NA BASHIR YAKUB -
Sheria ya Uwekezaji ya Mwaka 1977 imehamasisha uwekezaji kwa wazawa na wasio wazawa kwa kuweka mazingira rafiki kwa wajasiriamali katika nyanja zote. Wapo ambao wanajua fursa hizi na wamezitumia kujipatia maendeleo na wapo ambao hawajatumia fursa hizi. Nataka niseme kitu kimoja kuwa wazawa wengi wameshindwa kufanikiwa kwa kutojua uwepo wa fursa. Wengi wangependa kutumia fursa kama zipo lakini hawajui ziko wapi na zinapatikana vipi.
Badala yake wageni na watu wengine ambao si wenye asili halisi ya Tanzania ndio wamekuwa wakihabarishana kuhusu fursa hizi wanazitumia na wanafanikiwa sana. Wenyeji halisi wa nchi hii wanabaki kutazama mafanikio ya watu hawa wasijue yanapatikanaje. Ziko fursa ambazo zimetolewa na serikali na kuainishwa na sheria mbalimbali mojawapo ikiwa hii ya kusamehewa kodi kwa bidhaa zinazoingizwa nchini kutoka nje ya nchi. Wafanyabiashara watakubaliana na mimi kuwa ikiwa utapata msamaha mzuri wa kodi bandarini basi unayo nafasi kubwa ya kutengeneza faida kubwa katika biashara yoyote utakayoamua kufanya.
Mara zote kodi ndio huwa tatizo. Makala haya yataeleza namna ya kupata msamaha wa kodi.
1.KUHUSU MSAMAHA WA KODI NA USHURU.
Sheria ya uwekezaji ya 1997, sehemu ya ( iii ), kifungu cha 17 ( 1 – 8) kimeeleza kuhusu kujisajili katika kituo cha uwekezaji Tanzania na kupata cheti kiitwacho Certificate of Incentives. Kinachotakiwa ni mjasiriamali kujisajili katika kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na kupata cheti hiki ambapo kupitia cheti hiki mjasiriamali atakuwa akipata msamaha wa kodi wakati anapoingiza bidhaa kutoka nje ya nchi kwa miaka tatu.
Hapa kwetu, wageni na wafanyabiashara wenye asili ya Asia wanatumia fursa hii kwa ufasaha na sitaki kueleza mafanikio yao kwani kila mtu anayajua. Katika kuonesha dhamira ya dhati katika kuwapunguzia watu kodi kituo cha uwekezaji (TIC ) kimeanzisha kitengo kiitwacho TIC-TRA ambacho ndicho hushughulikia masuala yote yanayohusu namna ya kupunguziwa kodi .
2. NAMNA YA KUJISAJILI TIC.
Tumesema hapo juu kuwa ili uweze kufaidika na msamaha huu ni lazima uwe umejisajili katika kituo cha uwekezaji Tanzania (TIC). Hii ni namna ya kujisajili TIC.
( a ) Kwanza lazima uwe na cheti cha kuzaliwa kwa kampuni( Certificate of Incorporation). Hii ina maana kuwa ni lazima uwe na kampuni kwakuwa huwezi kuwa na cheti hiki bila kuwa na kampuni. Ulazima wa kuwa na cheti hiki ni kuthibitisha kuwa unayo kampuni na imesajiliwa kwa mujibu wa sheria.
( b ) Lazima uwasilishe katiba na waraka wa kampuni ( memorandum & article of association). Kimsingi unapokuwa umesajili kampuni hivi ni vitu ambavyo lazima uwe navyo. Hivyo nakala moja ya vitu hivi ndiyo inayotakiwa TIC.
( c ) Uwasilishe hati ya nyumba kama unamiliki nyumba ambayo ndio umeifanya kama ofisi yako au mkataba wa pango ikiwa nyumba unayofanyia biashara umeipanga.
( d ) Barua kutoka benki . Ukienda benki ukawaambia nimetumwa barua ya TIC wao wanajua ni barua ya aina gani inahitajika.
( e ) Nakala mbili za mpango kazi (feasibility study) . Mpango kazi ni maelezo kwa urefu yanayoeleza aina ya biashara inayofanywa na muombaji, mategemeo yake katika biashara hiyo, wafanyakazi anaotegemea kuajiri, mategemeo ya faida au matumizi na kila kitu kuhusu biashara ya muombaji.
( f ) Maelezo ya maafikiano ya kikao cha bodi ya kampuni ( board resolution) nakala moja. Haya ni maelezo kwa ufupi yanayothibitisha bodi ya kampuni kuridhia kampuni kusajiliwa na kituo cha uwekezaji TIC.
( g ) Barua ya maombi nakala moja. Hii ni barua rasmi inayolenga kuonesha nia ya mhusika ya kutaka kusajiliwa na kituo cha uwekezaji.
( h ) Pia kuna fomu ya maombi ambayo hutolewa na TIC wenyewe. Hii ni tofauti na barua ya maombi . Fomu hii hulipiwa dola 100 kupitia akaunti namba A/C 8702006002000 Standered Chrtered Bank.
3. BAADHI YA BIDHAA AMBAZO UTAPATA PUNGUZO LA KODI.
Punguzo la kodi unaloweza kupata ni kubwa kwa mfano lipo la asilimia 37.5, 25%, 20%,12% mpaka 100% n.k. Baadhi ya bidhaa ni vifaa vya umeme, mabasi yanayobeba kuanzia abiria 30 na kuendelea, vifaa vya ujenzi, malori tela, fenicha, kompyuta, vifaa vya uvuvi na madini, vifaa vya elimu na vitabu, vifaa vya kilimo vifaa, vya mawasiliano kama simu na vile vya utangazaji kama studio , vifaa vya usafirishaji na utalii na vingine vingi ambavyo sikutaja.
Hii ni namna ya pekee ya kufaidi fursa ambayo baadhi ya wafanyabiashara hasa wenye asili ya Asia wamekuwa wakifaidi. Aidha kuhusu nyaraka nilizoeleza hapo juu kuwa zinahitajika katika usajili wapo watu ambao huziandaa zote na hivyo hamna usumbufu wowote katika kukamilisha usajili.
Baada ya kukamilisha nyaraka hizo basi zitawasilishwa Kituo cha Uwekezaji Tanzania ( TIC) kilichpopo mtaa wa Shaaban Robert plot No 9, opposite na Shule ya bunge, Dar es salaam.
MWANDISHI WA MAKALA HAYA NI MWANASHERIA NA MSHAURI WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA SERIKALI LA HABARI LEO KILA JUMANNE , GAZETI JAMHURI KILA JUMANNE NA GAZETI NIPASHE KILA JUMATANO. 0784482959, 0714047241
Post a Comment