Tarehe 1 Agosti, tamasha la Afrifest lilifanyika mjini Brooklyn Park, Minnesota.
Hili ni tamasha ambalo huandaliwa mara moja kwa mwaka na bodi ya Afrifest Foundation ambayo mimi ni mwenyekiti wake. ili kuwakutanisha wa-Afrika, watu wenye asili ya Afrika waishio Marekani ya Kaskazini, Kati, na Kusini, pamoja na Caribbean, na pia watu wa mataifa mengine. Lengo kubwa ni kufahamiana, kuelimisha, na kuuenzi mchango wa watu weusi duniani kote, katika nyanja mbali mbali.
Hiyo jana ilikuwa ni mara ya kwanza kwa bendera ya Tanzania kupepea kwenye tamasha la Afrifest. Baada ya kushiriki matamasha na kujionea wenzetu wanavyotumia fursa kuzitangaza nchi zao, nilijiuliza kwa nini nisitafute bendera ya Tanzania, kama nilivyoeleza katika blogu hii.
Hatimaye, nilifanya uamuzi wa kununua bendera, niwe ninaipeperusha kwenye matamasha ninayoshiriki, maadam fursa zipo. Hapo kushoto naonekana na binti zangu Assumpta na Zawadi kwenye meza yetu, hiyo jana.
Sawa na kuweka vitabu mezani katika tamasha, ambavyo huwavutia watu waje kuulizia habari zake, sawa na kutundika bendera ya kampuni yangu ya Africonexion: Cultural Consultants, ambayo nayo huwavutia watu waje kuulizia maana ya Africonexion, bendera hiyo nayo ni kivutio na kianzio cha mazungumzo kuhusu Tanzania.
Miaka yote, nimekuwa nikishiriki matamasha chini ya kivuli cha kampuni yangu ya Africonexion: Cultural Consultants. Hata hivi katika kuelezea shughuli zangu, sikujiwekea mipaka, kwani utafiti wangu, ufundishaji, uandishi na utoaji ushauri katika masuala ya athari za tofauti za tamaduni, nagusia dunia yote, ikiwemo Tanzania. Lakini kuitundika bendera ya Tanzania kama nilivyofanya jana kunaongeza mwonekano wa nchi katika nchi za dunia.
Kwa kuwa bendera hiyo ilipepea hapo uwanjani siku nzima, kila mtu katika umati wa waliohudhuria tamasha aliiona. Wengi wa waliohudhuria walipiga picha hapo uwanjani, na haikwepeki bendera kuonekana katika baadhi ya picha.
Na Profesa Mbele
Post a Comment