Afisa mmoja katika Chuo Kikuu cha Zimbabwe amesimamishwa kazi baada yake kudaiwa kumpa Rais Robert Mugabe kofia isiyomtosha vyema wakati wa sherehe ya kufuzu kwa wanafunzi.
Msajili msaidizi Ngaatendwe Takawira aliwaaibisha wasimamizi wa chuo kwa kumpa kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 92 kofia ndogo sana, barua yake ya kusimamishwa kazi inasema, kama ilivyonukuliwa na vyombo vya habari huko.
Bi Takawira amekanusha madai hayo.
Inaaminika afisi ya rais haikuwa imewasilisha malalamiko yoyote.
Uamuzi wa kumsimamisha kazi Bi Takawira sana huenda ulifanywa na wasimamizi wa chuo wakitaka kumfurahisha rais na wala si kutokana na hasira kutoka kwa kiongozi huyo, mwandishi wa BBC aliyeko Harare Brian Hungwe anasema.
Wasomi waligundua mara ya kwanza kwa “kofia ya maarifa” haikuwa inamtoshea rais vyema wakati wa mahafali mwaka 2014.
Wakati huo, chuo kikuu kiliagiza kofia mpya ishonwe kwa ajili ya kutumiwa na Bw Mugabe mwaka huu.
Lakini dereva aliyetumwa kuwasilisha kofia mpya ambazo Bw Mugabe alifaa kujaribu kuzivaa aone ni gani ingemtoshea vyema alifukuzwa na walinzi wa afisi ya rais, mdokezi ambaye hakutaka jina lake litajwe ameambia BBC.
Kutokana na hilo, rais hakuweza kupata kofia inayomtosha vyema kabla ya mahafali ya mwaka huu yaliyofanyika Oktoba 2.
Bi Takawira amewasilisha kesi katika mahakama ya leba kupinga uamuzi wa chuo hicho wa kumsimamisha kazi.
BBC SWAHILI
Post a Comment