![](https://fbcdn-sphotos-a-a.akamaihd.net/hphotos-ak-xpa1/v/t1.0-9/11947523_10206331796066535_8844530215268803146_n.jpg?oh=a189c1cf1a42fcbbfc417785a38b502c&oe=5681146E&__gda__=1453975928_dfd5b219e60577e3c152d8f41ede9577)
Njau, Kalumekenge Na Ushahidi Wenye Utata!
Ndugu zangu,
Kuna kisa
cha hakimu aliyepata tabu sana katika kuthibitisha ukweli wa urefu wa
mtuhumiwa wa wizi. Mashahidi walikuwa wawili; Njau na Kalumekenge.
Wote wawili, Njau na Kalumekenge, walimwona mtuhumiwa akivunja mlango wa nyumba kabla ya kuingia ndani na kuiba.
Utata wa
ushahidi wao ni kuwa; shahidi Njau alitamka kwa kujiamini mahakamani
kuwa mwizi alikuwa mfupi. Na shahidi Kalumekenge naye aliongea kwa
kujiamini kuwa mwizi alikuwa mrefu.
Huu ni ushahidi wenye utata uliopelekea Bwana Hakimu aumize kichwa kabla hajapata njia ya kutatua utata huo.
Hatimaye ,
hakimu akapata njia ya kufahamu urefu halisi wa mtuhumiwa wa wizi.
Ndio, hakimu alibaini, kuwa kwa vile shahidi Njau ni mrefu, yeye
alimwona mwizi kuwa ni mfupi. Na kwa vile shahidi Kalumekenge ni mfupi,
kwake mwizi huyo alikuwa ni mrefu.
Basi,
Bwana Hakimu alichofanya ni kutafuta wastani wa urefu wa Njau na
Kalumekenge ili kupata urefu halisi wa mtuhumiwa wa wizi ambaye Njau na
Kalumekenge walimwona kwa wakati mmoja.
Kuna
tunachojifunza katika utata na utatuzi wa ushahidi huo. Umuhimu wa
mwanadamu kutokuwa na hulka ya kukurupuka na kuamua mambo. Kuacha
ushabiki. Umuhimu wa kutafakari kwa kina kabla ya kuamua.
Maana,
duniani hapa aliye juu anaweza kuyaona mambo kwa mtazamo wake, na aliye
chini vivyo hivyo. Kwamba wanadamu tunayoyaona tunayaona kwa mitazamo
tofauti. Vivyo hivyo kwa tunayoyasikia na kuyaangalia. Kwamba wanadamu
tuna hulka ya kusikia tunachotaka kusikia, na kuona tunachotaka kuona.
Na mjinga asipojua kuwa yeye ni mjinga unafanyaje?
Ni Neno Fupi La Usiku.
Maggid
Post a Comment