Wanadiaspora
wameelezea wasiwasi wao kuwa sheria mpya ya Makosa Ya Mtandao iliyoanza
kufanya kazi tarehe mosi mwezi huu nchini Tanzania, huenda ikaishia
Chumbe, imefahamika.
Hayo
yamekuja kwenye kongamano maalum lililoandaliwa na Jumuiya Ya
Wazanzibari Waishio nchini Marekani (ZADIA) kujadili Sheria Mpya ya
Makosa Ya Mtandao na Athari zake Kisiasa.
Wageni
rasmi katika kongamano hilo lililofanyika kwa njia ya simu walikua ni
Mwandishi khabari Bi Salma Said, na Mwanadiplomasia mstaafu Bw. Muhammed
Yussuf Mshamba.
Utata wa Kisheria:
Akizungumza
kwenye kongamano hilo, Bi Salma Said alisema kuwa sheria hii itakuwa na
utata kutokana na jinsi ya mchakato mzima wa kuipitisha ulivyokwenda.
“Sheria imepitishwa kimabavu, kwani wadau wote hawakushirikiswa, pia
ilipitishwa wakati Wabunge wa upinzani wakiwa wametoka Bungeni”
alifafanua Bi Salma na kuongeza kuwa Baraza la Wahariri Tanzania
liliikataa sheria hiyo na kupitisha azimio la kumshauri rais Kikwete
asiitie saini, lakini Mheshimiwa rais aliitia saini.
Kwa
upande wake, Bwana Muhammed Yussuf Mshamba ambaye pia ni Kada wa Chama
Cha Mapinduzi (CCM), alielezea wasiwasi wake juu ya uwezekano wa sheria
hiyo kutekelezeka kwa vile mfumo uliotumika kuiptisha haukukidhi haja.
Akizungumza
katika kongamano hilo, Bwana Mshamba ambaye aliwahi kuwa mtia nia wa
kuwania urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM alisema “Sharia ile
ilipitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini Zanzibar
hawakupata nafasi ya kuiangalia”.
“Kwa
mujibu wa kifungu cha 234 cha Katiba ya Zanzibar, sharia zote
zinazopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ambazo
zinatakiwa kutumika Zanzibar na Bara, kwa mujibu wa kipengele kile ni
lazima Baraza la Wawakilishi la Zanzibar lipewe nafasi ya kuziangalia”.
Alisema
Bwana Mshamba na kuongeza kuwa, sheria ile ilipitishwa wakati Baraza la
Wawakilishi limeshavunjwa na hakukuwa na njia ya kuliitisha angalau kwa
kikao cha dharura ili kuweza kuijadili.
Kutokana
na hali hiyo, Bwana Mshamba alisema kuwa, sheria ile kwa sasa haiwezi
kutekelezeka Zanzibar mpaka Baraza jipya la Wawakilishi
litakapochaguliwa na kuipitia.
Alielezea
sheria hiyo huenda ikapta upinzani katika Baraza jipya kwa vile mambo
yaliyomo ndaniyake yana utata. “Tunajua kuwa swala la mawasiliano, ni
swala la Muungano, lakini je ni kwa kiasi gani? Je swala la mtandao
linaingia?” Alihoji mwanasiasa huyo, na kuongeza “Kwa mujibu
nilivyoelewa, sharia ile ina mambo ya faragha, na Wazanzibari wanayo
faragha yao, na wana mambo yao wanataka wayashughulikie wenyewe”
Alitoa
wito kwa pande zote kukaa tena na kuipitia na kuijadili sheria hiyo ili
kweza kukidhi haja ya kisheria na kuweza kutekelezeka bila kuleta
madhara.
Kutokana
na utata huo wa kisheria, Mwenyekiti wa Jumiya ya Watanzania katika jiji
la Dallas Bwana Ben Kazora, alihoji uwezekano wa kuwakamata washukiwa
wa makosa mtandao ikiwa sheria yenyewe haiwezi kutumika Zanzibar.
Ni sheria
zipi zitakazotumika kuwakamata watuhumiwa, za Tanzania, za nchi
watuhimiwa walizo au sheria za kimataifa za mtandao?’ alihoji Bwana
Kazora.
