivyoenea nchini kila kona ni bidhaa za nje,” alisema Shemdoe na kuongeza:
“Nawashauri pelekeni kazi zenu kwa wenzenu huenda ni bora zaidi, msing’ang’anie hapa tu, hamtaweza kufikia malengo yenu.”
Wakati huohuo; Mkuu wa Kituo cha Raha Gani, Hafifa Kijazi alisema kituo hicho kina watoto yatima 18 wanaoishi katika mazingira magumu kutokana na kukabiliwa na upungufu wa vitendea kazi.
Alisema kituo hicho kina cherehani saba jambo ambalo amedai ni gumu kuwafundisha watoto wote kwa wakati mmoja, hivyo kuchukua muda mrefu kumfikia kila mmoja.
Kijazi aliyataka mashirika na taasisi za watu binafsi kukisaidia kituo hicho ili kuwapa elimu watoto hao.
Alisema endapo watapatiwa msaada wa vitendea kazi watoto hao wakipata elimu wataweza kujitegemea pamoja na kujiepusha na vishawishi vya mitaani.
Alisema watoto hao ambao wote ni wa kike wakiachwa wanaweza kujitumbukiza katika vitendo viovu, hivyo ni wajibu kwa jamii kukiangalia ili kufikia malengo.
Post a Comment