Aliyekuwa kiongozi Mkuu wa Taliban, Mullah Omar anayedaiwa kufariki dunia.
SERIKALI ya Afghanistan leo ilikuwa inachunguza kuvuja kwa habari miongoni mwa maofisa wake kwamba kiongozi wa Taliban, Mullah Omar, amefariki.
Uchunguzi huo umekuja baada ya maofisa wa serikali kudai kwamba mpiganaji huyo aliyekuwa na jicho moja alifariki miaka miwili iliyopita kutokana na ugonjwa. Hata hivyo, msemaji wa Taliban, Zabihullah Mujahidin, alikanusha madai hayo akisema Omar bado yu hai.
Kiongozi huyo ambaye ni vigumu kuonekana hadharani na ambaye ni mshirika wa Al Qaeda, aliendesha vita vikali dhidi ya majeshi ya Marekani ambayo yaliuangusha utawala wake nchini Afghanistan mnamo 2001.
Mmoja wa maofisa wa Afghanistan alisema: “Tunaweza kuthibitisha kwamba Mullah Omar alifariki miaka miwili iliyopita… nchini Afghanistan kutokana na ugonjwa. Alizikwa katika jimbo la Zabul (kusini mwa Afghanistan)” Zafar Hashemi, naibu msemaji wa Rais wa Afghanistan, Ashraf Ghani, alisema serikali ilikuwa inachunguza ripoti hizo.
“Tuna habari za kufariki kwa Mullah Omar, kiongozi wa Taliban,” alisema Hashemi na kuongeza: “Bado tunafuatilia ripoti hizi, na mara tukipata uthibitisho, tutawajulisha watu wa Afghanistan.”CREDIT: DAILY MAIL
Post a Comment