Uwezo Wa Kitaaluma
Licha ya
serikali ya Tanzania kujipiga kifua kukhusu uwezo wake wa kusimamia
sheria mpya ya Makosa ya Mtandao, washiriki katika kongamano hilo
walielezea wasiwasi wao kuwa Tanzania ina uwezo mdogo kiteknolojia
kuweza kuisimamia na kuitekeleza sheria hiyo kiutaalamu bila kuleta
madhara kwa jamii.
Akichangia
mada hiyo, mtaalamu wa sayansi ya kompyuta Dk Hassan Omar Ali, alisema
kuwa Tanzania ina uwezo mdogo kiteknolojia kuweza kufuatilia kesi za
aina hiyo, na hivyo kuna uwezekano wa watu kubambikizwa kesi na wakawa
hawana uwezo wa kujitetea.
“Kama
mnavyofahamu, mtu unawekwa ndani unaambiwa uchunguzi bado unaendelea,
kwa mambo ambayo tayari tunayaweza, uchunguzi unaendelea kwa miaka,
sikwambii kwa mambo ambayo hatuyawezi sasa hivi” alitoa changamoto Dk
Hassan aliyeandika kitabu cha “Kompyuta: Jifunze na Ielewe”
Msomi
huyo aliyewahi kuandika makala maarufu chini ya kichwa cha maneno:
“mawasiliano ya mtandao hayana siri”, alionya kuwa uwezekano wa mtu
kuweza kukamatwa kwa makosa ya kimtandao upo, ispokuwa tu kwa Tanzania
uwezo wake wa kiutaalamu na kifedha ni mdogo.
Mbali na
khofu ya upungufu wa wataalamu wa maswala ya mtandao, wanadiaspora pia
walielezea wasi wasi wao juu ya upungufu wa wataalamu wa sheria za
mitandao nchini Tanzania.
Akitoa
hoja katika kongamano hilo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watanzania katika
jiji la Dallas Bwana Ben Kazora, alielezea khofu yake kuwa upungufu wa
wataalamu wa fani hiyo huenda ukaleta athari mbaya katika utekelezaji wa
sheria hiyo.
“Je
wataalamu wetu wako tayari kusimamia sheria hii?” Alihoji Bwana Kazora,
na kuelezea khofu yake kuwa huenda swala hili likawa limechochewa
kisisasa.
Kutumiwa vibaya sheria ya Mtandao.
Kwa
upande mwengine, wazungumzaji katika kongamano hilo walielezea dukuduku
lao kuwa sheria ya mtandao huenda ikatumika vibaya kwa malengo ya
kisiasa au chuki binafsi.
Akifafanua
baadhi ya vipengele vilivyomo katika sheria hiyo, Bi Salma Said ambaye
pia ni mwanaharakati za kijamii, alisema kimantiki tunahitaji sheria
kama hii kudhibiti matumizi mabaya ya mtandao, ispkuwa yaliyomo ndani
yake yana utata.
“Katika
ile sheria, kuna kipengele kinasema, polisi akikushuku tu anaweza
kukwambia wende ukawasilishe simu yako Polisi, tena si kwa amri ya
mahkama, ni yeye tu askari” alilalamika Bi Salma, na kuongeza kuwa, simu
itaakapofika polisi haki ya faragha inapotea, kwani hujui ni nini
kitakachopekuliwa katika simu yako.
Kutokana
na hali hiyo, kuna uwezekano wa polisi kuitumia vibaya sheria hiyo ili
kumtia mtu adabu kutokana na chuki binafsi, alionya Bi Salma.
Akijibu
swali lililoulizwa kuhusu iwapo Bunge Maalum la Katiba lilitilia maanani
maswala ya faragha, enzi za mtandao na kumlinda mwananchi dhidi ya
ubabe wa Dola, Bi Salma ambaye alikuwa ni mnjumbe wa Bunge hilo alisema
“swala la uhuru wa faragha tulilijadili katika Bunge la Katiba, ingawaje
hatukwenda ndani kuhusu mambo ya mtandao”, na kuongeza kuwa Katiba
imeweka wazi haki zote za raia, na haki za uhuru wa faragha zimo kwenye
rasimu zote za Tume ya Jaji Warioba.
Kwa
upande wake, akijibu swali hilo, Bwana Muhammed Yussuf Mshamba ambaye
alikuwa mjumbe wa Tume ya Jaji Warioba iliyokusanya maoni ya wananchi na
kuandaa rasimu ya Katiba Mpya alisema “Katiba hata ya sasa inalinda
haki zote za kiraia, lakini serikali imekuwa na desturi ya kupitisha
sharia zinazokwenda kinyume na Katiba”.
Alifafanua
kuwa tatizo si Katiba, bali ni vyombo vinavyosimamia na kutelekeza
Katiba, na kusisitiza imani yake kuwa sheria mpya ya Mtandao itapata
upinzani mkubwa katika Baraza la Wawakilishi.
Naye Dk
Hemed Suleiman, alitahadharisha kuwa sheria hii inairejesha nyuma
Tanzania katika maswala ya kidemokrasia na haki za binadamu.
Akitoa
maoni yake katika kongamano hilo, Dk Suleiman alisema “Nina wasiwasi
kwamba tusipochukua tahadhari, hii sheria huenda ikatumika kidikteta, na
itaturudisha nyuma kutoka hatua tuliyofikia kuelekea kwenye demkrasia
zaidi, na matokeo yake ni kuibana demokrasia zaidi”.
Alitahadharisha dhidi ya uwezekano wa wanasiasa kuitumia vibaya sheria hii kwa ajili ya kuwakandamiza mahasimu zao kisisasa.
Hoja hiyo
pia iliungwa mkono na Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia Na Maendeleo
(CHADEMA) tawi la DMV nchini Marekani, Bwana Kalley Pandukizi ambaye
alielezea wasiwasi wake kuwa sheria hii inaweza kutumika vibaya na
kuwaathiri watu wengi ambao hawana uelewa wa kutosha wa sheria hiyo.
“Wasiwasi
wangu ni kuwa hizi sheria zitakapoanza kutumika zitakuja kuwaathiri
watu ambao hawajui athari za hiyo sheria” alisema Bwana Pandukizi na
kuendelea kuwa “Ndiyo maana baadhi ya wanasiasa wameingia wasiwasi na
kuhofu kuwa sheria hii huenda ikiawa imetengenezwa makhasusi kwa ajili ya
kuweza kuwatisha watu hususan katika harakati hizi za kisiasa
zinazoendelea”. Aidha mwanasiasa huyo wa CHADEMA alionya kuwa sheria
mpya inakwenda kinyume na haki ya uhuru wa vyombo vya khabari na watu
kujieleza.
Elimu Kwa Jamii.
Licha ya
kuikosoa sheria mpya ya Makosa Ya Mtandao, hata hivyo wazungumzaji
katika kongamano hilo liloandaliwa na ZADIA, walikubaliana kuwa iko haja
ya kuwa na sheria kama hiyo, lakini isiwe imetokana na utashi wa
kisiasa. Aidha walisisitiza umuhimu wa sheria kama hiyo kupitia taratibu
zote za kimsingi kabla ya kupelekwa Bungeni. Moja kati ya kasoro za
sheria hizo ni ukosefu wa elimu kwa wadau wote.
“Kwa
kawaida, sharia kabla haijapitishwa hufanyika semina, lakini sidhani
kuwa hilo lilifanyika” Alisema Kada wa CCM, Bwana Muhammed Yussuf
Msahamba, na kuongeza kuwa ikiwa kweli viongozi wetu walikuwa na nia ya
kulinda mila, silka na tamaduni zetu, basi hakukuwa na haja ya sheria
kama hiyo kupitishwa kwa hati ya dharuara.
Akijibu
swali kuhusu nini Wanadiaspora wanaweza kufanya kuhusiana na sheria hii
mpya, Bwana Mshamba alisema kuwa Wanadiaspora wanaweza kutoa mchango
mkubwa kwa kusaidia kutoa elimu kwa jamii kwa kupitia njia mbalimbali.
“Mumanyo
nafasi nzuri ya kuchangia, kwa njia za makongamano kama hili kuzipitia
sharia na kuzichambua” alisema bwana Mshamba na kuongeza kuwa
Wanadispora wanaweza pia kulinganisha sheria za nchi wanazoishi na
kupeleka uzoefu wao nyumbani kwa kushirikiana na Taasisi za kizalendo.
Kwa
upande wake, akijibu swali hilo, Bi Salma Said alisema “Elimu ni muhimu.
Ni vizuri kuipitia sheria na kutoa taaluma kwa jamii”. Na kusisitiza
kuwa mwamko na uelewa kwa jamii yetu ni mdogo khususan katika mswala ya
mitandao ya kijamii na sheria zake.
Post a Comment